Wakati Ulaya ikiwa inaonekana kubanwa vibaya na mafuriko ya wakimbizi wa Syria, ukweli ni kuwa ni nchi za Mashariki ya Kati ndizo ambazo hadi sasa zimewapokea na kuwahudumia wakimbizi zaidi ya 4,000,000 wa Syria, ingawa Umoja wa Mataifa unasema tatizo hili limechangiwa na ulimwengu ambao umekuwa ukituma fedha chache mno za kuwasaidia wakimbizi hao wabakie huko Mashariki ya Kati. 

Majaaliwa ya mamilioni ya wakimbizi wa Syria inatafsirika kwa nambari mara mbili kwa wiki kwenye jengo la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Wakiwa wanawasilisha ripoti zao za kawaida kwenye kasri hiyo iliyojengwa miaka ya 1930, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanaelezea wakimbizi wangapi wamewasili, wangapi wamekufa maji, na wangapi hawana cha kukila.

Mashirika hayo pia yamekuwa yakitoa takwimu juu ya uwezo wa nchi ambazo zinachukuwa wakimbizi na makisio ya wahamiaji wanaoweza kuhama kutoka maeneo yenye migogoro, na hivyo kuzipa serikali duniani fursa za kutosha kuzuia na kujitayarisha na kile ambacho mara nyingi huelezewa kuwa ni “wimbi” au “mafuriko” ya wakimbizi katika mataifa ya Magharibi.

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ni moja kati ya vyombo hivyo ambavyo sio tu vimekuwa vikitoa wito kwa serikali kubuni sera za kibinaadamu zaidi kwa ajili ya wakimbizi, lakini pia kuwasaidia zaidi ya wakimbizi milioni 4 wa Syria waliokimbilia mataifa ya Mashariki ya Kati.

Msemaji wa UNHCR, Melissa Flemin, anasema kwa maelfu ya wakimbizi hao, maisha yanazidi kuwa magumu, na hivyo miongoni mwao kumekuwa na msemo maarufu: “Sina la kupoteza na nitahatarisha maisha yangu katika kujaribu kufika Ulaya.”

Moja ya sababu za kuongezeka kwa tabia hiyo ni kukosekana kwa michango ya serikali duniani kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na ya misaada, hasa linapohusika suala la msaada wa chakula. Matokeo yake, familia za wakimbizi zimekuwa zikiwatoa watoto wao skuli na kuwapeleka kwenye maeneo ya kufanya kazi, au mitaani kuwa ombaomba au kuwaozesha kwa nguvu ama hata kuwalazimisha kuingia kwenye ukahaba.

Mashirika ya Umoja wa mataifa kawaida huratibu mahitaji ya kifedha katika hali kama hizi za migogoro na kutoa ombi la kimataifa kwa serikali zichangie mabilioni ya dola. Lakini yanachokipata ni fedha chache sana kuliko mafuriko ya fedha kama vile wengine wanavyodhania.

Kwa mfano, mashirika hayo yalikuwa yanasaka dola bilioni 7.4 kwa ajili ya shughuli zao nchini Syria kwa mwaka 2015. Lakini kufikia sasa, ni asilimia 37 ya fedha hizo ndizo ambazo ama zimefika kwenye akaunti zao au kuahidiwa kufika.

Hali haina afadhali kwa mipango yao ya kutumia dola bilioni 4.5 kwa kuwasaidia Wasyria waliokimbilia nchi jirani, ingawa hadi sasa ombi hilo limepata asilimia 41 ya fedha zinazohitajika.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (UNFP) limepunguza au hata kukata kabisa msaada wa chakula kwa wakimbizi nchini Jordan, Lebanon, Uturuki na Misri, mataifa ambayo ndiyo yaliyopokea idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Syria. Nusu ya kiwango cha chakula kilipaswa kukatwa kwa wakimbizi 850,000, dola 13.50 kwa mwezi kwa walioko Lebanon na dola 14 kwa walioko Jordan.

Msemaji wa WFP, Bettina Luescher, anasema makato hayo yaliathiri pia operesheni zao ndani ya Syria, ambako kwa maneno yake: “Familia zilipaswa kula chakula kichache zaidi, na mara chache zaidi.”

Luescher anaongezakuwa “Ni jambo la kutisha pale unapopaswa kumwambia mama anayetaka kuwalisha watoto wake kwamba: ‘Hatuwezi kukusaidia zaidi ya hapa kwa sababu hatujapokea michango ya kutosha. Ukosefu wa fedha za kutosha kwenye makambi ya wakimbizi, kunachangia kwenye hatua ya watu kukimbilia Ulaya.”

Chanzo: DW

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.