YANAYOJIRI sasa Zanzibar yamenifanya niyakumbuke ya Algeria ya miaka ya 1990, ingawa hali za nchi hizo mbili, pamoja na siasa zao, ni tofauti. Juu ya tofauti hizo, kuna ya kujifunza kutoka Algeria au labda niseme kuna moja kubwa la Tanzania kujifunza kutoka nchi hiyo rafiki.

Binafsi nililiona joto la kisiasa Algeria likizidi kupanda katika miaka ya mwisho ya 1980 nilipowashuhudia vijana wakizidi kuzipinga siasa za chama kinachotawala cha Front de Libération Nationale (FLN). Chama hicho kilichopigana na wakoloni wa Kifaransa kuikomboa Algeria kimekuwa kikitawala tangu nchi hiyo ipate uhuru 1962, mwaka mmoja baada ya Tanganyika.

Kufikia miaka ya 1980 ufisadi miongoni mwa watawala wa Algeria ulikuwa umekithiri kupita kiasi, hususan wale watokao sehemu ya mashariki mwa nchi hiyo. Wao wakiishi maisha ya raha lakini kwa Waalgeria wengi maisha yao yalikuwa magumu. Asilimia 45 ya wakazi wa mijini walikuwa hawana ajira, na miongoni mwao vijana ndio waliokuwa wengi.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Siku hizo ukiingia misikitini mjini Algiers ulikuwa ukiwakuta wengi wa vijana hao wakikaa katika vikundi vikundi vya duara. Vijana hao wa mjini wakiitwa “hittistes”. Ni vijana waliokuwa masikini, waliokuwa hawana ajira wala tamaa au fursa ya kuajiriwa. Duru zao misikitini zikijadili falsafa ya maisha, zikichanganya dini na siasa.

Mambo yalianza kwenda kombo Oktoba 1988. Mwezi huo maelfu kwa maelfu ya vijana hao wa mjini walimiminika barabarani na kuziteka barabara hizo. Majeshi ya usalama yaliwatwanga kwa risasi na kuwaua mia kadhaa ya vijana hao, lakini hawakutishika, hawakutetereka. Waliendelea kufanya fujo mitaani na kuitia kizaazaa serikali.

Ghasia hizo ziliitikisa serikali kiasi cha kuifanya ilazimike kuibadili Katiba ya nchi Novemba 3, 1988 na kuvihalalisha vyama vingine vya siasa. Algeria ikaingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Mojawapo ya vyama hivyo kilikuwa chama cha Front islamique du salut(FIS) au kwa jina lake rasmi la Kiarabu “al-Jabhah al-Islāmiyah lil-Inqādh”, kilichosajiliwa Septemba 1989.

Juni 12, 1990 kulifanywa uchaguzi wa serikali za mitaa; huo ulikuwa uchaguzi wa mwanzo kabisa uliokuwa huru na wa haki nchini Algeria. Chama cha FIS kilishinda kwa asilimia 54 ya kura zote zilizopigwa. Chama cha serikali cha FLN kilianguka vibaya sana.
Mwaka uliofuatia palipofanywa uchaguzi wa Bunge, chama cha FIS kiliibuka tena mshindi katika duru ya mwanzo ya uchaguzi huo Desemba 28, 1991. FIS kilipata viti 118 nakile cha FLN kilipata viti 16 tu.

Duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge ilikuwa ifanywe Januari 13, 1992 na hapakuwa na shaka yoyote kwamba chama cha FIS kingeibuka mshindi wa uchaguzi huo. Ilionekana kama demokrasia inafanya kazi. Lakini, na hapa ndipo Zanzibar ya leo inavyonikumbusha ya Algeria ya siku hizo, siku moja kabla ya uchaguzi Jeshi la Algeria lilifanya kama alivyofanya Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Jeshi liliufuta mchakato mzima wa uchaguzi.

Yaliyofuata baadaye hayasemeki. Nchi ilitumbukia katika janga la mauaji. Pakafuata vile viitwavyo vita vichafu (“la sale guerre”), vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi na wafuasi wa upinzani vilivyodumu kwa miaka minane.

Haijulikani hasa ni watu wangapi waliouliwa katika kipindi cha kutoka 1991 hadi 1999. Wa upande wa serikali wakisema watu 100,000 waliuliwa, wengine wanasema idadi halisi ilipindukia 200,000. Kuna waliouliwa kwa kipigwa risasi na kuna waliokuwa wakichinjwa. Watu wengine wapatao 15,000 walitekwa nyara na hadi leo hawajulikani walipo. Wamepotea.

Chanzo cha yote hayo ni kukiukwa Katiba na kuihalifu sheria kwa kuufuta uchaguzi uliokuwa halali.

Hatuombi hayo yatokee kwetu lakini siasa chafu zinazoendelezwa Zanzibar zinaweza mara moja zikaitumbukiza nchi katika janga la misiba. Hatutaki kuona hata tone moja la damu likimwaika seuze michirizi ya damu.

Si Algeria pekee lakini kuna mifano mingine duniani ambapo vitendo vya ukiukwaji wa Katiba baadaye viliangamiza nchi. Nchini Misri, kwa mfano, jeshi liliingilia kati 2013 na kumpindua Rais Mohamed Morsi aliyekuwa amechaguliwa kihalali.

Bila ya shaka, Algeria na Misri, ingawa ni nchi jirani, zina historia tofauti kama zilivyo Zanzibar na Algeria au Zanzibar na Misri. Hata hivyo, Wamisri walipaswa kujifunza kutokana na yaliyotokea Algeria na kuzipima athari za ukiukwaji wa Katiba. Lakini haikufanya hivyo. Zanzibar, kwa upande wake, ilipaswa kujifunza kutokanchi zote hizo mbili. Lakini nayo haijajifunza kitu.

Misri ilishindwa kujifunza kutoka Algeria na ndio maana hadi leo nchi hiyo inaendelea kukabiliwa na misukosuko ambayo ukiyachunguza utaona kwamba asili yake inatokana na hatua hiyo ya majeshi ya kuikiuka Katiba na kumpindua Rais Morsi 2013.
Tunashukuru kwamba wapinzani wa Zanzibar hawajachokozeka na wamebakia watulivu juu ya mbinu zote zilizofanywa, na zinazoendelea kufanywa, kuwapandisha jazba. Mara tu baada ya Jecha kutangaza kwamba uchaguzi mzima wa Zanzibar utarudiwa Machi 20, 2016 vikosi vya majeshi, ambavyo hupewa amri na Serikali ya Muungano, vilisambazwa mjini Unguja.

Kulikuwa na ripoti mwishoni mwa wiki iliyopita ya watu kubughudhiwa na hata kupigwa na wanajeshi bila ya sababu za maana.
Wazanzibari wanaamini kwamba vitendo hivyo ni uthibitisho wa nia na njama za Serikali ya Muungano za kuidhibiti Zanzibar isifurukute. Kwa wenye kutumia akili zao dhana hizo si ngeni. Yote hayo yalikuwa wazi kwao toka zamani kutokana na waliyokuwa wakiyasema akina Waziri William Lukuvi, kanisani; na Samuel Sitta, Uingereza na zaidi yaliyokuwa yakisemwa na hayati Asha Bakari, aliyefariki Dubai wiki iliyopita na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar.

Sijui kama ni sadfa tu kwamba siku aliyozikwa marehemu huyo ilikuwa ndio siku Jecha alipotangaza tarehe ya ule anaouita uchaguzi wa marudio. Hizi inawezekana ni salamu kwa Wazanzibari kwamba aliyoyasema bibi huyu ndio sera hai ya CCM, ingawa mwenyewe aliyeinadi katika Bunge la Katiba, akisikilizwa na viongozi wote wa nchi, na kupigiwa makofi, ameshatangulia mbele ya haki.

Lililojitokeza zaidi hapa, na kwa ithibati ya nguvu, ni kwamba sio CCM-Zanzibar pekee inayokataa pasiwepo demokrasi Zanzibar. Hii ni sera ya CCM na serikali zake mbili, ya Muungano na ile ya Zanzibar.

Bahati mbaya, na huu ndio ukweli, Zanzibar imekaa kama yatima katika siasa za madola makuu, hasa ukizingatia vita wanavyopigwa Waislamu duniani kote. Ukweli ni kwamba Zanzibar ni nchi isiyo na mtetezi. Inabuniwa, kusingiziwa na kupakazwa uongo na ulimwengu unakuwa tayari kuamini.

Inatosha kutangazwa, kama walivyotangaza baadhi ya wakuu wa CCM, kwamba Zanzibar isiachiwe kuwa na serikali isiyo ya CCM kwa sababu ikiwa hivyo itauvunja Muungano, watarudi “masultani” kutawala au kutaanzishwa dola ya Kiislamu au kwamba Zanzibarinafuga magaidi. Propaganda ovu kama hizi zinasambazwa hata nje ya nchi kwa sauti za chini na baadhi ya mabalozi wa Tanzania, hususan na mmoja aliye katika dola kubwa duniani.

Ukweli hasa hawausemi kwamba yaliyotokea Zanzibar ya kufutwa uchaguzini mapinduzi. Ni sawa nayaliyotokea Algeria kiliposhinda chama cha FIS na jeshi likaingilia kati na kusema “ajwar”, hakuna uchaguzi.

Wanaojiita watetezi wa demokrasia walikaa kimya yalipotokea hayo Algeria, kama wakaavyo kimya kwa haya ya Zanzibar. Kwa ya kwetu msamiati umegeuzwa na “mapinduzi” yameitwa“mgogoro” na Wazanzibari walitakiwa kuzungumza wenyewe kwa wenyewe kufikia muwafaka. Suala hili halionekani kuwa nisuala la serikali ya Muungano.

Dhulma wanayofanyiwa wananchi wa moja ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haimhusuRais wa Muungano, Dk. John Magufuli, kuingilia kati. Amewaachia Wazanzibari matatizo yao wenyewe. Lakini, wakati huo huo, akiwa Amiri Jeshi wa majeshi ya Serikali ya Muungano anaona ni sawa kutumia nguvu za dola dhidi ya wanyonge. Anaona kuwa hilo ndilo jukumu lake na ndio maana linatekelezwa kwa kasi kubwa.

Serikali ya Muungano haijali nainaringa kwa sababuinaamini kuwa ni moja kati ya vipenzi vya nchi za Magharibi na, kwa hivyo, haina wasiwasi. Kweli imetikisika kidogo kwa kunyimwa misaada na shirika la serikali ya Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) na kweli ina wasiwasi kwamba nchi nyingine, zikiwa pamoja na zile za Muungano wa Ulaya (EU), zinaweza nazo zikaiwekea vikwazo Tanzania lakini inaamini kwamba itaweza kuendelea kudanganya kwa propaganda zake na hivyo kupata afueni baadaye.

Juu ya hayo, kuna dalili kwamba serikali ya Tanzania itakuwa inajidanganya yenyewe ikifikiri hivyo. Si hayo tu lakini safari hii serikali haitovutana na madola ya nje peke yao. Itakabiliwa na changamoto kubwa pia bungeni kutoka vyama vya siasa vilivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Na kuna wanaojiandaa kulifikisha suala hili katika Mahakama Kuu ya Dunia (ICJ) pamoja na kuwafungulia mashtaka kwenye Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) baadhi ya viongozi wa Zanzibar na wa Bara endapo mapinduzi ya Jecha yatakuwa sababu ya kumwagika damu.

TANBIHI: Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema katika toleo Na. 442 la tarehe 27 Januari 2016. Mwandishi anapatikana kwa anwani ya barua-pepe ya ahmed@ahmedrajab.com.

One thought on “Yatima wa kimataifa ni mzigo wa Magufuli”

  1. Kuna mwanaharakati mmoja veteran na mchambuzi wa mambo ya siasa ya Zanzibar aliwahi kuniambia kabla ya uchaguzi huu wa Jecha maneno ambayo nahisi sasa Wazanzibari wapo katika uhalisia wake. Alisema: “Zanzibaris should pray for the BEST and prepare for the WORST”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.