Yapo maoni ya baadhi ya watu kwamba kitendo cha Maalim Seif Sharif Hamad, mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) kushiriki katika mazungumzo na mgombea mwenzake wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Mohamed Ali Shein, pamoja na viongozi wastaafu kuukwamuwa ‘mkwamo wa kisiasa’ uliojitokeza kufuatia ‘kufujwa‘ kwa uchaguzi wa Oktoba 2015 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kulikuwa ni kuwasaliti Wazanzibari.

Maoni hayo yamekuja baada ya kukwama mazungumzo hayo ambako nako kukafuatiwa na hatua nyengine ya Jecha kutangaza tarehe ya ‘kurudiwa uchaguzi‘ huo kwa staili ile ile. Zaidi ya hayo, zile kauli ambazo zilikuwa zikiendelea kutolewa na viongozi wa CCM, huku mazungumzo yakiendelea zilizoashiria wazi kabisa kutokuwepo kwa nia njema, zilishaonyesha muelekeo mbaya. Haya yamepelekea kuonekana kwamba kitendo cha Maalim Seif kushiriki na kuendelea mazungumzo hayo lilikuwa ni kosa kubwa na kimetumika kuhalalisha kuendelea kuwepo madarakani serikali ya CCM Zanzibar kinyume cha sheria.

Mjadala unaojitokeza katika maoni haya unahusu uhalali wa kisiasa (political legitimacy) ambao watu wanadhani umepatikana kutokana na kitendo hicho cha mazungumzo. Lakini hoja hiyo si sahihi kama baadhi ya watu wanavyodhania. Katika medani za kisiasa za kimataifa na katika sheria za kimataifa, suala hili linahusiana na sheria zinazohusu “utambuzi wa serikali” (recognition of government or states). Itabidi niilezee nadharia hii kwa ufupi kabisa ili uielewe

Dhana ya “utambuzi wa serikali”

Kuitambua serikali ni moja ya njia ya kuihalalisha uwepo wake na kuipa nafasi ya kufanya majukumu yake kwa ufanisi. Moja ya viashiria vya kuitambua serikali ni kuingia katika mazungumzo nayo, mfano kama mazungumzo ya kutafuta utatuzi wa mgogoro, au kushiriki katika shughuli za serikali kama vile wawakilishi wa chama kuingia katika chombo cha kuendesha serikali hiyo au baraza la kutunga sheria za serikali husika.

Hata hivyo, ni vyema tukatofautisha kati ya uhalali wa kisiasa (political legitimacy) kwa upande mmoja, ambao unaweza kuletwa na utambuzi (recognition), na uhalali wa kisheria (legality) kwa upande mwengine, ambao hauletwi na kitendo cha kuitambua serikali hiyo, bali msingi wake mkuu ni katiba ya nchi na sheria zake.

Kwa hali ya Zanzibar, huwezi kuzungumzia suala la mazungumzo yaliyofanyika kuwa yametoa msingi wa “utambuzi wa serikali” na kigezo cha uhalalishaji wa kisiasa wa serikali haramu iliyopo madarakani. Msingi wa hoja ni ule ule: kwamba uwepo wa serikali iliyopo madarakani ni kinyume na Katiba ya Zanzibar na sheria zake kutokana na muda wake wa kutawala kisheria kuisha. Ni bahati mbaya sana hakuna mbadala wa kutatua suala la kisheria isipokuwa sheria zenyewe na sio kama wanavyojidai kupendekeza watu wengine kuwa “busara na hekima” zitumike. Wanasheria mahiri wamechambua namna ambavyo Mwenyekiti wa ZEC na Tume yenyewe wasivyo na mamlaka ya kufuta uchaguzi ambao kisheria ulishakamilika. Hivyo basi, kufutwa kiharamu kwa uchaguzi wa Oktoba na vitoto vyake vyote vilivyotokana na ufutwaji huo ni haramu.

Kama ambavyo tangazo lililoufuja uchaguzi lilivyokuwa haramu, halikuhalalisha kisheria wala kisiasa kwa kulitoa katika Gazeti Rasmi la Serikali (kitendo ambacho nacho ni haramu), ndivyo hivyo hivyo yanayofuata yote hayapati uhalali wa kuhalalisha tukio moja baada ya jengine katika msururu wa matukio yanayovunja katiba na sheria za nchi, likiwemo la kuendelea kuwepo madarakani kwa serikali ya CCM na viongozi wake wote. Ndivyo hata pia lilivyo tangazo la Mwenyekiti wa ZEC la kurudiwa kwa uchaguzi.

Hii ni sawa sawa na kusema yote haya yaliyofuatia ni “kumpigia mbuzi gitaa” wakati yeye haelewi. Hakukuwa na uhalali wa kufuta uchaguzi, hakuwezi kuwa na uhalali wa yote yatokanayo na uvunjifu huo wa sheria na katiba. Hapa sina haja ya kupoteza muda kujadili tangazo lilikuwaje, lilitumia kipengele gani, na kadhalika, kwa sababu yote hayo ni BATILI na ni HARAM MUTLAQ.

Kwa hivyo, kwa Maalim Seif kwenda katika vikao hivyo hakukutoa uhali wa kisheria (legality) wala uhalali wa kisiasa (legitimacy) wa kuendelea kuwepo kwa serikali ya CCM. Lililopo hapa na ambalo halikuepukika lilikuwa suala la kuepusha umwagaji damu tukufu ya Wazanzibari. Na kwa hilo, Maalim Seif kamwe si msaliti bali ni shujaa, ndio maana hata Mzanzibari anayempinga kiongozi huyo, bado ndani ya nafsi yake anajuwa ametafautika na wanasiasa wengi wanaokurupuka kutumia nguvu ya umma bila kujaribu njia za kidiplomasia. Wazanzibari wenyewe wanaelewa fika dhamira mbaya ya CCM na serikali zake zote mbili ambayo wamekuwa wakiionyesha kwa kuendelea kuitawala kijeshi Zanzibar na kuwatesa raia zake, na bado hawajasahau mauaji ya raia wasio na hatia yaliyofanyika mwaka 2001.

Namna “utambuzi wa serikali” unavyotoa uhalali wa kisiasa

Ni vipi “utambuzi wa serikali” unapatikana na mahusiano yake na uhalalishaji kisiasa wa serikali iliopo madarakani? Labda nitoe mfano wa namna suala la utambuzi linavyofanya kazi au kutafsiriwa katika sheria za kimataifa katika muktadha uliowahi kutokea Zanzibar mara kadhaa na hususan nitajadili mgogoro wa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010.

Mara nyingi Zanzibar tumekuwa na chaguzi ambazo zinapoteza uhalali wa kisiasa (political legitimacy) kwa kutokuwa kwake za kidemokrasia, zikiandamwa na wizi wa kura au utangazaji wa matokeo yasiyo halali. Ilikuwa hivyo mwaka 1995, ikawa hivyo 2000, 2005, na hata huo wa 2010 uliomuweka madaraka Dk. Shein. Katika chaguzi zote hizo, kwa bahati mbaya licha ya kuvurundwa kwa matokeo na kutangazwa mshindi asiye halali, bado ZEC iliendelea kukamilisiha matokeo, kumtangaza waliyemtaka wao na kuapishwa. Haya yote yaliyofanywa baada ya CUF kushindwa kuzuia “bao la mkono” yanakuwa yapo katika misingi ya sheria za nchi na hivyo basi kuapishwa kuwa rais wa nchi na kuunda serikali kunakuwa kumekamilisha mchakato wa uchaguzi kisheria. Yanayobaki hapo ni malalamiko, ambayo yanaweza kuwa au yasiwe na msingi thabiti na uhalali.

Ndio maana hata kama ripoti nyingi za waangalizi wa ndani na nje ya nchi ziliarifu kuwepo kwa mapungufu ya msingi na ukiukwaji wa demokrasia, jambo hilo liliwapa CUF nguvu tu ya kususia na kutoitambua serikali iliyopo madarakani na si zaidi ya hapo. Kwa vile utaratibu wa kisheria ulitimia, malalamiko yanayobaki ni ya kisiasa na yanahusiana na uhalali wa kisiasa tu (political legitimacy) sio kisheria (legality).

Lakini ni vyema kuzingatia kwamba uhalali wa kisiasa sio jambo dogo, unaweza ukapelekea kuikosesha serikali uhalali wa kuongoza katika sehemu kubwa ya jamii hususan katika mazingira kama ya Zanzibar, ambapo vyama vina nguvu karibu sawa, ina maana nusu ya jamii hiyo inakataa kutawaliwa na serikali iliyopo kwa sababu hawaitambui. Na suala hili la kutokutambulika huwa ni sehemu ya mgogoro mkubwa ambao serikali za awamu kadhaa Zanzibar zimekumbana nao kwani wawakilishi wa upinzani walikataa kuhudhuria Baraza la Wawakilishi na hivyo basi Serikali kutokuwa na uhalali wa kisheria kupitisha baadhi ya maamuzi yake kutokana na idadi ndogo ya mahudhurio katika baraza hilo la kutungia sheria.

Historia ya karibuni ya Zanzibar inaonesha kuwa hata baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 na kuelekea uchaguzi wa 2010, CUF bado ilikuwa imesusia na haiitambui serikali ya Amani Abeid Karume. Katika chaguzi za 1995 na 2000, chama hicho kiliwahi pia kutokushiriki katika Baraza la Wawakilishi na kukata mahusiano ambayo yangepaswa kuwepo kati yao na serikali zilizokuwepo madarakani. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, wawakilishi wa CUF waliendelea kuingia katika Baraza la Wawakilishi huku chama chao kikiendelea na msimamo wake wa kutoitambua serikali. Itakumbukwa kwamba hatua hizi zilipelekea serikali kutafuta suluhu kupitia makubaliano maarufu yanayojuilikana kama Muafaka I na Muafaka II katika vipindi tofauti. Na katika kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010, utatuzi wa mgogoro ulipelekea kupatikana kwa makubaliano yaliyojulikana kama Maridhiano.

Sasa basi, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hata ile kukaa nao katika mazungumzo ni sababu tosha inayoashiria kuitambua serikali hata kama walisema hawatambui. Vile vile, kuingia kwa wawakilishi Barazani na kushughulika na shughuli za serikali, nako kulimaanisha kuitambua serikali tokea hapo walipoanza kufanya hivyo, kwa sababu utambuzi wa serikali katika sheria za kimataifa uko wa namna mbili: kwanza, ni utambuzi usio rasmi au tuuite utambuzi wa kivitendo/kiuhalisia (de facto recognition), ambapo japo unasema huitambui serikali, lakini vitendo vyako vinaashiria kuitambua; na, pili, ni kwa kutangaza rasmi hadharani kwamba unaitambua serikali na huu ni utambuzi rasmi (de joure recognition).

Kama kuna mgogoro mahala mara nyingi huanza kupatikana “de facto recognition” yaani utambuzi usio rasmi au wa kivitendo kwa kile kitendo tu cha kukubali kuyazungumza yaishe au kushiriki katika shughuli za serikali. Itakumbukwa kwamba katika kutafuta suluhu ya mgogoro uliotokana na uchaguzi wa 2005, kuliundwa Kamati ya Maridhiano ambayo ilizaa Maridhiano yenyewe. Hivyo kulikuwepo na kitendo cha kuzungumza baina ya CUF na serikali, ambacho kilitoa utambuzi kwa serikali “de facto”. Nilibahatika kuwepo katika moja ya mikusanyiko ya viongozi wakuu wa CUF, akiwemo Maalim Seif Sharif, na niliibua hili swali hata kabla hayajatokea yaliyotokea. Niliuliza kwa nini CUF iliendelea kuwaachia wananchi waamini kuwa CUF haijaitambua serikali wakati imeshaitambua tokea zamani? Suala hili lilikuja kuwa bomu zito hapo baadae baada ya Rais Karume kutaka CUF itoe tamko la kuitambua serikali ndipo mazungumzo ya maridhiano yaendelee. Wananchi walipojulishwa hilo na kwamba Maalim Seif yuko tayari kufanya hivyo, jazba zikawapanda. Na sina haja ya kueleza hadithi nzima, nyote mnakumbuka.

Lakini licha ya yote yaliyotokea, kwanza kitendo kile kiligeuka kuwa ni turufu ya CUF kuelekea maridhiano. Na kwa umahiri wake na kupendwa na wananchi ,Maalim Seif akaitambua rasmi serikali kupitia matamko rasmi ya chama na hata katika mikutano yake ya kichama. Na bahati wananchi wakamuelewa kupitia dhana nzima ya Maridhiano na hatima ya nchi yao. Hatimaye Maalim Seif aliyasema haya haya ninayoyazungumza kuhusu utambuzi wa serikali katika mahojiano yake na waandishi wa habari ambao walitaka kujua “kwa nini sasa na sio tokea zamani kuitambua serkali? Na mwisho wa yale, kutokana na nia thabiti za waliokuwa katika Kamati ya Maridhiano, ndipo ikapatikana Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Hakuna uhalali wa kisiasa bila ya uhalali wa kisheria

Nimetoa mifano hii ili uone namna ambavyo suala la uhalali wa kisiasa linavyohitajika katika kuipa uhalali serikali iliyopo madarakani baada ya sharti kubwa zaidi kutimia, yaani sharti la kuwepo uhalali wa kisheria. Hivyo basi ni dhahiri kwamba huhitaji uhalali wa kisiasa ili kutoa uhalali wa kisheria na kamwe hiyo sio sahihi. Madhali sheria imevunjwa na kugaragazwa, basi hata uitambue, serikali hiyo haitambuliki na kutambua kwenyewe kutakuwa haramu (unlawful recognition) kama ilivyo serikali yenyewe. Ni lazima kwanza murudi pale pale mulipojikwaa. Kinyume chake hayo ndio sahihi, yaani unahitaji uhalali wa kisheria kwanza ili upate uhalali wa kisiasa.

Hivyo basi, kitendo cha mazungumzo ya Maalim Seif na wahafidhina wa CCM Zanzibar – akina Dk. Shein na Balozi Seif Ali Iddi pamoja na viongozi wastaafu – hakitoi uhalali kwa serikali haramu kwa namna yoyote ile kama vile ambavyo navyo juhudi za Maalim Seif kuutatua mgogoro huo kwa kukutana na hao zisivyoweza kuzingatiwa kama usaliti asilani abadani. Kwanza, Maalim Seif aliweka wazi kwamba si yeye wala si Dk. Shein ambao wana uhalali wa kuwa katika madaraka kwa mujibu wa Katiba na akasisitiza kwamba suluhu yoyote ile katika mazungumzo hayo lazima izingatie na kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba 2015 na si vyenginevyo. Hivyo, kwa mujibu wake, alikuwa anakutana na mgombea mwenzake kupitia CCM, na sio rais wa Zanzibar. Pili, tuseme Dk. Shein ni rais kama anavyopenda kuitwa, basi bado kitendo cha Maalim Seif kuingia kwenye mazungumzo naye kilipaswa kuzingatiwa kama njia ya ufumbuzi wa mgogoro na sio cha utambuzi wa serikali wala uhalalishaji wa serikali iliyopo madarakani, kwa sababu ili iwe hivyo lazima kuwepo na uhalali wa kisheria kwanza.

Kwa maana hiyo, katika muktadha huo, kwetu sisi Wazanzibari, Maalim Seif amekuwa akitetea damu zetu ambazo Wahafidhina walishaandaa mipango ya kuzimwaga kabla muda haujafika. Nikisema kabla mda haujafika namaanisha kwamba kama kudai haki ya kuheshimiwa demokrasia Zanzibar ni lazima Wazanzibari wamwage damu yao, basi muda ukifika tuko tayari ila kwa sasa bado wananchi wa Zanzibar wana imani kubwa juu ya busara za kiongozi wao na juhudi anazozichukua kidiplomasia licha ya muendelezo wa vitendo haramu vya CCM Zanzibar.

Kinachoonekana hadi sasa ni kama kwamba CCM na vyombo vyake vya ulinzi na viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanataka Wazanzibari wauwawe kwa kudai haki yao, kama kwamba Umoja wa Mataifa ya Afrika (AU) unaendelea kubaki kimya bila kuuchukulia hatua ubakwaji wa demokrasia Zanzibar, na vile vile kama kwamba dunia kupitia Umoja wa Mataifa (UN) unayashuhudia yanayotendeka Zanzibar kama filamu tu sebuleni mwao. Wote hao wanawatumia Wazanzibari ujumbe mbaya.

Naomba nitumie msamiati wa Mwanasheria Othman Masoud Othman wa kuuita mzozo uliopo Zanzibar kuwa ni “busha” badala ya jipu, na nionye kama ambavyo muonyaji mwenye kuipendelea mema nchi yake angelionya, kwamba kama watumbuaji wa majipu wameshinda kulipasua busha lililopo Zanzibar, basi wanawalazimisha Wazanzibari wajisaidie wenyewe.

Lakini tunamuomba Muumba atulinde na vitimbi vya uongozi wa namna hii, na haki ya Wazanzibari ipatikane kwa salama na amani.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Khamis Issa, ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika masuala ya Utawala wa Umma nchini Norway

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.