Chama cha APPT Maendeleo, kimetangaza rasimi kwamba hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio kutokana na kupoteza imani na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), baada ya kufuta kibabe matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.

APPT kinakuwa chama cha pili kutangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa Machi 20 baada ya Chama kikuu cha upinzani Zanzibar, CUF kutoa tamko lake kama hilo mwezi uliopita.

Msimamo wa APPT ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama hicho, Peter Kuga Mziray katika barua yake kwa (ZEC), ambayo nakala yake ilisambazwa kwa vyombo vya habari Zanzibar.

Mziray alisema njia iliyotumiwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi haikuwa ya kisheria hivyo APPT Maendeleo haitambui kufutwa kwa uchaguzi huo.

Alisema kwa kuwa chama chake hakitambui kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, hakioni sababu ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Zanzibar.

“Tunapenda kuthibitisha kwamba Chama chetu cha APPT Maendeleo hakitashiriki katika uchaguzi huu na tunaitaka ZEC ihakikishe inakiondoa chama chetu katika orodha ya vyama vitakavyoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20 mwaka huu,” alisema.

Mzirai alisema kitendo cha Mwenyekiti wa ZEC kutangaza kufuta matokeo hayo bila kuwashirikisha wadau wa uchaguzi huo, ilikuwa ni dharau dhidi ya wagombea waliokuwa wakishiriki uchaguzi huo.

“Tunajihisi tumedharauliwa sana kwa kitendo ulichofanya Oktoba 28 mwaka 2015 kufuta uchaguzi kama ulivyotangaza wa marudio bila ya kukaa pamoja na wadau wakuu wa uchaguzi,” ilisema taarifa ya Mziray.

“ZEC haiko huru na haiwezi kusimamia uchaguzi wa huru na wa haki Zanzibar.”

Aidha, taarifa ilisema Wazanzibar wameonyesha woga na wasiwasi mwingi tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi kutoka na serikali kuendelea kuimarisha ulinzi mkali mitaani kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Katika matokeo ya uchaguzi yaliyofutwa, APPT Maendeleo hakikusimamisha mgombea wa urais wa Zanzibar hata hivyo.
Pia taarifa ya chama hakueleza kilisimamisha wagombea wangapi wa Uwakilishi na udiwani katikamajimbo 54 ya Unguja na Pemba.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI, 7 Februari 2016

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.