Tarehe 22 Januari 2016 ni siku nyengine kwenye historia ya Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha, kujitokeza katika televisheni ya serikali akisema uchaguzi wa marudio utafanyika tarehe 20 Machi mwaka huu na wala hakutakuwa na kampeni wala wagombea wapya wagombea, bali wale wale waliowania katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba alioufuta kinyume na sheria siku tatu baada ya kufanyika kwake.

Inafahamika wazi kuwa Jecha alichukuwa hatua hiyo baada ya kuonekana dhahiri kwamba Chama cha Wananchi (CUF) kimeshinda kwenye nafasi ya urais ambayo iligombewa na Maalim Seif Sharif Hamad na pia kuongeza idadi kubwa ya viti vya uwakilishi na udiwani.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Ushahidi uliokusanywa vituoni na kusainiwa na mawakala wa wagombe wa vyama vyote unathibitisha hayo kuwa CUF ilishinda urais kwa asilimia 52 ya kura zote halali ikiwa na zaidi ya kura 25 za ziada na kikatwaa viti 27 ya uwakilishi, sambamba na viti vyote vya udiwani kisiwani Pemba. Hiyo ni hata baada ya wapigakura 30,000 kutopiga kura zao kisiwani Pemba pekee. Hadi Jecha anatangaza kuufuta uchaguzi, tayari wawakilishi 30 walishakabidhiwa vyeti vyao vya ushindi kutoka ZEC pamoja na madiwani wote wa Pemba na Unguja.

Kwa hivyo, Jecha aliufuta uchaguzi si kwa sababu ya kuwa uchaguzi huo ulikuwa na mapungufu kama alivyodai, lakini ni kwa kuwa chama cha kada huyo wa CCM aliyewahi kugombea nafasi ya uwakilishi jimbo la Amani na kuanguka kura za maoni mwaka 2005 kilikuwa kimepoteza. Na hii ni hoja kubwa inayomfanya Mzanzibari yeyote aliyepiga kura tarehe 25 Oktoba na yule ambaye alikosa lakini ana haki hiyo, arudi tena kituoni kwenda kurejea kile kile alichokifanya tarehe 25 Oktoba.

Ingawa hadi sasa chama cha CUF hakijatoa msimamo wa kushiriki uchaguzi huo wa marudio na wengi tukiamini kuwa wameususia, ukweli ni kuwa CCM inahofu sana ‘kugaragzwa’ zaidi endapo CUF watazinduka na kuamua kurudi kwenye ulingo na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo. Hii ni kwa kuwa hamasa na dhamira ya wana-CUF inafahamika vyema. Endapo wakiamua kushiriki jambo, basi huwa ni kwa imani yao na si ushawishi wa kitu fulani kama ilivyo kwa vyama vyengine.

Sasa endapo CUF ikiingia katika uchaguzi – na kwa upande wangu napendelea waingie uchaguzi ili uwepo ushindani wa kweli – basi kuna hatari ya CCM kupoteza baadhi ya majimbo ambayo walishinda kwa uchache wa kura katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba. Vile vile, kuna hatari ya ‘kugaragazwa’ kwa zaidi ya kura 50,000 kwenye nafasi ya urais.

Hivyo, kwa mwenye kujuwa, anafahamu kuwa kada wa CCM Jecha Salim Jecha amekipalilia chama chake mkaa. Hakina manusura, labda CUF tu iamuwe kufunga mikono nyuma.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.