Viongozi wa mataifa ya Pasifiki ya Kusini ya Fiji na New Zealand wanataka kuondosha bendera ya Uingereza kwenye bendera za nchi zao, lakini mipango yao ya kuanzisha bendera mpya zinazoakisi utambulisho wa kitaifa zinakumbana na upinzani mkali wa wananchi.


Waziri Mkuu wa New Zealand, John Key, na kiongozi wa Fiji, Voreqe Bainimarama, wanayataka mataifa yao kuanzisha bendera mpya, wakisema muundo wa bendera za sasa unaakisi zaidi historia ya kikoloni kuliko utambulisho wa jamii zao.

Raia katika mataifa yote mawili tayari wameshawasilisha michoro ya bendera mpya kwa kamati maalum za kitaifa. Bendera ya Fiji yenye mji wa samawati ikiwa na kibendera cha Uingereza kipembeni na nembo yenye taifa iliyochorwa kwa ndizi, muwa, simba na njiwa, ilianza kupepea kwa mata ya kwanza mwaka 1970, nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Muingereza.

Bainimarama anasema kuanzia tarehe 10 Oktoba mwaka huu, siku ya maadhimisho ya uhuru huo, Fiji itaanza kupepea bendera mpya, akihoji kwa nini hadi leo bendera ya nchi hiyo ina simba wa Uingereza na msalaba wa Mtakatifu George.

Lakini upinzani katika hilo ambalo limekuwa na mapinduzi ya kijeshi mara nne tangu mwaka 1987 wanasema hatua ya kubadilisha bendera ya nchi si ya kidemokrasia na wanataka iitishwe kura ya maoni kuamua. Mbunge Ratu Isoa Tikoca anasema alama zilizomo kwenye bendera ya sasa zinaakisi mchango wa kihistoria wa Uingereza kwenye maendeleo ya Fiji. “Alama gani tutakazotumia na zikaakisi kweli historia yetu ya mapinduzi ya kijeshi. Je, tujumuishe bunduki, pingu na vifaru?” , anauliza mbunge huyo wa upinzani.

Serikali ya New Zealand itafanya kura ya maoni kwa awamu mbili kuamua juu ya suala hilo la kuibadilisha bendera yao, ikitarajiwa kutumia takribani dola milioni 20 za Kimarekani. Zidi ya michoro 10,000 iliwasilishwa kwenye ofisi za Mradi wa Bendera Mpya, kabla ya minne kuchaguliwa.

Katika awamu ya kwanza watatakiwa kuchaguwa wanayoipenda kati ya minne hiyo, ambayo yote ina alama asilia za jamii ya Wamaori, wenyeji asilia wa visiwa hivyo. Katika awamu ya pili ya kura ya maoni hapo mwezi Machi 2016, wananchi wataamua ikiwa waibadilishe bendera ya sasa yenye alama ya bendera ya Uingereza kwa bendera mpya au la.

Waziri Mkuu wa New Zealand, John Key, anataka bendera hiyo ibadilishwe na kuwa na urinda wa rangi ya fedha unaowasilisha timu ya taifa ya rugby, All Blacks, lakini wanajeshi wa zamani wanapinga kubadilishwa bendera ambayo wameitumikia.

Chama cha Wanajeshi Wastaafu (RSA) kinapiga kampeni ya kuharibiwa kwa kura ya maoni katika hatua yake ya awali, wakiwataka wapiga kura kuandika “naitaka bendera ya sasa” kwenye karatasi za kura. “Kura hizi za maruhani pia zinahisabiwa kwa hivyo ni njia nzuri ya kuhakikisha sauti za wale wanaopigania bendera yetu zinasikika kwa uwazi katika kila hatua ya mchakato huu,” anasema BJ Clark, rais wa wanajeshi hao wastaafu.

Clark anasema New Zealand ni sawa na Australia, ambayo waziri wake wa mambo ya nje, Julie Bishop, amesema jeshi la nchi yake lina mafungamano makubwa na bendera ya nchi yao ambao pia ina nembo ya bendera ya Uingereza.

Chanzo: DW

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.