Sisi Jumuiya ya Vijana CUF tunakubaliana na Uongozi wa CUF Taifa kuwa hakuna sababu yoyote ya kushiriki katika Uchaguzi wa Marejeo kwa sababu CUF ilishapewa ridhaa ya kuongoza nchi na wapiga kura halali wa Zanzibar. JUVICUF inawatahadharisha viongozi wa CCM kuwacha kung’ang’ania kuishinikiza tume ya uchaguzi kutorejea katika kumaliza kazi yake ya kutangaza matokeo halali ya uchaguzi, kutawaaminisha na kuwachochea vijana kutafuta njia mbadala ya kuweka madarakani aina ya uongozi wanaoutaka.

TAMKO LA JUVICUF KWA VYOMBO VYA HABARI  14/01/2016
Ndugu wanahabari;
Jumuiya ya Vijanawa CUF (JUVICUF ) imeguswa sana na hatua ya Katibu Mkuu wa CUF na aliyekuwa Mgombea Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, kwa hatua yake ya kuueleza umma wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla juu ya hali ya kisiasa ilivyo hapa Zanzibar, hatua za mazungumzo baina ya Viongozi wa Serikali ya Zanzibar na Viongozi wastaafu na athari ya ule unaoitwa “mkwamo wa kisiasa”.
JUVICUF inampongeza kwa dhati, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa taarifa yake ambayo sio tu ilikuwa ya kina lakini pia ilipitia hali nzima ya utata uliotengenezwa kwa makusudi kubadilisha na kubatilisha maamuzi ya wananchi wa Zanzibar waliyoyafanya kupitia sanduku la kura tarehe 25, Oktoba 2015 ili hatimaye kuipokonya CUF ushindi wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar bila ya uhalali wa kisheria na kikatiba.
Maalim Seif, ametoa muongozo na elimu kubwa. Amefanya uchambuzi wa kina na kuonyesha kila kasoro katika maamuzi ya Tume kiasi ambacho hakuna cha kuweza kukatalika.
Ndugu wanahabari;
Sisi tunaamini Maalim Seif amethibitisha bila ya chembe yoyote ya shaka kuwa hapakuwa na uhalali wowote wa kufuta chaguzi za Udiwani, Uwakilishi na Urais wa Zanzibar na kwamba uamuzi wa Tume ulikuwa ni sehemu ya njama zilizopangwa na kupikwa baada ya CCM kuona kuwa haina manusura kwa vile hesabu mezani zilikuwa wazi kuwa CUF ilikuwa imeshashinda kwa asilimia 52%,na kuipita CCM kwa zaidi ya kura 25,000.
JUVICUF inakubaliana na Maalim Seif kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Nd. Jecha Salum Jecha alishinikizwa ili abadili muelekeo wa matokeo ya uchaguzi ambao umemalizika kwa salama na amani na kuthibitishwa na taasisi zote zilizo angalia uchaguzi iwe zile za ndani na zile za nje. Kwa hivyo JUVICUF tunasema kuwa hakuna uongozi halali uliopo madarakani hivi sasa Zanzibar na tukubali kuwa kuna ombwe la uongozi ijapokuwa kuna watu wanajipa uhalali wa kukalia viti vya Uwaziri, Umakamu wa Pili na Urais wa Zanzibar.
Ndugu wanahabari
msimamo wetu JUVICUF ni kuwa uongozi wa Serikali ya Zanzibar uliopo madarakani hauna uhalali na kwa hivyo hauna nguvu za kikatiba na kisheria kufanya maamuzi wala kuendesha nchi na kila kitendo kinachofanywa nao ni haramu na mutlak, hivyo tunamtaka Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dr. Ali Mohamed Shein kuwacha kutia ulimi wake puani badala yake asimamie maneno yake aliosema “UTARATIBU WA KUKABIDHIANA NCHI NI KUFANYA UCHAGUZI NA ALIESHINDA KUKABIDHIWA NCHI” ni vyema akawa muungwana na mstaarabu kwa kutembea juu ya mstari wa maneno yake hayo.
JUVICUF inakubaliana na Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF kuwa Uchaguzi Mkuu haukufutwa kwa nguvu yoyote ya kikatiba na kisheria na kwa hivyo matokeo yake bado ni halali na yanapaswa kuendelea kutanganzwa na mshindi kupatikana.
Hivyo JUVICUF inaitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itimize wajibu wake kwa kurudi katika kazi ya majumuisho ya kura na hatimaye kumtangaza mshindi wa nafasi ya Urais Zanzibar ili kuepuka kuiingiza Zanzibar katika mgogoro wa kisiasa ambao unaweza kusababisha kuchafuka hali ya utulivu na amani.
Aidha, JUVICUF inalaani hatua zozote zinazolenga kuishinikiza Tume kufanya Uchaguzi wa Marejeo kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na utaratibu wa kikatiba na kisheria na ni wazi kwamba kitendo hicho ni kuyakanyaga maamuzi ya kidemokrasia yaliofanywa na wazanzibar tena kwa misingi ya uhuru na haki mnamo tarehe 25,October 2015.

Ndugu wanahabari
Sisi Jumuiya ya Vijana CUF tunakubaliana na Uongozi wa CUF Taifa kuwa hakuna sababu yoyote ya kushiriki katika Uchaguzi wa Marejeo kwa sababu CUF ilishapewa ridhaa ya kuongoza nchi na wapiga kura halali wa Zanzibar. JUVICUF inawatahadharisha viongozi wa CCM kuwacha kung’ang’ania kuishinikiza tume ya uchaguzi kutorejea katika kumaliza kazi yake ya kutangaza matokeo halali ya uchaguzi, kutawaaminisha na kuwachochea vijana kutafuta njia mbadala ya kuweka madarakani aina ya uongozi wanaoutaka.
Ni lazima CCM ikubali ukweli kuwa vyama vingi vya siasa vimeletwa ili kupata ushindani ambao utaleta mabadiliko ya utawala kwa ajili ya kuleta maendeleo na kwamba chama kisicho kuwa CCM kinaweza kushinda uchaguzi na kuongoza Dola ya Zanzibar.
Ndugu wanahabari
JUVICUF inasikitishwa na hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa kipindi cha miezi hii mitatu toka Serikali isiyo kuwa halali kushikilia uongozi na kusababisha mkanganyo mkubwa miongoni mwa wananchi .
Gharamaza maisha zimepanda, wananchi wamo katika mkorogo wa mawazo na usalama uko katika hali tete ambapo makundi ya Mazombi yaliopewa baraka na aliekuwa waziri wa vikosi vya SMZ, Nd. Haji Omar Kheir, bado yanaendelea kuwahilikisha wananchi katika maeneo mbalimbali huku Jeshi la Polisi likiwa kimya na kuvifumbia macho vitendo hivyo vya kiharamia.
Ndugu wanahabari
Kwa kuwa hakuna udhibiti wa Serikali, vitendo na lugha za kibaguzi zilizo kuwa zikijitokeza kwenye Bango la Kisonge na bango la maskani ya Kachorora huku Mamlaka zinazohusika zikishindwa kuchukua hatua stahiki sasa jambo hilo la hatari linajitokeza dhahir na kupewa baraka zote na Viongozi wa Kitaifa wa CCM kama ilivyotokea katika maandamano ya Umoja waVijana wa CCM (UVCCM) siku moja kabla ya kilele cha Sherehe za Mapinduzi.
Kutokana na athari zake kwa jamii pana ya wazanzibari, JUVICUF inalaani vikali lugha ya kibaguzi za kuwaita Wazanzibari waliochanganya damu kuwa ni MACHOTARA, na ni Vibaraka vya masultani. Lugha hii si tu inawavunjia heshima watu waliomo katika jamii yetu na walio na haki zote kama raia na wananchi wa Zanzibar, lakini pia inawachonganisha wazanzibari na ina nia ya kuvunja umoja wa wazanzibar na watanzania kwa ujumla kwa maslahi ya kikundi cha watu wachache walioweka mbele maslahi yao binafsi.
JUVICUF inaunasihi Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuacha mara moja kuhusika na kuwachonganisha wazanzibari na kuacha kuwakebehi na kutoa lugha kwani hatua hii haina manufaa yoyote kwa mustakbali wa zanzibar na watu wake. JUVICUF inawataka vijana wa Zanzibar kubaini kuwa UVCCM haina sifa na imepoteza uhalali wa kujinasibisha na wanamapinduzi wa Zanzibar kwa kwenda kinyume na malengo ya mapinduzi na hivyo inawaomba vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kukataa kutumika katika kuleta mifarakano inayoratibiwa na jumuiya hiyo.
Vilevile, JUVICUF inawataka Wazanzibari na wapenzi wa CUF waendelee kubaki katika hoja. Na hoja yetu ni kuwa CUF ilishinda uchaguzi ulio kuwa huru na wa haki, Kwa hiyo, hakuna hata sababu moja ya kuwepo Uchaguzi wa Marejeo kama inavyodaiwa kutaka kufanywa na Viongozi WAHAFIDHINA wasioipendelea mema Zanzibar na wananchi wake. Hivyo tunawataka Vijana wa Zanzibar na wa Tanzania kwa ujumla tuwe tayari kulikataa hilo kwa nguvu zetu zote .
JUVICUF inatoa wito kwa wananchi wote kuwa watulivu, huku wakisubiri maelekezo ya Viongozi wa juu wa Chama na wasikubali kuchokozeka kwa hali yoyote ile maana CCM na UVCCM watafanya majaribio kadhaa. JUVICUF inawahakikishia vijana wote nchini kuwa iko tayari kuulinda maamuzi ya wazanzibari dhidi ya njama ovu zilizopangwa na watu wasioheshimu demokrasia wala kujali sauti ya umma kupitia kisanduku cha kura.
JUVICUF inawasihi vijana wa Zanzibar na Wananchi wote kuwa makini zaidi katika kipindi hiki na kutokatishwa tamaa na matamko ya kiholela yanayotolewa na viongozi wa CCM waliojipachika madarakani kwani kila wanachokifanya ni hatua za mwisho za uhai wa Chama hicho kilichopoteza sifa na kupoteza uhalali wa kuongoza. Vijana wa Zanzibar na Tanzania wanapaswa kufahamu kuwa hatua hizi za sasa za CCM ni mateke ya mwisho ya farasi anaekata roho (Last kicks of dying horse).
JUVICUF inawatanabahisha vijana kuwa CCM haina manusura na kwamba kila kitu kitakuwa sawa na maamuzi ya wazanzibari yataheshimiwa kwa njia ya suluhu yenye manufaa kwa watu wote kwa kupitia nguzo ya Katiba yetu na sheria za nchi yetu

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA

HAKI SAWA KWA WOTE

MAHMOUD A. MAHINDA
KATIBU MTENDAJI – JUVICUF

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.