Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, biashara haramu ya pembe za ndovu, dhahabu na mbao yenye thamani ya mabilioni ya dola inachochea vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kuyafadhili makundi ya waasi na kuifaidisha mitandao ya wafanyabiashara kwenye mataifa jirani, na hivyo ni vigumu kuzuwia vita hivyo bila kwanza kuwadhibiti wafanyabiashara hao haramu. 

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inasema makundi ya kihalifu yenye silaha ambayo yana mafungamano na mataifa ya nje yanahusika kwenye utoroshaji wa kiwango kikubwa cha dhahabu, madini, mbao, mkaa, na pembe za ndovu, biashara ambayo kwa mwaka huingiza hadi dola bilioni 1.3.

Mapato yatokanayo na biashara hiyo yanayafadhili makundi 25 yenye silaha, ingawa wengine wanasema makundi hayo yanafikia 49, na ambayo yanachochea migogoro kwenye eneo la mashariki ambalo tangu hapo limeshasambaratishwa kwa vita vya muda mrefu.

Kudhibiti maeneo yenye utajiri wa madini ndiyo sababu kubwa ya kuyaingiza majimbo mawili ya Kivu kwenye miongo kadhaa ya mapigano, yakipoteza maisha na makaazi ya maelfu ya raia.

Martin Kobler, mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo na anayeongoza kikosi cha wanajeshi 20,000 wa kulinda amani, (MONUSCO) anasema laiti rasilimali zinazopotea mikononi mwa makundi ya kigaidi zingelitumika kujenga shule, barabara na hospitali, basi mustakabali wa Wakongo ungelikuwa mzuri sana.

Sehemu kubwa kabisa ya mapato yanayoingia mikononi mwa makundi ya wahalifu wenye silaha inatokana na dhahabu, ambayo huwapatia hadi dola milioni 120 kwa mwaka. Sehemu kubwa ya mapato hayo huchukuliwa na makundi yaliyo nje ya eneo hilo masikini kabisa, huku asilimia mbili ikikisiwa kurudi kwa makundi yenye silaha, yaani dola milioni 13, ambazo hutumika kuchochea zaidi mapigano.

Mapato haya yanawakilisha gharama halisi kwa ajili ya kiasi cha wapiganaji 8,000 wenye silaha kwenye eneo hili kwa mwaka, na pia kuyawezesha makundi yaliyoshindwa au kunyang’anywa silaha, kuibuka tena na hivyo kuendelea kulifanya eneo hilo lisiwe na utulivu, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Makundi ya kihalifu yanatumia fedha yanazopata kuendeleza mkakati wa “wagawe uwatawale” miongoni mwa makundi yenye silaha ili kuhakikisha kuwa hakuna kundi moja peke yake linaloweza kuimiliki na kuiendesha biashara hiyo.

Kongo ina kiwango kikubwa sana cha madini, ikiwemo dhahabu, shaba, chuma, almasi, na hata uranium, lakini sehemu kubwa ya raia wake wanaishi kwenye umasikini wa kutupwa.

“Hebu fikiria, laiti tungeliweza kutumia mamilioni ya dola yanayopotea kwenye mapato yanayoibiwa na makundi ya kihalifu mashariki mwa Kongo kuwalipa walimu, madaktari na kuinua fursa za kibiashara na utalii,” anasema Kobler, akiongeza kwamba “Tunapaswa kuigeuza dhahabu kuwa kodi, na kodi kuwa maendeleo kwa ajili ya mustakabali wa watu.”

Sehemu kubwa ya harakati za waasi zinahusisha udhalilishaji raia na usafirishaji haramu wa maliasili, huku waasi hao wakionekana kuchochewa zaidi katika kujinufaisha kiuchumi basala ya kuwa na ajenda ya kisiasa.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa mitandao ya makundi hayo ya kihalifu ina mashiko yake ndani ya Kongo yenyewe – kama vile Kivu ya Kaskazini na Kusini – na hata mataifa jirani, kama vile Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania.

Kwa mujibu wa UNEP, si madini pekee yaliyo hatarini kwenye vita hivi, bali pia wanyamapori, wakiwemo sokwe wa milimani wanaokutikana katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga na walinzi wa wanyama hao.

Ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, zaidi ya walinzi 200 wameshauawa na kundi ya kihalifu, hasa wanaofanya biashara ya mkaa.

Chanzo: DW

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.