Kampeni ya Rais Xi Jinping wa China ya kupambana na ufisadi mkubwa iliyopewa jina la “chui na nzi” kwa sababu ya kuwalenga kwake maafisa wakubwa na wadogo wa serikali inaonekana sasa kuchukuwa muda mrefu zaidi na ikiwasakama maafisa wa ngazi za juu zaidi kuliko ilivyotegemewa. 

“Chui” ambao hadi sasa wameshanaswa kwenye mtego wa Xi Jinping tangu mwaka jana ni pamoja na Ling Jihua, mshirika wa zamani wa Rais Mstaafu Hu Jintao; Su Rong, aliyekuwa makamo mwenyekiti wa baraza la siasa la chama tawala – chombo cha juu kabisa cha kisiasa nchini China; na Jiang Jiemin, mkuu wa zamani wa kamisheni ya usimamizi wa mali na utawala.

Mwaka jana pekee, Kamisheni Kuu ya Uchunguzi wa Nidhamu ilifanya uchunguzi dhidi ya maafisa 71,748 na hadi sasa 23,646 kati yao wameadhibiwa. Katika siku za karibuni, kampeni hiyo ya kupambana na ufisadi imeanza kuwalenga maafisa wa ngazi za juu jeshini, huku wachambuzi wakitazamia kuwa mwaka huu kampeni hiyo itakwenda mbali zaidi, kwa kuanzia na kuyapeleleza makampuni na mashirika yanayomilikiwa na serikali.

Kuna pia iliyopewa jina la Operesheni Saka Mbwamwitu iliyozinduliwa mwezi Julai mwaka jana, ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kuwaandama maafisa wa serikali walioamua kukimbilia nje ya nchi ndani ya kipindi cha miongo miwili iliyopita. Taasisi ya Masomo ya Sayansi ya Siasa ya China inakisia kuwa kiasi cha maafisa 16,000 hadi 18,000 wameikimbia nchi hiyo na kiasi cha dola bilioni 140 kati ya mwaka 1990 hadi 2008.

Athari za kampeni hii dhidi ya ufisadi zimeanza kuonekana kwenye maisha ya ulimbwende ya vigogo nchini China. Ijumaa iliyopita, jimbo la Macau lililazimika kuahirisha maonyesho ya saa za kifahari yaliyokuwa yafanyike mwezi ujao, kwa sababu ya mahudhurio madogo sana kutokana na vita vya rushwa vinavyoendelea China Bara.

Meneja wa maonyesho hayo, Vincci Tung, aliliambia gazeti la South China Morning Post kwamba hawezi kukanusha ukweli kuwa kupungua kwa kiasi kikubwa kwa wateja wa hadhi ya juu kwenye majumba ya kamari ya Macau kumeathiri mkufu mzima wa tasnia ya anasa, yakiwemo mauzo ya vito vya thamani. Ambapo kamari ni haramu China bara, ni halali Macau, moja ya maeneo tajiri kabisa duniani.

Hong Kong, ambayo ni mkoa mwengine wa China wenye utawala wake wenyewe, nayo pia imeathirika na kampeni hii ya Rais Xi Jinping. Sekta ya udalali wa nyumba inatajwa kuporomoka kwa takribani asilimia 20 kutoka dola milioni 438 mwaka jana, hadi dola milioni 346 mwaka huu. Huku sekta ya mauzo ya kazi za sanaa na vitu vya kale ikishuka kwa asilimia 27 kwa mujibu wa Mark Saunderson, mkurugenzi wa Maonyesho ya Sanaa ya Kisasa ya Asia.

Wakati haya yanaweza kuonekana kuwa matokeo mabaya ya kampeni hii dhidi ya rushwa kwenye uchumi wa China, ukweli ni kwamba ni matokeo muhimu sana na yanayoilinda heshima ya uwekezaji wa ndani na nje wa taifa la pili kwa uchumi mkubwa duniani.

Uongozi wa Rais Xi Jinping umesimamia mageuzi makubwa kwenye mfumo wake wa kisheria, yakiwemo yale yanayolinda haki za watu mmoja mmoja, kuzuia utumiwaji mbaya wa sheria na pia kuifanya mahakama kuwa taasisi inayoendeshwa kitaalamu zaidi.

Hata hivyo, wakati akisonga mbele kwenye mageuzi ya sheria na vita dhidi ya rushwa, kiongozi huyo naye analaumiwa kwa kufuata desturi ile ile na mfumo wa chama kimoja – wa kukifanya Chama tawala cha Kikomunisti kuwa ndicho kilicho juu ya kila kitu.

Mwezi Februari mahakama ya ngazi za juu ya China ilisisitiza kwamba moja ya misingi mitano mikuu ya mageuzi kwenye mfumo wa kisheria wa nchi hiyo ni kuuheshimu uongozi wa chama hicho na kuhakikisha kuwepo kwa malezi sahihi ya kisiasa.

Chanzo: DW

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.