Wakati wadau kadhaa wa maswala ya kisiasa wakipinga kile kinachoendelea visiwani Zanzibar, makamishna wawili wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Nassor Khamis na Ayoub Bakar, wameibuika jijini Dar es Salaam leo na kupinga marudio ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Machi kwa madai kuwa uchaguzi huo si halali kulingana na matukio yaliyotokea tangu kufanyika kwa uchaguzi halali wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

Wakizungumza na wanahabari katika hoteli ya Lamada mchana wa leo, makamishna hao wamesema sababu kubwa ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo ni kutokana na kuvurugwa kwa Katiba ya Zanzibar kuanzia kwenye kitendo cha kufuta matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana, ambapo “mwenyekiti wa Tume hiyo hakuwa na mamlaka ya kisheria kufuta uchaguzi huo bila kuwashirikisha makamishna wake.”

Makamishna hao wamesema kuwa sababu nyingine inayowafanya kupinga uchaguzi wa marudio ni kutokana na kukamilika kwa uchaguzi wa mwaka jana ambapo hata “baadhi ya washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani walishakabidhiwa vyeti vyao na mawakala kusaini kuwa uchaguzi huo kuthibitisha kuwa haukuwa na kasoro”, na wakaongeza kuwa wanashangaa kuambiwa baadaye kulikuwa na kasoro nyingi zilizopelekea kuubatilisha.

Makamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Ayoub Bakar (kulia) na Nassor Khamis, wakizungumzia kupinga kwao uchaguzi mkuu wa marudio wa Machi 20.
Makamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Ayoub Bakar (kulia) na Nassor Khamis, wakizungumzia kupinga kwao uchaguzi mkuu wa marudio wa Machi 20.

 

Khamis na Bakar wamesisitiza kuwa kitendo cha kurudia uchaguzi halali, ambacho kinatarajiwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 7 hadi kukamilika kwake, ni matumizi mabaya ya rasilimali za taifa kwani uchaguzi ulishafanyika na “kinachoendelea sasa ni mbinu tu za kuubatilisha uchaguzi halali wa Oktoba 25.”

Kwa mujibu wa makamishna hao, tukio la tarehe 28 Oktoba la kufutwa kwa uchaguzi huo lilitanguliwa na matukio mengine kadhaa ambayo yalionyesha wazi kuwa kuna kikundi cha watu kilichokuwa kinamshauri Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kando ya Tume yake na hivyo hakikuwa maamuzi ya tume nzima.

“Tarehe 26 Oktoba mwaka jana, CCM walileta barua ya malalamiko na kumtaka mwenyekiti na tume kufuta uchaguzi huo, wakati tayari tulishaanza kutoa vyeti kwa washindi. Mwenyekiti aliitisha kikao cha Tume na tulipitisha kwa pamoja kuwa maombi ya CCM hayakuwa na mashiko, hivyo mchakato wa kujumuisha na kutanganza matokeo ulipaswa kuendelea,” amesema Khamis, ambaye kitaaluma na mwanasheria na jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Akisimulia mkasa mzima ulivyokuwa baada ya hapo, Khamis amesema baada ya maamuzi hayo ya Tume, ndipo siku iliyofuata Mwenyekiti Jecha hakufika katika ujumuishaji wa matokeo kwa siku nzima (tarehe 27 Oktoba), na ndipo siku iliyofuatia (tarehe 28 Oktoba) waliposikia kuwa ametangaza kufuta uchaguzi bila kuwashirikisha wajumbe wengine wa Tume hiyo.

“Baada ya hapo, ndipo ofisi yetu ikaanza kuzungukwa na wanajeshi na kuamuriwa tusifanye lolote, huku jaji mkuu wa mahakama ya Zanzibar (na makamu mwenyekiti wa ZEC) naye akiwa amekamatwa na kupekwa polisi.”

Makamishna hao wameweka wazi kuwa kwa matukio kama hayo wanaamini kuwa Tume hiyo imeacha kufanya kazi zake kisheria na sasa inafanya kazi kisiasa jambo ambalo linampotezea sifa Mwenyekiti wa ZEC kuendelea kuiongoza Tume hiyo.

Aidha wamesema kuwa hali iliyopo ndani ya Tume kwa sasa sio hali ya taasisi inayoweza kusimamia uchaguzi wa haki, kwani wajumbe wamekuwa wakipingana kwa kila hoja inayoletwa jambo ambalo linafanya uchaguzi wa marudio kutiliwa mashaka na wajumbe wengi wa Tume hiyo.

“Sisi kama makamishna wa ZEC tunawatolea wito wenzetu kwenye Tume kuacha kufuata mkumbo na badala yake wasimamie sheria inavyosema ili kuwapatia Wazanzibari haki yao ya kikatiba,” wamesema.

NB: Imechukuliwa na kuhaririwa kwa hisani ya blog ya Habari 24

 

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.