Ikiwa ni takribani miezi mitatu tokea Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar kutuhumiwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar kwa madai ya kuwepo kasoro nyingi kwenye uchaguzi huo, sasa kitendo hicho kimekuwa sehemu ya mfumo wa chaguzi kwenye taasisi nyengine visiwani kama ilivyoigizwa kwenye uchaguzi wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wa hivi karibuni, anaripoti Khelef Nassor.

Siku chache zilizopita wanafuzi wa SUZA walitekeleza haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kwa kufanya uchaguzi ambao ungewapatia kiongozi atakayewaongoza kwa mwaka wa 2016/2017. Lakini katika kile kilichoonekana kuwa ni uminywaji na uporwaji wa haki ya wapiga kura, uchaguzi huo uligubikwa na dosari na ukiukwaji wa demokrasia hali iliyopelekea aliyeshinda uchaguzi huo kutotangazwa huku tuhuma za CCM kuuharibu uchaguzi huo zikielezwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye chanzo cha kuaminika, uchaguzi huo uliowahusisha wagombea wawili wa kiti cha urais – Ahmed Mohammed Omar na Mohammed Hassan Fadhil – ulianza dosari tokea kwenye hatua za awali kutokana na kuingizwa watu wasiokuwa wanafunzi tena wa chuo hicho kwenye Tume ya Uchaguzi na kuruhusiwa kusimamia uchaguzi huo, hatua ambayo ilipingwa vikali lakini bila ya mafanikio na mgombea aliyedaiwa kuporwa ushindi wake, Ahmed Mohammed.

Jinsi kura ya wana-SUZA ilivyochakachuliwa

Ahmed anasema licha ya kumuandikia barua mkuu wa utawala wa wanafunzi (Dean of Students) na kumtaka amuondowe mmoja wa makamishna kwenye tume ya uchaguzi, kwa kuwa kwa mujibu wa sheria zao hakupaswa kuwemo kwenye tume hiyo baada ya kupoteza sifa za uwanafunzi, hatua yake hiyo haikuzaa matunda.

Ahmed Mohammed Omar, mgombea urais anayedai kuporwa ushindi.
Ahmed Mohammed Omar, mgombea urais anayedai kuporwa ushindi.

“Kiukweli nilikuwa sina imani naye kamishna huyo, kwa sababu alikuwa ni mtu ambaye tayari ameshamaliza chuo, na nilijua tu kuwepo kwake pale ni kichocheo cha kuja kuuharibu uchaguzi, na hivyo nilimuandikia barua Dean of Students asitishe uwepo wake kwa sababu hata wanafunzi walikuwa wanalaumu kwa nini ashirikishwe mtu ambaye ameshamaliza chuo, lakini barua yangu haikujibiwa” Ahmed aliuambia mtandao huu wa Zanzibar Daima.

Matokeo yake, anasema, hata idadi ya kura zilizopigwa na zile zilizotangazwa ni tofauti, hali ambayo anayoiita “wizi wa wazi wazi”.

“Hebu angalia, kura zote zilizopigwa ni 1,831, kura halali ni 1,771 na kura zilizoharibika ni 37. Mimi niliambiwa nimepata kura 834 na mpinzani wangu akapata 952. Sasa ukizijumlisha kura zangu na za mpinzani wangu na zile 37 zilizoharibika, utagundua kuwa kura zote zilizopigwa ni 1,823 ambapo na sio 1,831 hivyo kura 8 zimezidi hapa. Huu ni uchakachuaji wa hali ya juu.” Alisema huku akionesha karatasi za matokeo ambazo zinaonekana kuandikwa kwa kufutwafutwa.

Licha ya kuwepo kwa dosari hiyo, amesema uchakachuaji mwengine ulijitokeza kwenye zoezi la uhesabuji wa kura. Katika zoezi hili fomu za mawakala wote wawili zilionesha kwamba yeye alipata ushindi, lakini kitu cha kilichomstaabisha ni kwamba siku ya pili yake fomu za tume zilibadilishwa matokeo yake na hivyo kumpatia ushindi Mohammed Hassan kinyume na sheria.

Zanzibar Daima ilipomtafuta Mohammed Hassan Fadhil ndiye mgombea anayelalamikiwa kupewa ushindi usio wa halali, hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo akisema angelifanya hivyo pale tu ambapo angelipewa ridhaa na uongozi wa chuo.

“Unajua ndugu mwandishi, SUZA ni taasisi kubwa. Kwa hivyo siwezi kuzungumzia jambo lolote linaloihusu taasisi bila ya ridhaa kutoka kwa uongozi husika,” alibainisha.

Kwa mujibu wa mmoja wa makamishna wa tume iliyoendesha uchaguzi huo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, “kura zilizohisabiwa na kutiwa saini na wagombea wote wawili mbele ya mwanansheria, zimeonesha kwamba mgombea Ahmed ameshinda uchaguzi dhidi ya Mohammed”, lakini walipotaka kuyatangaza matokeo, uongozi wa chuo uliwataka kuahirisha zoezi hilo hadi utakapojiridhisha.

“Baada ya kufanya majumuisho, tuliona kwamba mgombea Ahmed Mohammed Omar, ameshinda uchaguzi. Kwa hivyo baada ya kukubali, ni kwamba wagombea wote walitia saini kukubali kushinda na kushindwa kwa ridhaa yao. Baada ya hapo tuliamua kwenda kwenye kikao na mbele ya kikao, akiwepo makamo na mwanasheria wa chuo, na baadhi ya makamishna wezangu, alikiri kwamba ameshindwa na akaulizwa tena si chini ya mara tatu,” alieleza kamishna huyo.

Aidha, alielezea kilichotokea baada ya hapo kuwa ni cha kustaajabisha kabisa, kwani tume yao iliekewa kikao na uongozi wa chuo na kutakiwa kutangaza matokeo kwa kutumia fomu ambazo alisema hazikuwa halali kutokana na uchakachuliwaji uliofanywa na baadhi ya wajumbe wa tume hiyo ili kumpa ushindi wa kibabe Mohammed, mpinzani wa aliyeporwa ushindi.

“Mimi nilishangaa sana. Wakati tunataka kumtangaza mshindi, uongozi ulitoa amri kwetu na kututaka tutumie fomu ambazo si halali ili kumpa ushindi asiyeshinda, na kwa bahati mbaya sana mwenyekiti wetu bila ya hata kuhoji alikubali kufanya hivyo.”

Jeshi la Polisi lamwagwa chuoni

Pamoja na hayo, alisema katika kile kilichoonekana kuwa ni kulazimisha kumtangaza asiyekuwa mshindi, jeshi la polisi lilimiminika katika kituo cha kutangaza matokeo kilichopo Beit-el-Raas kando kidogo ya mji wa Unguja, ili kuhakikisha hakuna yoyote ambaye ataleta vurugu kwa kupinga uamuzi huo.

Abdalla Daudi Ubwa, Katibu Mkuu wa Kamati ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar.
Abdalla Daudi Ubwa, Katibu Mkuu wa Kamati ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar.

“Kwa kweli hatukuwa huru hata kidogo, na tume yetu haikuwa na tofauti yoyote na ile ya Jecha (ZEC) kwani uongozi wa chuo ulituingilia katika kazi yetu kwa kutulazimisha tumtangaze Mohammed ambaye kimsingi hakushinda uchaguzi. Pia tuliona maajabu makubwa kuona jeshi la polisi likizingira kwenye eneo ambalo matokeo yalikuwa yanatangazwa” aliongeza.

Jitihada za Zanzibar Daima kumtafuta aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi huo ziligonga mwamba, kwani licha ya awali kuahidi kukubali kufanya nasi mahojiano wakati wa jioni, alipotafutwa wakati husika, simu yake ilikuwa imezimwa.

Lakini kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Kamati ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar, Abdalla Dadi Ubwa, alisema hali hiyo imewasikitisha sana, kwani inaweza ikaleta athari kubwa kwa wanafunzi pamoja na kujenga taswira mbaya kwamba hata taasisi hizo za juu kitaaluma zinaendeshwa kisiasa.

Shutuma dhidi ya CCM

Abdalla alisema hawashangai sana jambo hilo kutokea kwani hata huko nyuma chuo hicho kilishakumbwa na matokeo kama hayo ya kupindisha maamuzi ya wananchi huku akiituhumu CCM kuendesha mchezo huo kupitia mawakala wake walio vyuoni.

“Mimi kama Katibu na wezangu wote hatushangai kwa sababu huu ni mchezo ambao tumeuzoea na umeshawahi kutokezea siku nyingi huko nyuma, na tunajua kuwa hizi ni njama za CCM kuwa wao wanataka kuona kwamba siku moja vyuo hivi wanavihodhi na wanaviendesha vile wanavyotaka wao,” alieleza Abdalla.

Licha ya mpango huo kuandaliwa lakini Ubwa amesema kamwe hawatofanikiwa kwa jamii ya wasomi ni tofauti na jamii nyengine kwani wao ni vigumu kupelelekeshwa.

“Jambo hilo ni gumu sana kwani wasomi ni tofauti na watu wengine. Wasomi wanatakiwa wawe waelewa mambo mengi na wanelewa ni nini wanachotakiwa kufanya na pale ambapo wanaona hapa wanataka kuburuzwa, wanasema hapa tunaburuzwa na hatuhitaji kwenda huko,” alisisitiza.

Hata hivyo ameuomba uongozi wa SUZA kukaa na kutafakari upya ili wamrejeshee ushindi wake Yule ambaye alishinda uchaguzi huo kwani kutofanya hivyo ni kutia sura mbaya chuo hicho na Zanzibar kwa ujumla.

“Tunaiomba bodi ya SUZA na uongozi wake wote, warejeshe haki ile kwa aliyeshinda kwa maslahi ya taifa letu na kwa maslahi ya wanafunzi wetu wa vyuo, lakini pia kwa maslahi ya kutokugeuka na kuikengeuka haki” Alishauri.

Pia alielezea msimamo wao kama jumuiya wataungana na aliyeporwa ushindi wake ili kushirikiana katika hatua zozote za kisheria amabazo atahisi kwamba ni muhimu kuzichukua na zitaweza kumpatia haki yake hiyo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.