Kichwani mwangu najenga picha ya jinsi mazungumzo kati ya Rais John Magufuli na watangulizi wake wawili, Jakaya Kikwete wa awamu ya nne na Benjamin Mkapa wa awamu ya tatu, yalivyokuwa na kile ambacho watatu hao waliambiana na kukubaliana juu ya kadhia ya Zanzibar.

“Sasa nilifanye nini mimi suala la Zanzibar?” Ndivyo ninavyomuona Magufuli akimuuliza Mkapa, ambaye naye kwa ufasaha kabisa akamjibu: “Mimi nilikabidhiwa serikali mbili na Mzee Mwinyi, ya Muungano na ya Zanzibar. Nikahakikisha natumia nguvu zangu na za dola kukabidhisha serikali hizo mbili kwa Kikwete. Wewe umekabidhiwa moja tu, ya Muungano. La kufanya ni kuhakikisha unairejesha na ya pili, ya Zanzibar. Bila ya hivyo, kuna makaburi ya nusu karne yatakuja kufunuka hapa, na harufu yake itatufanya sote tuliowahi kutawala Tanzania pamoja na vyombo vyetu tushindwe kukaa salama.” Kisha Mkapa, ambaye wakati akiwa Amiri Jeshi Mkuu ndipo watu wapatao 60 walipouawa na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, akaondoka na kumuacha Magufuli akipiga hesabu za kutia na kutoa.

Alipomuita Kikwete, suali lake lilikuwa tafauti kidogo: “Mzee kwa nini hukulimaliza suala la Zanzibar na umeondoka na kuniwachia mimi mzigo huu?” Jibu la Kikwete likawa: “Nilitumia nguvu zangu na vyombo vyangu vyote kumzuia Lowassa asikushinde na nikukabidhi serikali ya Muungano. Sasa tumia nguvu na vyombo vyako vyote kumzuia Seif na umkabidhi serikali Shein.”

Kisha Kikwete, ambaye chini ya utawala wake hakufanya chochote cha kuuziba “mpasuko” alioutaja kwenye hotuba yake ya mwanzo bungeni Disemba 2005, akaondoka na kurudi Msola, akimuacha Magufuli na uamuzi mmoja tu – kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kutawala pande zote mbili za Muungano kwa gharama yoyote ile, mbinu ikiwa ni ile ile ya kujifanya hahusiki na masuala ya Zanzibar kijuujuu, lakini chini kwa chini abariki na asaidie hujuma zinazofanikisha azma yao ya pamoja.

Kwa hivyo, wakati Balozi Seif Ali Iddi alipotoka kuzungumza na Rais Magufuli na akaja kusema kuwa amiri jeshi mkuu huyo alikuwa ameamuru kurejewa kwa uchaguzi, hakuwa akidanganya. Ile hujuma ya tarehe 28 Oktoba 2015 ya kuufuta uchaguzi ilifanywa tu kwa jina la Jecha Salim Jecha, lakini kwa maagizo na baraka zote kutoka kwa amiri jeshi mkuu wa wakati huo, kwa mujibu wa Maalim Seif Sharif Hamad. Nilikuwepo Bwawani wakati askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walipokivamia kituo cha kutangazia matokeo, siku moja kabla ya hujuma hiyo ya ‘kuufuta uchaguzi’, ambayo sasa inafahamika wazi kuwa yalikuwa ‘mapinduzi baridi’ dhidi ya matakwa ya wapigakura wa Zanzibar.

Nakisia wakati Maalim Seif alipokwenda kumuona Magufuli kabla ya Balozi Iddi, kiongozi huyo aliyejijengea sifa ya “mtumbua majipu” alijifanya kuwa yuko tayari kufanya kazi na Maalim Seif kama kiongozi wa Zanzibar, alimradi tu pawepo na amani. Hata akajidai kumtupia ndoana Maalim Seif kwamba “najuwa jamaa zangu wa CCM Zanzibar hawawezi kukushinda kwenye uchaguzi, sasa kwa nini usirejee tu uchaguzini, hili jambo tukalimaliza moja kwa moja?”

Unaweza kuithibitisha picha hii inayonijia kichwani mwangu kama una uwezo wa kuunganisha punje moja moja ili kuunda mkufu kamili. Nilikuwepo Zanzibar kabla ya tarehe 25 Oktoba, siku yenyewe ya uchaguzi na wiki takribani mbili baadaye. Kuwa kwangu mwandishi wa shirika la habari la kimataifa kulinipa fursa ya kuingia mwingi, kuzungumza na wengi na, hivyo, kuyashuhudia mengi. Hata kwenye siku ya kwanza kabisa ya kufanyika kwa mazungumzo ya Ikulu, tayari uamuzi ulikwishachukuliwa. Nilijulishwa baadaye kwamba wiki mbili kabla ya mazungumzo hayo kuvunjika rasmi, tayari CCM ilishaingiza makaratasi ya kura kutokea China, hiyo ikimaanisha kuwa tangu awali haikuwa na mbadala mwengine.

Sasa tarehe ya kile kinachoitwa ‘uchaguzi mkuu wa marejeo’ ndio imeshatangazwa na, kinyume na ilivyotazamiwa na wengi, CUF imesema haitoshiriki kwenye ‘uchaguzi’ huo. Uamuzi huu, hapana shaka, umeishitua sana CCM, ambayo ilikwishawekeza pakubwa kwenye kuutumia ‘uchaguzi’ huo kujijengea uhalali wa kubakia madarakani kwa njia ya kura, ambayo kiukweli hauiamini.

Ndiyo, sijateleza. Namaanisha hasa kuwa CCM haiamini kwenye kura, bali inaamini zaidi kwenye matumizi ya vyombo vya dola kujibakisha madarakani. Lakini kwa kuwa siku hizi kura ndiyo njia ya kilimwengu kubakia madarakani, huwa inakwenda vituoni kila baada ya miaka mitano kuuonesha huo ulimwengu kwamba nayo ipo madarakani kwa ridhaa ya wananchi. Tangu awali kabisa, CCM ilishasema serikali isingelipatikana kwa kutumia kikaratasi cha kura. Na wala hilo si la CCM Zanzibar pekee, kama wengine wanavyotaka tuamini, bali hiyo ndiyo akili ya CCM nzima, kwa ujumla wake. Inaamini bullet not ballot (risasi na si kura) kwa kutumia msamiati wa mpambanaji Malcolm X.

Utawala wa Rais Magufuli unatokana na CCM na hivyo una imani hiyo hiyo waliyonayo watangulizi wake, Kikwete na Mkapa. Na la Zanzibar ni suala maalum kwao. Sera yao ya Muungano kuelekea Zanzibar haijawahi kubadilika tangu mwaka 1964. Kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere kwenda kwa Mzee Ali Hassan Mwinyi, kuja kwa Mkapa hadi kwa Kikwete na sasa Magufuli, CCM ni wale wale na mtazamo wao ni ule ule. Ni mtazamo ulio na misingi yake kwenye akili ya mkaliaji dhidi ya mkaliwaji, ambapo mkaliaji huamini kuwa lazima mkaliwaji awe na udhaifu wa kutosha kuweza kukaliwa. Nilisema katika makala yangu iliyotangulia kwamba kuna uhusiano mkubwa sana baina ya kile Indonesia ilichoitendea Timor ya Mashariki au Morocco dhidi ya Sahrawi mwaka 1975 na kile ambacho muongo mmoja nyuma Tanganyika iliitendea Zanzibar.

Hata hivyo, hili halimaanishi kuwa habari ni mbaya tupu. Hapana. Kuna upande mwengine mzuri wa hadithi hii. Nao ni kuwa, kadiri sera ya CCM kuelekea Zanzibar inavyosalia kuwa ni ile ile na akina Magufuli kuwa ni wale wale, Zanzibar nayo inazidi kuwa chura kwenye tumbo la chatu. Uamuzi wa chatu la kummeza chura mzima mzima kwa kudhani kuwa humo tumboni mwake chura huyo angekufa na kuozeana, lilikuwa kosa la kihistoria ambalo linamuandama chatu daima milele.

Mwandishi mmoja wa Kifaransa ambaye nilikutana naye Mjini Unguja tulipokuwa tukiripoti matukio ya uchaguzi mwezi Oktoba, aliniandikia wiki moja baada ya ‘mapinduzi’ ya tarehe 28 Oktoba na kuniambia “Poleni Wazanzibari. Nawasikitikia nyinyi na nchi yenu!” Jibu langu kwake lilikuwa “Ahsante kwa kuonesha kwako kujali, lakini usiipe pole nchi yangu wala watu wangu. Sisi ni wakongwe kwenye masuala kama haya na imara kama Ngome Kongwe. Ni kizazi cha Mwana wa Mwana, Mwinyi Mkuu, na Mkamandume. Ni vitukuu vya waliokuja kwa majahazi, watoto wa wavuvi wa mwambani, makuli wa bandarini, wakulima wa maweni na mabondeni na wakwezi wa minazi mirefu kwenye upepo mkali. Sisi ni wa kudumu. Tutasimama imara baada ya hili na jengine lolote litakalokuja!” Majibu yangu kwake ndiyo yaliyonipelekea kuandika shairi “Wa Daima!” 

Ndiyo. Zanzibar ni ile ile ambayo ilipambana na Mreno katika karne ya 16, ikaja kupambana na Mwarabu na Muingereza kwa pamoja katika karne ya 19 na 20 na ikaanza kupambana na Mtanganyika kwenye karne ya 20 na 21. Itafanya hivyo tena na tena kadiri itakavyopaswa. Sababu ni kuwa uhalisia wa mapambano ya Zanzibar unavuuka mipaka ya siasa za kutaka  madaraka tu na umo, kwa hakika kabisa, ndani ya kiini cha uhuru, mamlaka na uwezo wa kujiamulia. Hilo litabakia hivyo daima milele.

Kitu kimoja tu ndicho ninachokiomba usiku na mchana kwenye mapambano haya – kwamba yaendelee kuwa mapambano yanayotumia njia za amani kufikia lengo na hata siku moja yasije yakaangukia kwenye mtego wa mtawala wa kuyageuza kuwa machafuko na umwagaji damu. Kwa mfano, kwa kuchanganyikiwa kwao hivi sasa watawala wameamua tena kuyafungulia makundi yao ya kihalifu – maarufu kama mazombi – kuingia mitaani na vijijini kupiga na kutesa watu pamoja na kuharibu mali zao. Serikali ya Muungano, kama kawaida yake, imejitia pamba masikioni na miwani ya mbao machoni. Inajifanya haioni wala haisikii hayo yanayotokea. Imekuwa ikifanya hivyo kila mara, kama staili yake ya kuyabariki na kuyalinda madhila wanayoyapata Wazanzibari kwa jina la kuulinda utawala wao. Wazanzibari hawapaswi kuchokozeka wala kujibishana na mazombi haya, si kwa kuwa wao ni watu dhaifu na wanyonge, bali kwa kuwa wao ni watu wenye dhamira kubwa na maono ya mbali zaidi ya pale mazombi na waliowatuma wanapoweza kupaona.

Siku tatu baada ya Rais Magufuli kukutana na Maalim Seif mwezi Disemba na wawili hao kuelezea matumaini yao ya kukwamuka mkwamo wa uchaguzi, niliandika kwamba kulikuwa na makosa matatu ya watangulizi wake ambayo Rais Magufuli angelipaswa kuyaepuka kama kweli anataka suluhisho la kudumu visiwani Zanzibar, ambayo unafiki, kukosa uthubutu na kiburi. Haya ni mambo ambayo yamewakabili Wazanzibari kwa miaka yote, lakini kamwe hawakuvunjika moyo. Badala yake, duara la wale wanaopingana na siasa za mkaliaji limekuwa likitanuka siku hadi siku na sio kufinyika. Maana yake ni kwamba hata pawe na kitisho cha hali gani, bado Zanzibar inaendelea kubakia kuwa ile ile.

One thought on “Magufuli ni wale wale lakini Zanzibar nayo ni ile ile”

  1. Uliyoyaandika si picha ya bahati nasibu bali ni tafakari ya hali ya juu kabisa. Tazama ya juzi alipokwenda Lukuvi kumueleza Magufuli, wa hapa kazi, eti hana uwezo wa kuingilia wanayoyatenda kamati “Huru” za uchaguzi. Tutakuwa tumerogwa kutarajia wazo jengine kutoka kwake. Yalianza wiki iliyopita pale Mutungi kubariki marejeo ya uchaguzi. Usanii mwengine umefanywa hivi juzi tu na yule mzushi wa kuandika makala katika gazeti la Amerika kuchochea chuki za kigaidi dhidi ya Zanzibar. Huyu ni Kinana. Alidai watashinda nakushauri tena wazidishe mikakati. Izara ya kiulimwengu imewafikia. Doh! Kwani wa ndani na nje walishuhudia pigo. Uwanja wamewachiwa wazi. Wenye kuhesabika wamejitoa. Hivyo vyama vya chini ya 1% ni I sey na sisi tumo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.