Katika makala hii, nakusudia kupitia machache katika maneno ya hekima na busara yaliyowahi kusemwa na wanafikara na wanaharakati wa ukombozi duniani kuhusu uhalisia wa saikolojia ya mkandamizaji na mkandamizwaji. Kupitia tafakuri hii nakusudia kuwatia moyo Wazanzibari kwamba wamefika wakati wametambua namna ya kujinasua kutoka makucha ya madhalimu baada ya kupiga kura kidemokrasia kuwakataa na kisha wakaendelea kukataa kuingizwa kwenye mtego wa vurugu na machafuko unaotegeshwa na madhalimu hao.

Pamoja na yote yanayoendelea katika siasa za Zanzibar, naamini kwa dhati kwamba mara hii somo la kidemokrasia litasimamishwa kwa nguvu ya umma na kwa njia za amani, kwani wananchi ndio waamuzi wa mwisho juu ya nani awatawale na namna gani watawaliwe. Hii ni kinyume kabisa na kasumba na vitisho vya walafi wachache wa madaraka na vibaraka wao wanaojaribu kuuaminisha umma kwamba wao walipewa hatimiliki ya nchi na waliusiwa wasiitoe kwa vikaratasi vya kura, na kwamba nguvu zao za mizinga na vifaru daima zitakuwa juu ya nguvu za kura halali zinazowakataa.

Ukimya na msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakati wananchi wa Zanzibar wakiwa katika taharuki kubwa na hofu ya umwagaji damu kutokana na ubakwaji wa demokrasia, jirani yake na mshirika wake katika Muungano na ambaye ndiye hasa “Muungano” wenyewe, ameamua kukaa kimya kwa kutochukua hatua za kukomesha uhuni unaofanywa na kikundi cha watu wachache wanaong’ang’ania madaraka. Kilicho kibaya zaidi ni kwamba kiuhalisia wananchi wa Zanzibar wanajua kikundi hiki kinawekwa na kuendekezwa na kupewa nguvu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wazanzibari wanapoona silaha nzito nzito za kijeshi zikiingizwa katika visiwa vyao wakati wa uchaguzi, wanajeshi wakimwagwa kila eneo la miji yao kwa kisingizio cha kulinda amani, na huku vikosi vya kihalifu vilivyoundwa na chama tawala vikiwafanyia maudhi na udhalilishaji usio na mwisho, wanaelewa fika kuwa bado Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hajataka wajiamulie mustakabali wao na nchi yao kupitia kisanduku cha kura. Hii ndio sababu kuu kwa nini kadri siku zinavyosonga mbele Wazanzibari wanazidi kuukataa Muungano. Walianza kwa kushauri marekebisho ya mfumo na utatuzi wa kero lakini wakapuuzwa, wakataka Muungano wa Mkataba lakini wakabezwa, na mwisho wakasema “hebu tuacheni tupumue!” lakini wakakandamizwa.

Kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa Tanzania Bara kuonesha wanaheshimu kila kinachoamuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika wakati huu ambao serikali hiyo haina hata uhalali wa kuwepo madarakani, ni za kejeli na za kuwadhihaki Wazanzibari. Katika muktadha huu, yale maneno maarufu aliyowahi kuyasema mwanadiplomasia na mpiganiaji haki wa Afrika Kusini, Desmond Tutu, yanaakisi namna Wazanzibari wanavyojihisi juu ya unafiki huu. Askofu Tutu aliwahi kusema “ukijifanya huegemei upande wowote wakati unaona uonevu unaendelea ,maana yake umechagua kumuunga mkono anayeonea. Ikiwa tembo ameweka mguu wake juu ya mkia wa panya na wewe unabaki kusema huegemei upande wowote, panya hatakuelewa kwa msimamo wako huo”.

Hata kama tukichukulia kuwa jirani zetu viongozi wa Tanganyika wana nia njema na Zanzibar, swali linabaki kwa nini wakae kimya mbele ya uvunjifu wa haki ulio wazi? Kama kuna mtu ana haki na wajibu zaidi kuhakikisha Zanzibar ipo salama wakati huu wa mkwamo wa kisiasa, basi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tena si kwa maslahi tu ya ujirani mwema, bali kwa wajibu wake kama Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Kiongozi Mkuu wa Dola iitwayo Tanzania.

Martin Luther King, mpigania haki za watu weusi Marekani, naye pia aliwahi kututanabahisha kwamba “janga kubwa zaidi sio ukandamizaji au ukatili ufanywao na watu waovu, bali in ule ukimya wa watu wema kuhusu dhulma hiyo.” Kinachoushangaza ulimwengu ni kwamba Rais Magufuli ameuona mgogoro wa Burundi kwa Pierre Nkurunziza ni muhimu zaidi kuupatia ufumbuzi, wakati ndani kwake hali si shwari.

Yawezekana baadhi ya ndugu zetu wa maeneo mengine ya Tanzania hawaoni haja ya kukemea hili kwa kwa sababu wapo salama na mbali na Zanzibar na, hivyo, hawatafikwa na yale yanayowafika Wazanzibari, lakini ni vyema wakakumbuka kwamba kinachoendelea Zanzibar kinawahusu moja kwa moja, kama vile asemavyo mwanafikara Thomas Paine kuwa “yoyote ambaye anatamani kulinda uhuru wake, ni lazima amlinde hata adui yake kutokana na dhulma; kwa sababu ikiwa atakiuka wajibu huu, anaandaa mazingira ya yeye kufikwa na mfano wa yale yale (yanayomkumba adui yake kwa sasa).”

Kuna mifano halisi na ya wazi kwenye hili. Madhila yaliyokuwa yakiwafika Wapemba kila baada ya uchaguzi tokea uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995 kwa kuadhibiwa kwa kuikataa CCM na utawala wa kimamluki wa Zanzibar, kwa muda mrefu yalionekana kama kwamba ni mambo ya hadithini, si uhalisia. Sasa hivi wazi wazi bila hata kificho yanawafika Wazanzibari wa Unguja, na pia ubeberu wa CCM umeshabainika hata Tanzania Bara. Wanaharakati waliokwenda kinyume na mfumo tawala wameng’olewa meno kwa pakari, wameuwawa kikatili, na wengineo wamehujumiwa kwa kila aina ya hujuma. Sasa imefika wakati hata wabunge ambao wamepewa “kinga na upendeleo maalum” chini ya sheria za nchi, wanadhalilishwa ndani ya Bunge wakitolewa kwa mbwa na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia kwa sababu tu wamepaza sauti zao kukemea uovu.

Serikali ya Rais Magufuli inasimamia mwenendo huo wa kidikteta na haijali chochote kile alimradi tu chama tawala kinalinda ajenda yake. Hili linasaidia kwa upande mwengine kuwaonesha wenzetu wa Bara kwamba CCM haina sumile kwenye upapiaji wake wa madaraka. Inaweza kutenda lolote lile ambalo halifikiriki kwa akili ya kibinaadamu, maana kama alivyosema mwanafalsafa Aristotle: “Akiwa kwenye ubora wake, mwanaadamu ni mnyama utukufu wa hali ya juu, lakini akitenganishwa na sheria na haki, basi anakuwa unyama wa hali ya juu.” Ndivyo CCM ilivyo inapojiona kuwa inakaribia kutenganishwa na madaraka au ushawishi wake kwa umma.

Njia ya kujinasua na ubakwaji wa demokrasia Zanzibar

Njia pekee ya kujinasua ni kuikataa amri ya mkandamizaji na kulazimisha kujitoa kutoka kwenye makucha yake ya dhuluma. Gharama ya uhuru na haki yaweza kuja kwa namna nyingi kama vile mfungwa anavyokataa kula gerezani au akiwa mikononi mwa wahalifu ili kulazimisha haki itendeke. Mfungwa huyu anaweza akawa dhaifu kupitia kiasi ikashindikana hata kuendeleza kumtesa kwa sababu nako kutamtoa uhai wake. Kwa kuwa mfungwa ni sehemu muhimu ya uhai wa magereza na au nyenzo muhimu kwa wahalifu waliomteka kupata wanachokitaka, ni jukumu la mamlaka kuhakikisha anaendelea kukitumia kifungo chake ima iwe kwa haki au kutokana na uonevu, kwa sababu kifo chake hakitawanufaisha chochote kwa kile wanachokitafuta kwa njia ya mateso.

Hii inamaanisha kuwa hata mtawala dhalimu vipi, lazima awe na wa kuwatawala, hivyo wanaotafuta haki ni lazima watambue kuwa kuna gharama inapaswa kulipwa ili kujinasua kutoka kwenye minyonyoro ya dhulma, na watambue pia kuwa ujabari wote wa dhalimu wao ni kwa sababu wao wamekubali kuendelea kuwa chini yake. Pindi watapoamua kukata minyonyoro hiyo, yeye atazidisha nguvu zake zote aendelee kuwakandamiza, na hivyo gharama kubwa itahitajika kujikomboa.

Msingi wa ukombozi ni kujitambua kwa wanaokandamizwa. Kujitambua kutawaunganisha walio kwenye idhlali kwa kuwa wamoja kwa msingi wa mateso ambao wote wameyapitia. Mshikamano wa namna hii ni hatari sana kwa dhalimu. Atatumia mbinu za kuwagawa, na anaweza kufanya hivyo kwa njia na gharama yoyote. Waandishi mashuhuri na weledi wa fasihi nchini mwetu kama Ustadh Shaban Robert katika kitabu chake cha ‘Kusadikika‘ na Profesa Said Ahmed Mohammed katika kitabu chake ‘Kivuli Kinaishi’ wamefafanua kwa upana namna dhana ya kujitambua na elimu zilivyo silaha madhubuti mkononi mwa anayeonewa. Kwa mfano, katika ‘Kivuli Kinaishi‘ tunapomuona muhusika Mtolewa akiitambua ‘nyeupe’ kuwa ni ‘nyeupe’ na ‘nyeusi’ kuwa ni ‘nyeusi’, kinyume na namna ‘unga wa ndere’ wa muhusika Bi Kirembwe unavyopaswa kumfanya aone. Hiyo ni ishara ya kujitambua na msingi wa kujinasua yeye na wenzake kutoka katika idhilali.

Hatima na mustakbali wa ukombozi wa mkandamizaji na mkandamizwaji utategemea uthabiti wa mshikamano wa waliodhulumiwa, maana hata dhalimu pia anahitaji kukombolewa kwa mujibu wa wanafalsafa wa ukombozi akina Frantz Fanon na Paulo Freire, ambao wanaona kwamba “dhuluma ni mfumo wa kimahusiano baina ya dhalimu na mdhulumiwa.” Katika mfumo huu, dhalimu yeye mwenyewe hayuko huru kama vile ambavyo alivyo mdhulumiwa. Kwa nini? Dhalimu humnyima uhuru na kuendelea kumtia khofu mdhulumiwa katika juhudi zake za kuendelea kumdhibiti. Hutumia kila silaha zilizo katika uwezo wake zikiwemo kuwabagua, kuwagawa, kuwapendelea baadhi yao dhidi ya wengine, kudanganya na kupotosha ili kumtia hofu na kumuaminisha anayekandamizwa kuwa hiyo ndio jaala yake na kwamba akijaribu kinyume cha hayo yatamfika mabaya zaidi. Hivyo hana budi kutii.

Ili mfumo huu uendelee, dhalimu kila siku anapaswa kutengeneza dhulma kubwa zaidi kwa sababu anayedhulumiwa huwa yupo katika jitihada endelevu za kujinasua. Hivyo basi dhalimu na yeye hujikuta yupo katika khofu akiogopa anayemdhulumu asipate uhuru. Hivyo, yeye mwenyewe yapaswa akombolewe awe huru kutokana na mfumo huo wa dhuluma. Kwa wale wanaoangalia katuni ya kitoto ya Kirikuu wataona ukombozi huu wa dhalimu ulipojitokeza kwa kukombolewa Mchawi Karaba kufuatia ushujaa wa mtoto Kirikuu.

Mwandishi wa habari na mshairi Mohammed Ghassani anaandika hivi kwenye shairi lake ‘Si Huru Siye na Wao’ (hatuko huru sisi tunaodhulumiwa wala wao wao wanaotudhulumu):

Kwa nini niulizayo, sambe sina jawabuye
Ningawa nauza leo
Yawapo kale kwa hayo
Ungajuwa hayo nawe, nayo mengi mengineyo
‘Kwa nini’ hii naiwe, kwetu na kwao zinduo
Tukikaa tutambuwe
Si huru siye na wao!

Katika muktadha wetu, Chama cha Wananchi (CUF) na Wazanzibari walioshinda uchaguzi halali kiujumla wamekuwa wakinyimwa haki ya kuunda serikali ya visiwa hivyo kwa njia za kidhalimu na kiuonevu na huku wakilitambua hilo. Vijana husema, mara hii wameutambua wa ‘jibwa’ kwa kudhihirisha matokeo halali kinagaubaga na kukataa kuiachia Tume ya Uchaguzi (ZEC) nafasi ya kuvuruga ushindi wao. Baada ya kuizuwia ZEC kumtangaza asiyeshinda kuwa mshindi kama ambavyo imefanya kwenye chaguzi zote za 1995, 2000, 2005 na 2010, mwenyekiti wa tume hiyo akaamua kuufuta kabisa uchaguzi mzima wa tarehe 25 Oktoba 2015 kinyume na sheria na kisha akavunja tena sheria kwa kutangaza uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi 2016.

Kwa mara nyengine tena, Wazanzibari wamejitambua kwamba uchaguzi huo wa marudio ni mtego wa panya na ndoana ya uonevu iliyotupwa na chambo kumtega na kumrudisha kifungoni Mzanzibari ambaye kwa sasa mguu mmoja umeshatoka nje kuelekea uhuru. Na sasa, kwa mara ya kwanza kabisa, Wazanzibari wanayo nafasi na uhalali katika historia wa kumuondosha mtawala aliyeendelea kuwabagua, kuwapandikiza chuki, kuwafitinisha na kuwaonea.

Mpigania haki za kiraia nchini Marekani, Malcolm X, aliwahi kusema: “Siamini kuwa pale watu wanapokuwa wanakandamizwa pasipo na haki kwamba wamuachie mtu mwengine baki aje awawekee kanuni ambazo kwazo wao wataibuka kutoka katika ukandamizaji huo.” Nami nimalizie uchambuzi huu kwa kusema maneno yanayofanana na ya Mzee Nelson Mandela kwamba “sikatai kuwa kwa kupendekeza haya niloyapendekeza nitakuwa nimepanga hujuma dhidi ya watawala. Sipendekezi haya kwa hamasa ya uzembe au kwa sababu ninapenda vurugu.” Nimependekeza haya kutokana na tathmini ya umakini ya hali ya kisiasa ya nchi yangu baada ya miaka mingi ya dhuluma, ubaguzi, unyonyaji na ukandamizaji wa Wazanzibari unaofanywa na utawala wa CCM visiwani Zanzibar kwa niaba na msaada mkubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzanzia, ambayo kiilivyo hasa ni serikali ya Tanganyika iliyojivisha joho tu la Muungano.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Khamis Issa, ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma nchini Norway.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.