Taarifa iliyotolewa siku ya tarehe 12 Januari 2016 na Daniel Chongolo, aliyejitambulisha kuwa mkuu wa mawasiliano na umma wa Chama cha Mapinduzi (CCM) inasema chama hicho “kimesikitishwa sana na ujumbe wenye maudhui ya ubaguzi ulioandikwa kwenye moja ya mabango yaliyobebwa na mmoja wa wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 za Mapinduzi ya Zanzibar” na kwa hilo chama hicho tawala kinaomba radhi, kinapinga na kinakemea.

Taarifa hiyo kwa umma inafuatia shinikizo la wachangiaji wengi kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kusambaa kwa picha zinawaonesha vijana wa CCM visiwani Zanzibar wakipita na mabango yanayosomeka “Machotara wa Hizbu, Zanzibar ni nchi ya Waafrika” na au “Machotara Vibaraka wa Sultani watupishe na Mapinduzi yetu” mbele ya viongozi wa CCM na serikali ya Muungano, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Balozi Seif Ali Iddi na Makamu wa Rais wa Tanzania, Bi Samia Suluhu Hassan, tarehe 11 Januari 2016, ikiwa sehemu ya sherehe hizo. Lau ingelikuwa si hiyo nguvu ya mitandao ya kijamii, hakuna ajuwaye ikiwa CCM ingelijipa tabu ya kuandika waraka wake wa aya tatu na kuusambaza mitandaoni kwa haraka ile.

Mimi ni mmoja wa wanaodhani kuwa Chongolo alifanya haraka mno kutoa tamko lake na zaidi imekuwa bahati mbaya sana kwamba amelitoa. CCM haina la kujutia wala la kulikemea kwenye hili, kwa kuwa chuki za kibaguzi ndio uzi uliolifuma guo linaloitwa CCM Zanzibar. Kujaribu kuukata uzi huo ni kutaka kulirarua guo lenyewe, na sidhani ikiwa CCM Taifa inapendelea hivyo. Historia inaonesha kuwa Dodoma inaweza kupoteza kila kitu – ikiwemo heshima yake ya kitaifa na kimataifa – lakini sio kuiwajibisha CCM Zanzibar pale inapochupa mstari.

CCM Zanzibar na chuki za ubaguzi ni mfano wa samaki na maji. Kama ambavyo samaki hawezi kuishi nje ya maji, ndivyo nayo  isivyoweza kuishi nje ya mduara wa chuki za kibaguzi. Ndani ya mduara huo, ndimo ulimo “uhalali”, pumzi na maisha yake. Wimbo mmoja maarufu wa mwimbaji wa taarab wa Zanzibar, Fatma Issa, unauliza: “Hutaki Mwanakwerekwe, mwenzangu uzikwe wapi?” Suali hilo hilo pia linaweza kuulizwa kwenye muktadha huu: ikiwa CCM haitaki chuki za kibaguzi, iishi kwa njia  gani?

Huu ni ukweli ambao CCM Taifa unaujuwa vyema na inafaidika nao. Chuki za kibaguzi ni sehemu ya mfumo ulioiunda na unaoiendesha CCM yao upande wa Zanzibar nayo imekuwa ikiutumia ipasavyo. Mara kadhaa wenyeviti wa CCM Taifa katika awamu mbali mbali, wakiwa madarakani na wakiwa wastaafu,  wamekuwa wakiitumia kete hiyo hiyo kuendeleza maslahi yao.

Katika sherehe kama hizi za Mapinduzi za mwaka 2004, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa wakati huo, Benjamin Mkapa, alisimama pale uwanja wa Amani akinadi: “Tusemeni Mapinduzi Daima kwa sauti kubwa hadi vitukuu na virembwe vya masultani na mahizbu watusikie, kwa sababu bado wangalipo”. Kwenye jukwaa kuu, ilikuwepo familia ya Rais Mstaafu Amani Karume, ambayo yenyewe ni sehemu ya vitukuu hivyo. Disemba 2005, Rais Jakaya Kikwete alisema kwenye mahojiano yake na gazeti la Mwananchi kuwa kisiwa cha Unguja ni ngome ya chama chake isipokuwa tu kwenye Mji Mkongwe kwa kuwa hapo pana Wapemba wengi. Tarehe 23 Oktoba 2015, wakati akifunga kampeni za CCM kwenye uwanja wa Kibandamaiti, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, akitumia wimbo wa “Msegeju ana ng’ombe”, alisema utawala wa Zanzibar ni miliki ya Afro-Shirazi wa Unguja na sio Wapemba kwani wao hawakuguswa na Mapinduzi, bali wamealikwa tu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa hivyo, mfumo wa chuki za kibaguzi dhidi ya kundi fulani la Wazanzibari ni wa kitaasisi ndani ya CCM. Si jambo la jana kwenye sherehe za mwaka huu za Mapinduzi tu. Lina mizizi mirefu na inayofahamika ndani ya tabaka tawala. Kwa mfano, wakati wa harakati za madai ya Katiba Mpya, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alipanda jukwaani na kuwataka wafuasi wake kuimba na kutosahau wimbo wa “Mwana wa Nyoka ni Nyoka”, akijibu hatua ya Chama cha Wananchi (CUF) kutumia wimbo wa wanamapinduzi “Sisi Sote Tumegomboka”.

Narejea. Chuki za kibaguzi ni za kitaasisi katika genge liitwalo CCM Zanzibar. Unaposikia kuwa chama hicho kinaimarisha maskani zake au kinaendesha “madarasa ya itikadi”, inachokifanya hasa ni kufundisha “namna bora zaidi” ya kuzitekeleza chuki hizo za kibaguzi kwa maslahi ya watawala. Ndio chimbuko la makundi ya kihalifu yaliyopewa majina ya Janjawidi, Mazombi na Masoksi. Vijana kwenye makundi hayo hufundishwa chuki za hali ya juu dhidi ya Wazanzibari wanaochukuliwa kuwa wapinzani. Hupewa hekaya za mabibi zao kufyagilishwa kwa matiti hadi barabara zikawa safi wakati wa utawala wa kisultani, au mamba zilizochanwa kwa visu ili mke wa sultani aone mtoto alivyokaa tumboni, au kupandishwa mnazi mkwezi wa Kiafrika kisha akapigwa risasi ili watoto wa Kisultani waone mtu akifa, au ya Jumba la Maajabu la Forodhani kujengwa kwa kufukiwa vichwa vya Waafrika weusi kwenye kila nguzo yake. Baada ya hapo, hufundishwa kutumia silaha za kienyeji na za moto kuwadhuru Wazanzibari mitaani, ambao huambiwa ni kizazi cha Masultani, Mahizbu, na kikoloni.

Matokeo yake huonekana kila kwenye uchaguzi unaofanyika visiwani humo. Miongoni mwa mikasa iliyoripotiwa na shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch kwenye mauaji ya 2001 kisiwani Pemba, ni ile ya familia nzima kubakwa mbele ya wazazi wao, huku wabakaji wakiwaambia wanafaidi “matoto ya Kisultani”.

Nilikuwa sehemu ya timu ya waandishi wa habari kuelekea uchaguzi wa 2005, na miongoni mwa matukio niliyoyashuhudia ni ushahidi wa mkaazi mmoja wa Kianga mwenye asili ya kisiwa cha Pemba ambaye mke wake alibakwa mbele ya macho yake, huku akiwa kafungwa kamba na akiambiwa kuwa hiyo ni salamu kuwa arudi kwao Pemba. Mara kadhaa ubao maarufu wa Kisonge umekuwa chombo cha habari cha CCM Zanzibar kikisambaza ujumbe unaotokana na siasa hii kongwe na imara ndani ya chama hicho – “siasa ya uchotara”.

Hata kilichotokea tarehe 28 Oktoba 2015 hakiendi mbali hata kidogo na ukweli huu. Jecha Salim Jecha wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) alitoa tamko lile akiwa mafichoni aliko kwa sababu tu ya kutekeleza “siasa za uchotara”, ambazo haziruhusu utawala wa Zanzibar kuwa mikononi mwa hao machotara.

Kwa uwazi kabisa, mfumo huu wa chuki za kibaguzi umejengewa hoja kuwa madaraka ya kuiongoza Zanzibar hayawezi kukabidhiwa kwa yeyote ambaye si mwana-CCM mwenye mizizi ya kibaguzi na chuki dhidi ya Wazanzibari wengine. Yaani haitoshi tu kuwa mwana-CCM, lakini pia awe mwenye chuki za kutosha ya kibaguzi na ukatili wa kutosha. Mwana-CCM anayeonekana kukengeuka hilo na kuzungumzia umoja wa Wazanzibari, mshikamano na mapenzi kwa dhati, hafai. Ndiyo yanayomkumba Amani Karume kwa kuwa amethibitisha kutoka nje ya mduara huo.

Ndio maana, wengine hatuoni mantiki ya CCM kujipa tabu ya kuomba radhi kwa kitu ambacho ni sehemu yake, kwa sababu haitaweza kukiwacha na ikikiwacha itakufa. Haitakuwa tena CCM hii ambayo ilijiamulia kurithi kila mabaya ya mtangulizi wake, ASP, na kuyaacha yote mema ya chama hicho kikongwe visiwani Zanzibar.

Na bado kuna sababu nyengine ya CCM kutopaswa kuomba radhi – Wazanzibari wanaobaguliwa kwa mabango kama haya ni watu madhubuti na imara zaidi kuliko chuki zenyewe dhidi yao. Maneno yaliyomo kwenye mabango kama hayo yamekuwa yakisemwa takribani kwa mwaka wa 50 huu, na bado wanaosemwa hawakuwahi kuvunjika moyo wala kurudi nyuma. Kinyume chake, wamekuwa wakiendeleza imani yao kuwa Zanzibar ni nchi yetu sote kwa pamoja na kwamba sisi ndio wenye haki ya kuamua khatima yake kwa njia za kistaarabu. Matokeo yake wamekuwa wakiwavutia wengine waliokuwa na mtazamo huo huo wa kibaguzi dhidi yao.

Leo hii, kwa aliye mkweli wa nafsi yake anaujuwa ukweli mmoja – CCM imegeuka kuwa chama cha wachache visiwani Zanzibar – uchache wa wafuasi na uchache fikra njema za kuiendesha nchi. Uwingi pekee ilionao CCM kwa Zanzibar sasa ni uungwaji mkono inaoupata kutoka vyombo vya dola ambavyo vinamilikiwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano.

7 thoughts on “CCM haina la kuomba radhi kwa “siasa za uchotara””

  1. Assalaamu alaykum alhabib, umeandika vya kuandika, wenye macho wataona, wenye masikio watasikio. Kwa sisi tunaoitwa machotaja tuliozaliwa unguja na kuishi kwa miaka yote haya tunayajua vyema na imekuwa kama silaha ya kutushambulia hata kabla ya hivyo vyama vyingi kuanzishwa. Wakati huo wa chama kimoja baba yangu alikuwa balozi wa nyumba 10 wa CCM lakini bado tulikuwa tunatukanwa kwa namna tofauti. Huu kweli ni mfumo ambao CCM wakiucha chama kitakufa. Maana kundi la watu wanaowaongoza sidhani kama wana akili za binadamu wa kawaida, kwa sababu binadamu wa kawaida hata kama hakusoma skuli bado ana akili ya kutafakari na kufanya maamuzi yake binafsi. Safari bado ni ndefu kupata uhuru tunaostahili.
    Abuuhmad

  2. Kwa hakika muandishi nakupigia saluti umeandika kwa fani ya kistaarabu ya kutosha. Kwa mwenye akili kwake huu ni ukweli kama mba ya mwezi. Dhulma haiza ila dhulma kwa sababu Mungu ni muadilifu ingelikuwa mapinduzi ni ya kubarikiwa basi tungekuwa mbali. Mapinduzi yameleta matunda zaidi ya kikoloni. Hakuna lilopatika la kheri ila chuki za kuendelezwa na kujineemesha kwa viongozi wachache wanosingizia uzalendo….Ikiwa uchotara ni ila mbona Obama katawala dola kubwa ulimwenguni.

  3. Makala yameandikwa kwa tafakari ya hali ya juu kabisa. Itawasaidia wale wote wanaotafuta chimbukizi cha haya mawazo ya kibaguzi. Mtiririko wa upotovu/ujinga huu unaendelea kutuvuruga. Makala haya yananikumbusha vile viroja na kauli za kibaguzi zilizotolewa hadharani wakati ule Bunge la Katiba lilipokuwa linajadili ripoti ya Warioba. Unachopanda ndio utakacho zaa.

  4. Nakupongeza Bwana Ghassan, maneno yako tunayaandika kwa “Wino wa Dhahabu” Mungu akubariki umetufungua macho. Kwa kweli hakuna serikali ulimwenguni inayofuga magengi kina Janjawidi na masoksi kulea chuki ili kuleta vitisho kwa kila anaewapinga. Huu ni ujangiri, uhuni na ugaidi wa kiserekali tarehe ya kisiasa duniani hajawahi kuandika. CCM ndio serkali ya kihuni ya kwanza duniani. Hata wakikataa kubakuwa madaraka kibabe ni ushahidi wa kutosha kuonesha uhuni. Wakati huu wa kileo kitu Mapinduzi yamepitwa na wakati. Democracy imetanda dunia, nchi za kikomonist zimebadilisha siasa. Hakuna tena kitu mapinduzi, umeshidwa kaa pembeni mpishe mwenzio. Serikali zote za kimapunduzi duniani zime prove failure. Kwa ajili ya maslahi yenu binafsi mnayalinda kwa mtutu wa bunduki na huku mkileta ukabila kuwatenganisha wazanzibari. Ndugu zangu wazanzibari wasitutishe hawa Wahafidhina mguu kaburini safari ya akhera inawakaribi baada ya kutubu kwa maovu na damu waloimwaga wa wamo wanatifitina za ubaguzi. Hawa ni watu madhalimu moto unawangoja.

  5. Napenda kujitokeza japokuwa mimi sio mzanzibari, haki haijifichi iko wazi. Kwa hakika maneno anosema Ghassany yamefika upeo wa haki hakuna kuyapinga au kutowa dosari. CCM bado wamo kwenye giza, dhamira zao mbovu za udanganyifu. Wanawapambia watu historia za uwongo na potofu wapate kubaki madarakani japokuwa hawatakiwi na uma. Kweli mkoloni hakupendeza lakini hakuwa muovu kama ilivyo CCM hivi sasa hasa ya Zanzibar, hakukuwa na vigengi vya kupiga watu Na vitisho. Nchi ilikuwa na maendeleo makubwa wakati wa kikoloni ndani ya miaka52 ya mapinduzi Zanzibar imerudi nyuma miaka miya mbili. Historia zilopita zishapita. Rais Kenyata alisema baada ya uhuru “We have to learn to forgive and forget” vijana wetu wanataka maendeleo ya kuwatowa kwenye umasikini, historia ya usultan haiwasaidii kitu. Viongozi walipitiwa na wakati kazi yao kuzalisha chuki katika jamii na kupigia debe historia potofu hawafai kuleta maendeleo ya nchi ila juu ya nafsi zao. Kwa ufupi viongozi wa CCM Zanzibar wamefilisika ustaarabu itafika wakati itabidi waondolewe kwa nguvu na kumwaga damu. Utawala wa mabavu haukubaliki duniani popote pale

  6. Allah swt anajua zaidi kuliko sisi nini kakusudia kwa yaliyo andikwa katika mabango kuhusu machotara

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.