HALI ya kisiasa Zanzibar si rafiki tena. Sababu ni kinachofuatia matukio makubwa mawili: Moja, tangazo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) la kutaja 20 Machi kuwa siku ya uchaguzi wa marudio, badala ya ule uliofutwa Oktoba 28, 2015.

Pili, ni tangazo la Chama cha Wananchi (CUF) la kukataa katakata kushiriki uchaguzi huo; uamuzi uliopitishwa Alhamis iliyopita na Baraza Kuu la Uongozi (BKU) la chama hicho.

Kufuta uchaguzi kulikuja kama mbinu ya CCM kuitumia Tume – na kwa kweli ni Mwenyekiti Jecha Salim Jecha – kubaki madarakani kwa kuikatalia CUF kuongoza serikali kwa kutangaziwa ushindi wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 kupitia mgombea wake wa urais, Maalim Seif Shariff Hamad.

Kilichoifikisha hapo Zanzibar ni chuki za kisiasa ndani ya CCM Bila ya shaka mivutano hiyo ya kimaslahi ya Madaraka baina ya Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF imeibua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na inaisukuma kw anguvu Zanzibar kutumbukia kwenye shimo la moto kwa kadri siku zinavyosogea mbele.

Tofauti na mawazo ya wengi kwamba harakati za kisiasa zilizojikita katika mitazamo ya chuki na uhasama zimejenga taswira ya kutoaminiana baina ya viongozi wa vyama vinavyopingana na kumuona Maalim Seif, ambaye ametokana na chama hichohicho cha CCM, kama adui wa kisiasa na wakati huohuo akionekana na kundi kubwa kama mkombozi wa Zanzibar.

Kuna dhana pia kwamba kuzaliwa kwa CUF kumetokana na harakati za watu wa kisiwa cha Pemba pekee za kupinga utawala wa CCM, lakini ukweli washiriki wa harakati hizo ni wananchi wenyewe kutoka Pemba na kisiwa kikuu cha Unguja waliochoshwa na utawala wa CCM.

Waliosaidia harakati hizo kwa lengo la kuing’oa CCM, miongoni mwao ni watu wanne waliokuwa mstari wa mbele watokao Unguja ambao ni Machano Khamis Ali aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Ali Haji Pandu aliyewahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Shaaban Khamis Mloo aliyewahi kuwa Waziri na Katibu wa Mkoa wa CCM Mkoa wa Pwani Tanzania Bara na Khatib Hassan aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Zanzibar na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ambao baada ya
kufukuzwa CCM, walianzisha harakati hadi kuanzisha chama cha upinzani.

Kutoka Pemba, waliojiunga nao walikuwa Soud Yusuf Mgeni aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Mapinduzi, Suleiman Seif aliyekuwa Waziri, Hamad Rashid Mohamed aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano na Mbunge wa kuteuliwa kwa miaka kadhaa na baadae mbunge mchaguliwa Jimbo la Wawi, Pemba.

Pia katika kundi hilo alikuwemo Maalim Seif Hamad aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya CCM.

Kwa kutokuridhiswa na utawala wa CCM, walijiengua waziwazi baada ya kufukuzwa.
Lakini pia walikuwepo wengine wengi waliounga mkono harakati hizo za kupigania maslahi ya Zanzibar na kusimama kidete kukosoa mwenendo wa viongozi wa CCM Bara kuwa unaoziminya haki za Zanzibar kujenga uchumi.

Serikali ya Muungano mpaka leo imebaki na lawama kuwa inatekeleza sera hodhi kwa kila fursa inayoweza kutumiwa kuisaidia Zanzibar. Kwa kuwa Maalim Seif amebainisha kuwa CUF itaendeleza mapambano dhidi ya CCM na kuhakikisha wanachukua dola kuongoza Zanzibar ili kuirudisha hadhi yake mbele ya uso wa dunia.

Lengo pia ilikuwa ni kuwapa mamlaka wananchi ya kuchagua kiongozi wamtakae na akishachaguliwa aongoze serikali. ambae ameporwa ushindi wake katika uchaguzi uliofutwa na kuiwacha Zanzibar katika njia panda na taharuki na uwezekano wa kutokea uvunjifu wa amani. Imejitokeza hofu kubwa Zanzibar kwamba uchaguzi unaorudiwa ambao CUF imeshatangaza kutoshiriki, umelenga tu kuibakisha CCM madarakani, mgombea wake, Dk. Ali Mohamed Shein atatangazwa mshindi piga ua.

Uamuzi huo si tu utavunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kumfanya Dk. Shein kuongoza chini ya mazingira mabaya, yalioyochangiwa na kuivunja Katiba ya Zanzibar na yumkin yakampata yaliyomkuta Dk. Salmin Amour Juma ambaye hakutambuliwa urais wake baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kwa CUF kudai iliporwa ushindi.

Serikali aliyoiunda Dk. Salmin ilitengwa na wafadhili na mashirika ya kimataifa ya misaada kwa kunyimwa misaada huku kukiwa na kumbukumbu za kiongozi huyo kukataa ushauri wa Mwalimu Nyerere wa kuunda Serikali ya pamoja na CUF.

Mbinyo wa kukosa misaada uliifanya serikali ya Zanzibar kwa miaka yote kumi kiasi cha kukosa uwezo wa kulipa wafanyakazi wake mishahara kila mwezi.

Nchi ikakabiliwa na upungufu wa bidhaa za chakula na vifaa vya kutolea huduma za afya.
Kama hayo hayatoshi, Zanzibar ikaendelea kuandamwa na misukosuko ya hujuma na fujo ya kudhoofisha miundombinu ya kiuchumi na kuchafuliwa visima vya maji vijijini kwa kutiwa vinyesi na kusababisha miripuko ya maradhi ya kipindupindu ambayo yamepoteza maisha ya watu zaidi ya 50.

Kwa wakati wote huo, Zanzibar haikuwa na utulivu wa kisiasa na Dk. Salmin alitumia nguvu kubwa za vyombo vya dola kudhibiti hali, lakini alishindwa na kuiwacha Zanzibar na tatizo lile lile la mgogoro wa kisiasa.

Awamu ya Dk. Amani Abeid Karume aliyemfuatia Dk. Salmin iliingia vibaya kwa kurithi sera za mabavu za kupambana na upinzani hadi nae kujikuta katika njia panda kwani miezi mitatu tu baada ya kushika madaraka, askari wa serikali waliua waandamanaji karibu 100 katika mauaji ya Januari 2001, ya kupinga uporaji wa ushindi wa CUF kwenye
uchaguzi wa 2000.

Karume alivyoona hali hiyo mbaya alilegeza msimamo wa mapambano dhidi ya CUF, kwa kuthubutu kufanya maridhiano na Maalim Seif na kuwezesha kubadilishwa Katiba kwa kuingiza kikatiba sharti la kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo iliwezesha kurudisha utulivu Zanzibar.

Alipoingia madarakani Dk. Shein mwaka 2010 na kwa kushirikiana na Maalim Seif walifanikiwa kuiongoza Zanzibar kwa miaka mitano pasina fujo ukiacha zile zilizotokana na kampeni ya kundi la Uamsho ya kupinga Muungano wakati wa kuelekea kutafutwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kufutwa kwa uchaguzi miezi mitatu iliyopita kumeibua upya siasa za chuki kwa kuwa viongozi wahafidhina wa CCM wamemshika miguu Dk. Shein kumdhibiti Jecha asitangaze ushindi wa Maalim Seif uliokuwa dhahiri kwa kuwa asasi zote za uangalizi wa uchaguzi zilishapata matokeo hayo na kusifia kiwango cha usimamizi wa uchaguzi wakisema kimekuwa kizuri kuliko uchaguzi wa 2010.

Tabaani kwa kipindi cha miezi minne kutoka Octoba 28, 2015 ulipofutwa uchaguzi hadi kutangazwa kwa kiitwacho uchaguzi wa marudio, kumeiweka Zanzibar roho juu tena huku joto la kisiasa likipanda kwa kasi.

Kama Dk. Shein alikubali kuachiwa utawala kwa kupitia ZEC mwaka 2010 baada ya uchaguzi uliofanyika kwa amani na usalama, kwa nini sasa asitumie uungwana uleule kutoa haki kwa mwenzake kwa kuiacha ZEC ileile ikatangaza matokeo yaliyobaki hivyo kuleta utulivu? Dk. Shein anayo mamlaka ya kufanya hivyo kwa utawala wa ndani, badala ya kushikilia kuiingiza nchi katika uchaguzi ambao kila mwenye akili nzuri anajua hautasaidia kuleta utulivu bali kupandisha joto la kisiasa na kuzusha mashaka ya usalama wa wananchi.

Kwa kufanya hivyo, Dk. Shein atakuwa amemrahisishia Dk. Magufuli kuchukua hatua imara na za kisheria za kukazia utaratibu wa kikatiba wa kulinda usalama ili kuepusha janga la vikosi pamoja na makundi ya maharamia wanaotii viongozi wa CCM, kuumiza na hata kuwaua raia.

Usiri wa Dk. Shein kuondoa mkwamo kwa njia hiyo unaongeza hatari inayoinyemelea Zanzibar kuwa nchi na sehemu ya Jamhuri ya Muungano isiyotawalika. Mazingira hayo hayatampa nafuu yeyote katika azma ya kuijenga upya Zanzibar na kuipaisha Tanzania kupata uchumi wa kiwango cha kati.

Chanzo: MwanaHalisi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.