Ni kweli Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salum Jecha ametangaza kuwa Zanzibar itakuwa na uchaguzi wa marejeo hapo Machi 20 baada ule wa kikatiba na kisheria wa kila miaka mitano yeye mwenyewe kuufuta.

Ni kweli pia Tume ya Uchaguzi ZEC imetangaza ratiba ya uchaguzi huo ambao utakuwa kwa madiwani, Wajumbe wa Baraza la Wawasilishi na pia ule wa Urais wa Zanzibar ukiwa ni uchaguzi wa tano tokea kurejeshwa mfumo wa ushindani wa kisiasa hapo 1992 na chaguzi kufanyika 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Ingawa wengi hatukushangazwa na tangazo la Jecha, kwa sababu nyimbo ya mrejea ilikuwa ikitiwa mahadhi kwa kasi na ikapata waimbaji wake, lakini baadhi yetu tunajiuliza masuala mengi kwamba kwa hali gani uchaguzi ulioitishwa wa marejeo utafanyika?

Pamoja na propaganda na kelele nyingi mimi nina mawazo kuwa uchaguzi huo hautafanyika au tuseme hauwezi kufanyika kwa sababu una makando kando mengi, kwa kutumia lugha ya siku hizi, na kufanyika kwake kutaleta mzozo zaidi kuliko suluhu.

Na Ally Saleh
Na Ally Saleh

Huwa najiuliza wale wanaopigia debe kuwepo na mrejea na wale ambao wanaunga mkono hivi akili zao zimesita kufikiri, au macho yao hayaoni kuwa tunakokwenda siko na kulazimisha ni kuipeleka Zanzibar katika shimo?

Hivi uchaguzi gani utaoweza kufanyika na ukaitwa uchaguzi kwa maana ya sifa za uchaguzi katika hali ambayo hakuna maelewano ya kitaifa na kutomaliza mivutano iliyotokana na Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015?

Hivi ni kwa njia gani utafanyika uchaguzi mwengine ilhali uliomalizika unahojiwa na suala lake bado liko juu kwenye ajenda na kwa maana hiyo utapataje ushawishi wa umma kushiriki uchaguzi katika hali kama hiyo?

Mtu aweza kuwaza na asiwe na makosa hiyo tume ya ZEC inayotaka kusimamia huo uchaguzi wa marejeo inao uhalali wa kufanya hivyo? Jee katika kipindi hiki imepata nafasi ya kujipima na kujiona bado inatosha katika dhamana na dhima hiyo?

ZEC inawezaje au inathubutu vipi kuweka kando kirahisi ( to simply brush aside) madai mazito yanayotokana na Uchaguzi uliofutwa kukiwa na hoja kadhaa za kikatiba na kisheria ambazo majibu yake hayapo kwa sababu yalotolewa hayatoshi?

Hivi ni kwa faida ya nani na ili kipatikane nini ZEC kutangaza tarehe ya Uchaguzi wa marejeo huku pande ambazo chombo hicho imeshindwa kulinda na kusimamia haki zao, zinakutana kujadili vipi kujitoa katika mkwamo ambao zimeingizwa na chombo hicho?

Kushiriki Uchaguzi huja kwa kuwarai wananchi na kuomba ushiriki wao hasa katika nchi yetu ambao kupiga kura si matakwa ya kisheria, bali ni ushawishi wa vyama, ZEC itapangaje uchaguzi huku ikijua kuwa kuna sehemu kubwa ya wapiga kura wanataka waelezewe juu ya hatma ya kura zao walizopiga Oktoba 25?

Hivi Tume kweli, haki ya Mungu, inataraji kuwa CUF italegeza msimamo wake na ije ishiriki uchaguzi ambao unasimamiwa na Tume ile ile ilowapoka ushindi wao kwa kura za ushindi zaidi ya 25,000? Wajumbe wa Tume ya ZEC kweli wanaamini hivyo?

Au kweli ni fikra yenye umadhubuti kuwa vyama vyengine vikishiriki inatosha na uchaguzi utakuwa na uhalali? Kwa hali gani tutafanya uchaguzi bila ya ushiriki wa CUF? Itoshe tu kusema kuwa “madam wamesusa basi sisi twala?”

Hivi ZEC wanaamini uchaguzi urudiwe kwa vyama kuweka wagombea wale wale wa Oktoba ili kurahisisha uchapishaji wa makaratasi ya kupigia kura, ni jambo la busara kwa vyama? Kwani wagombea wa vyama huamuiliwa na ZEC au vyama vyenyewe?

Uchaguzi wa marejeo utafanyika vipi bila ya kampeni kwa vyama kama inavyosema Tume jee hili limekaa vipi? Hii tumeiga wapi au tumeona wapi wakati hata katika chaguzi ndogo za Ubunge au Uwakilishi ni utamaduni wa Zanzibar kuwa kunakuwa na kipindi cha kampeni?

Au ZEC inahimiza Uchaguzi ili kukimbilia Zanzibar isiingie katika kipindi cha kupitisha bajeti kikatiba bila ya kuwa na Serikali na Baraza la Wawakilishi kutimiza masharti hayo? Lakini katika hali gani basi kuweko na mrejeo?

Mrejeo ufanyike vipi wakati hali ya kutokuwepo uhakika wa usalama ipo na inashamiri au tuseme haikuwahi kuondoka tokea kumalizika uchaguzi hadi leo? Mbona imeripotiwa mara kadhaa kuwa makundi ya kihuni ya watu wanaoziba nyuso zao Mazombie na Masoksi yanatisha na kupiga raia hata hivi juzi? Kwa hali gani uchaguzi utafanyika.

Kwa hali gani na kwa faida gani ufanyike uchaguzi wa marejeo wakati wadau wetu wa maendeleo wanasema haki imenyongwa Zanzibar na kwamba katika hili msimamo wao uko wazi kuwa uchaguzi usifanyike na aliyeshinda apewe ushindi wake?

Tutafanyaje uchaguzi wa marejeo tukijua kuwa CCM inawabeba wahafidhina wa Zanzibar ambao wao wenyewe ndio walitayarisha “kifo chao cha kisiasa” kwa sera za ubaguzi, kutotimiza ahadi zao kwa umma japo wanajisifia kutekeleza kwa asilimia nyingi?

Kutakuwaje na uchaguzi wa marejeo wakati ukiwepo itakuwa ni sifa mbovu na doa jeusi kwa Tanzania mbele ya macho ya kimataifa na hata kwa nchi zetu za jirani na tulionao katika jumuia za Afrika Mashariki EAC na Kusini mwa Afrika SADC?

Lakini pia katika hali hii tutafanyaje uchaguzi huku tukijua kunaweza kuwa na fujo ambayo italeta mtafaruku kwa umma lakini pia inaweza ikaleta mtikisiko wa kiuchumi kwa Zanzibar na Tanzania na kuteteresha hali ya kiusalama ya nchi yetu inayosifika kwa amani yake?

Tunanyamazaje sisi viongozi, sisi makundi ya haki za binaadamu, sisi waandishi wa habari, sisi viongozi wa kidini ilhali tunajua hali ya Zanzibar ni rahisi kuripuka na kwamba kinachotokea Zanzibar kinaweza kuwa na athari ya moja kwa moja Tanzania Bara?

Tunakubali vipi uchaguzi wa marejeo kwa kujua kuwa hayo yote yanaweza kutokea? Hapa ndipo ambapo bado nafikiri kuwa Rais Magufuli bado ana wajibu wa kuchukua uongozi kulisimamia jambo hili.

Mimi sikubaliani kabisa na wanaosema kuwa amefungwa mikono kisheria. Kama kisheria iko hivyo jee kisiasa na jee kiuongozi? Au ndio anaamini alichokifanya kimetosha na amenyanyua mikono? Au ameamua kuungano na mtizamo na msimamo wa chama chake na liwalo na liwe?

Tunapenda sana iwepo amani Zanzibar na kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya uamuzi kuwa uchaguzi urejewe ila mimi nitaendelea kujiuliza uchaguzi huo utarudiwa kwa hali ipi? Hii tulonayo kweli inafaa kushikilia jambo hilo?

NB: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mtanzania la tarehe 3 Februari 2016.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.