Mahusiano kati ya Pakistan na India yamekuwa yakitandwa na shaka na tuhuma baina yao tangu mahasimu hao kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947. Sasa miaka takribani miaka 70 baadaye, kunaonekana fursa mpya za majirani hawa waliowahi kuwa taifa moja kupatana na kuishi kwa masikilizano. 

Mwaka 1947 haukuwa tu mwanzo wa uhuru kwa wananchi wa mataifa hayo, bali pia mwanzo wa uhasama ambao umedumu kwa miongo sita sasa. Ndipo mbegu ya mtafaruku ilipoanza nafasi ya kumea ingawa haikuwa mizizi yake. Ndipo palipoundwa taifa la Pakistan ili kuipatia jamii ya Kiislamu nchi yao wenyewe, uamuzi ambao uliwang’oa mamilioni ya watu kutoka ardhi zao za asili na kupoteza maisha ya maelfu kadhaa waliokuwa wakihama na kuhamia, huku wakikabiliwa na mashambulizi.

Tangu wakati huo, mataifa hayo mawili ya kusini mwa Asia yenye nguvu za kinyuklia, yameshapigana vita vikubwa mara tatu, mbali na mashambulizi ya hapa na pale mipakani. Mara mbili kati ya hizo walipigania umiliki wa jimbo la Kashmir lililo kwenye milima ya Himalaya. Jimbo hilo limegawanywa pande mbili, lakini kila upande unataka liwe lake lote.

Uhasama wa mataifa haya umo takribani kwenye kila jambo – kutoka jeshini hadi michezoni. Mwaka 1998, walifanya majaribio ya nyuklia ya kulipiziana kisasi, sambamba na mashindano ya silaha yasiyotangazwa rasmi. Wakiwa kwenye amani, hushindana kwenye mchezo maarufu wa kriketi, moja za alama zinazowaunganisha walizorithi kutoka mkoloni Muingereza. Lakini hata mechi za kirafiki za mchezo huu, ambao wenyewe wanauchukulia kama dini yao ya pili, mara kadhaa huishia kuwa mapambano ya ngumi.

Mataifa haya mawili yana kitu chengine ambacho kinauwanganisha ingawa hawataki kukitambua, nacho ni mafungamano makubwa ya kilugha na kitamaduni, yanayoakisi karne kadhaa za mafungamano ya kidugu baina yao. Sekta ya filamu ya Bollywood inayotumia lugha ya Kihindi nchini India inakaribiana sana na lugha rasmi ya Kiurdu inayotumiwa kwenye michezo ya televisheni nchini Pakistan.

Mambo hayo yanaifanya fursa ya kufanya biashara kuwa kubwa sana baina yao, lakini ubishani wa kisiasa unaifanya fursa hii kutokuonekana wala kupewa umuhimu. Mara kadhaa, viongozi wa kisiasa hawakubaliani juu ya kipi kinapaswa kujadiliwa mwanzo kwenye mazungumzo yao. Pakistan inataka kuiweka Kashmir kuwa kiini cha mualaka wowote wa kidiplomasia, huku India ikitaka kwanza wajadili ugaidi unaovuuka mipaka kati yao.

Jitihada za mwisho rasmi za kuwakutanisha mahasimu hawa zilikuwa ni mazungumzo ya mwaka 2004, ambayo yalisitishwa baada ya watu wenye silaha kuuvamia mji wa Mumbai mwaka 2008, ambapo serikali ya India inawalaumu wanamgambo wa kundi la Lakshar-e-Taiba lenye makao yake nchini Pakistan. Badala yake, nafasi ya mazungumzo hayo ikaonekana kuchukuliwa na makabiliano ya mara kwa mara ya mpakani, ambayo yanaifanya fursa ya kukaa kitako kuwa mbali zaidi.

Hata hivyo, mapema mwezi Disemba, majirani hao waliamua kurejea kwenye majadiliano, jambo ambalo limezusha tena matumaini kwa mahasimu hao wa Asia ya Kusini. Uamuzi huo ulichukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Sushma Swaraj, aliyetembelea mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, akiwa njiani kuelekea kongamano la nchi za eneo hilo nchini Afghanistan.

Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alikutana na mwenzake wa Pakistan, Nawaz Sharif, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Mabadiliko ya Tabia Nchi mjini Paris mwezi Novemba, huku milango ya kidiplomasia ikifunguka.

Kisha mwishoni mwa 2015, Modi akafanya ziara ya kushitukiza mjini Islamabad akiwa njiani kutokea Moscow na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Sharif, mjini Lahore, kumtakia kheri za siku yake ya kuzaliwa. Kwa wengi, wanaona huu ni mwanzo mwengine mwema kwenye kuirejesha historia njema ya raia wa pande hizo mbili, ambao miongo sita iliyopita walikuwa watu wa taifa moja.

Chanzo: DW

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.