Jumuiya yetu imeanza kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote walio husika na kadhia hiyo kwa vile tayari tumeanza kuwafahamu waliofanya vitendo hivyo kupitia mamlaka za mawasiliano na vyombo vya dola, wanachama wetu wote ambao wamechanganya damu wasijisikie wanyonge na hali ya kubaguliwa au kukwazwa na kitendo kilichofanywa na genge hilo la wahuni wa upizani wenye lengo la kutaka kutufarakanisha na kutugawa baada ya kuishiwa na hoja za msingi katika kipindi hiki.

TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI (UVCCM) KWA VYOMBO VYA HABARI                                            ALHAMIS 13 JANUARI 2016

Nina furaha kuwaita ndugu zangu waandishi wa habari katika mkutano wetu huu muhimu wenye mambo machache ila ni muhimu na yenye msingi kwa nchi yetu yanayohusiana pia na jumuiya yetu ya Umoja wa Vijana wa CCM.

Kwanza tunampongeza kwa dhati kabisa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kujitokeza rasmi mbele ya wananchi na kueleza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika ili kumpata Rais mpya kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu.

Pia tunampongeza kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa wakati akihutubia hafla ya kuwapokea vijana 700 wa UVCCM waliotembea kwa miguu kuunga mkono maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, mwaka 1964.
Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. Ali Mohamed Shein ilikuwa ni ya kimapinduzi, aliyoitoa kwa ujasiri mkubwa, tena kwa kujiamini huku ukihimiza na kuwataka wananchi waendeleee kudumisha amani, utulivu, umoja na upendo.

Tunaungana na Dkt. Shein kwa kuwashajihisha wananchi wa Zanzibar hasa wanachama wa CCM mahali popote walipo, kujiandaa kwa ajili kushiriki uchaguzi wa marudio hapo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itakapotangaza tarehe kwa mujibu wa sheria ikiwa ni sehemu ya kutekeleza matakwa ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

ZEC ni chombo huru kilichoundwa kisheria na inafanya kazi zake kwa mujibu wa taratibu bila kuingiliwa au kushinikizwa na mtu, taasisi au kiongozi yeyote, hivyo wananchi hatuna njia mbadala ya kutokisiliza.

Ndugu waandishi wa habari
Ikumbukwe kuwa Chama Cha Mapinduzi kinachotokana na kuungana kwa vyama viwili vya TANU na ASP, havikuwa vyama vyenye sera ya ubaguzi wa rangi, ukabila au kutazama imani ya dini ya mtu.
Vilikuwa ni vyama vyenye wanachama wa makabila yote, rangi, imani za dini, wasio na dini na vilipiga vita ubaguzi kwa kuhimiza umoja, amani na mshikamano wa kitaifa letu.
Aidha, misimamo na sera hizo zikarithiwa na bado zinaendelezwa na Chama Cha Mapinduzi na kwa wakati wote zimekuwa zikifuatwa, kusimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.
Dunia yote ni mashahidi kwamba Tanzania chini ya utawala wa serikali za CCM imekuwa mstari wa mbele kukemea kwa vitendo na kulaani mahali popote penye ukandamizaji wa haki, ubaguzi wa rangi au maonevu yanayotokana na kukosekana msingi ya usawa, haki na kwenda kinyume na utawala bora.
Mathalan kwa upande wa Zanzibar ASP iliungwa mkono na watu wa makabila, rangi na dini zote na hata mara moja hakuna ushahidi kama mtu alibaguliwa, au kuvunjiwa haki zake za msingi na za kisheria kwa sababu ya asili yake, nasaba au rangi aliyonayo na kabila lake.
Hali hiyo ndiyo iliyokifanya chama chetu na jumuiya zake kuwa na wanachama mchanganyiko, huku wakishika na kupewa dhamana kwa nyadhifa za juu, kama urais, ubunge, uwakilishi na nafasi kadhaa muhimu za kisiasa na kiutendaji Serikalini.
Ikumbukwe kuwa kabla ya Mapinduzi lilikuwa ni jambo la nadra kwani hakukuwa na utamaduni wa mwafrika kumuoa mwarabu au muhindi, mwarabu nae kupiga hodi katika nyumba ya mwafrika ili kupeleka posa kwa Mwafrika.
Ni matokeo na msimamo wa sera ya serikali ya ASP chini ya Rais wake hayati Mzee Abeid Amani Karume, ikasema wakati umefika kwa wananchi wa Zanzibar kuchanganya damu na kuzika tabaka la ubaguzi.
Uamuzi huo kwa sehemu kubwa ndiyo uliofungua milango ya haki, usawa, umoja na ushirikiano wa watu bila kubaguana kwa mtazamo ya rangi, imani ya dini au ukabila.

UVCCM tumesikitishwa na tunalaani vikali kitendo kilichofanywa na vyama vya siasa vya kuunganisha picha za wana-CCM watiifu na kuwanasibisha na maneno ambayo hayana uhusiano nao tofauti na maudhui ya ujumbe uliokusudiwa, kitendo hicho kilikuwa na nia ya kutaka kuwagawa na kuwafarakanisha wana-CCM kwa kisingizio cha ukabila. Kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa vikali na ni jambo lisilovumilika wala kukubalika hata kidogo, miongoni mwetu.
Nichukue nafasi hii kwa unyenyekevu na heshima kubwa kuwaomba wana-CCM wote walionasibishwa na ujumbe wa picha hizo kuwa wastahamilivu na wavumilivu.
Jumuiya yetu imeanza kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote walio husika na kadhia hiyo kwa vile tayari tumeanza kuwafahamu waliofanya vitendo hivyo kupitia mamlaka za mawasiliano na vyombo vya dola, wanachama wetu wote ambao wamechanganya damu wasijisikie wanyonge na hali ya kubaguliwa au kukwazwa na kitendo kilichofanywa na genge hilo la wahuni wa upizani wenye lengo la kutaka kutufarakanisha na kutugawa baada ya kuishiwa na hoja za msingi katika kipindi hiki.
Tunajua kuwa wapinzani wetu na wasiotutakia mema wamelivalia njuga swala hilo kwenye mitandao ya kijamii wakifikiri huo ndio mtaji wao wa kutugawa kisiasa, kutuhasimisha ili tukose kufahamiana, kupendana na kuendeleza mshikamano na umoja wetu.
Jambo hilo kamwe halitatokea na wala hawataweza. UVCCM haitagawanyika na wala chama chetu hakitadhoofika kwa sababu hiyo. Wana-CCM siku zote tunaongozwa na busara na hekima za viongozi wetu na hapa naomba ninukuu.

“Mwanachama wa CCM yeyote aliye imara hayumbishwi wala hatetereshwi na vijineno vya kuvunja moyo viwe vya kweli au kutengenezwa bali huzidisha uaminifu na uimara wake katika chama, si vyema wana CCM kucheza ngoma msiyoijua aliekuwemo yumo na asiyekuwemo haingii CCM wote ni ndugu hatutabaguana kwa rangi dini wala kabila ni watoto wa ASP na sasa ni Chama Cha Mapinduzi na akitoka mtu kutaka kujaribu kutugawa hatoweza’’ DK: Salmin Amour Juma Rais Mstaafu wa Zanzibar.
Hata pale aliyekuwa mgombea Mwenza wa urais kupitia chama cha CUF Juma Duni Haji mwaka 1995 kwenye viwanja vya Kibandamaiti aliposema kwamba mwaka huo chama chao kikishinda uchaguzi utakuwa ndiyo mwisho wa utawala wa mtu mweusi na hata pale vijana wa CUF walipowaita wamakunduchi 1 sawa na mbwa 10 wa Pemba chama chetu kilitumia hekma na busara kuhakikisha mbegu hizo za ubaguzi hazimei miongoni mwetu.
Niseme tena na tena kwa sauti ya juu kabisa huku nikiwataka wanachama wetu wote wenye mchanganyiko wa damu walipuuze jambo hilo ambalo tunaamini wanaosambaza na kutumia sura zao wametumwa na maadui wetu kwa lengo la kutugawa kwa maslahi ya anaowatumikia.
Zanzibar yetu ni moja, watu wake wote ni ndugu wa damu, hatubaguani na hatutabaguana kwa nasaba za Upemba au Uunguja, Uzanzibari na Utanganyika, kwa asili ya Uafrika au Uzungu , Ungazija au Uarabu. Chama chetu ni kimoja chenye mjumuiko wa makabila, rangi na imani tofauti sote tukiwa wenye wajibu na usawa katika kusimamia haki tukipinga vitendo vya kibaguzi na maonevu.
UVCCM tunasema kwamba hatutaweza kupata maendeleo ya nchi yetu na mafanikio ya aina yoyote ikiwa tutabaguana, kuoneana, kuvunjiana heshima au kudharauliana kwa sababu za kipuuzi na za kijinga ambazo hazifai mbele ya dunia iliostaarabika.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.
‘’Kidumu Chama Cha Mapinduzi’’
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.