Pale hadithi mbili zinapokutana njiani – moja ikiikimbia jana yake na nyengine ikiikimbilia kesho yake – panakuwa na fursa ya kujihakiki upya sio tu kama fanani na hadhira, bali pia kama wahusika wa hadithi zenyewe, kama watenda na watendwa wa mifumo yetu ya kisiasa na kijamii.

Ndicho kitu cha kwanza ambacho hadhira ya mchezo wa maonesho, Puma, anachoweza kujifunza. Puma, mchezo ulioandikwa, kutayarishwa na kuongozwa na Mkawasi Mcharo Hall, ni igizo linaloakisi majeraha ya Wakenya kutoka yale ya mapambano ya uhuru zaidi ya nusu karne iliyopita hadi vidonda vya mauaji ya baada ya uchaguzi wa 2006. Lakini je, sanaa inaweza kutumika kuyaponya majeraha haya na kuwapa Wakenya fursa ya kusonga mbele kama taifa moja?

Usimulizi wa hadithi

Usimuliaji hadithi una njia nyingi kwenye jamii za Waswahili, ikiwemo njia hii ya sanaa za maonyesho, ambayo huikusanya hadhira sio kwa namna ya paukwa-pakawa, mwanangu mwana siti, kijino kama chikichi, bali kwa kuwashuhudia mafanani na watambaji wakionyesha kwa vitendo mkasa ambao vyenginevyo ungesimuliwa kwa mdomo.

This slideshow requires JavaScript.

Kote kwenye historia yake, mwanaadamu ameitumia sanaa kujisemea na kuyasemea yanayomzunguka, ndio sababu ya sanaa kuitwa mdomo wa jamii, na ndio maana kuna ulazima wa sanaa kuakisi jamii husika. Ndipo mchezo huu wa Puma ulipo pia.

“Ikiwa naweza kuufupisha, mchezo huu ni kuhusu makutano ya hadithi mbili. Upande mmoja kuna msichana ambaye yupo kileleni mwa kutimiza ndoto yake kubwa maishani, na upande mwengine una mwanamme mtu mzima ambaye anakimbia mateso yake ya nyuma. Wanakutana, na kile kinachotokea kwenye makutano haya ndicho kinachokuwa hadithi ya mchezo wenyewe,” anasema Mkawasi.

Na kweli. Ndani ya Puma muna hadithi mbili zinazokutana – moja ni hadithi ya Mwalimu Kulungu, mtendwa wa mauaji ya 2006 – 2007 nchini Kenya, ambaye alimpoteza mke wake na mtoto wake mchanga, aliyezaliwa usiku ule ule yalipoanza machafuko baada ya uchaguzi mkuu.

Kwenye jukwaa la Jumba la Maonesho la Taifa jijini Nairobi mwanzoni mwa mwezi Disemba 2015, nilimshuhudia muhusika huyu akitamba kwa malalamiko na maumivu: “Siku ile jirani yangu alikuja na kuniambia kuwa kuna watu wanakuja kuichoma moto nyumba yangu. Tulikuwa tumejenga nyumba yetu hapo, lakini sasa tulionekana kama wageni, kama watu wa kabila lisilofaa. Nilikuwa mwalimu kwenye Mavani Forest, nikingojea shule zifunguliwe kwa mwaka mpya. Nilikuwa na nafasi kubwa ya kuwa msaidizi mwalimu mkuu. Siku hiyo mke wangu alikuwa nyumbani, tulikuwa tukitegemea kupata mtoto wa kwanza baada ya kuhangaika muda mrefu kwenye ndoa yetu….”

Upande mwengine ni hadithi pia ya Tunu, bintiye Salma ambaye ana ndoto ya kuimba mbele ya Rais wa Jamhuri ya Kenya siku ya taifa lao linapotimiza nusu karne. Ndoto take inajikuta kwenye mtihani, pale puma ilipompandia njiani akikimbilia kuitimiza. Mwenzake, Kalole, anasikika akimuhimiza ajiinuwe na waende hivyo: “Kimbia Tunu. Kimbia…. Tutachelewa… tutakuta sherehe zimekwisha. Na kumbuka ulisema baba yako anakuja kukuona ukiimba. Lazima uharakishe Tunu.”

Lakini ndani ya hadithi mbili zinazokutana, ndimo pia munamoibuka hadithi nyengine tata na changamano kwenye jamii ya Kenya. Mojawapo ni ya mama yake Tunu, Salma, ambaye sio tu kuwa anabeba machungu ya kuzaa na Mchungaji anayemkana bintiye, bali pia taifa linalomkana yeye na jamii yake ya Wanubi wa Kibera.

“Ambapo kwa muda wote nimechukuliwa kuwa mimi si raia halali wa nchi hii. Nchi yangu mwenyewe. Nchi waliyozaliwa baba na mama yangu. Mimi ni Mnubi. Daima nimekuwa nikipigania kupata elimu na kazi ya heshima. Lakini, hapana, wanatoa madai yasiyowezekana. Eti nilete vyeti vya kuzaliwa vya bibi na babu zangu. Lakini waliishi Kibera miaka mia kadhaa iliyopita, nimesema. Tunafukuzwa kwenye maofisi ya serikali kama kuku waliokwenda kuchafua nyumba za matajiri,” analalamika Salma.

Kwenye  makutano ya hadithi hizi, mtazamaji anakutanishwa uso kwa iso na matokeo machungu ya dhuluma ya kijamii na kisiasa kwa watoto wa taifa la Kenya, mojawapo ni jaala ya akina Boss na rafikiye – watoto wanaoishi mazingira magumu mitaani, maarufu kama chokoraa. Na ndani yao, licha ya magumu wanayopitia, unakutana na sura nyengine ya ubinaadamu. Ni wao wanaosaidiana na Mwalimu Kulungu, Bibi Truvera na Kolela kumpeleka Tunu hospitalini.

Ujumbe wa hadhira kwenda nao nyumbani

Ndani ya kipindi cha nusu karne ya uhuru wake, taifa la Kenya limepitia kwenye masaibu kama haya, ambayo ingawa ni hadithi za mtu mmoja mmoja, jamii moja moja, na hata mtaa mmoja mmoja, kwa ujumla wake ndizo zinajenga moja ya taswira za Kenya iliyotusimamia mbele yetu.

Na zote zimo kwenye onyesho la Puma, ambalo baada ya kuliangalia kwa makini, hadhira inaondoka na ujumbe mmoja mzito – jamii inapaswa kuponyeshwa majeraha yake. Ndivyo alivyoiambia Kate, ambaye alikuwa sehemu ya hadhira: “Ukifiria zile ghasia zilizotokea, ni sisi vijana ambao tulizifanya kwa wingi. Na tukiwa kama watu tuliofanya ghasia zile hatukupona madonda yetu, tutayahamishia haya kwa watoto wetu. Na hilo si jambo zuri.”

 

Lakini kwa hadithi kusimuliwa ikasimulika katika onyesho la jukwaani na kuifanya hadhira iondoke na ujumbe halisi ambao mtayarishaji alitaka kiwe kifurushi cha mwisho kabisa kubebwa na hadhira yake kwenda nacho nyumbani, kunahitaji ubunifu mkubwa wa sio dhamira ya onyesho, bali pia lugha na ujenzi wa wahusika.

Nje ya jukwaa, nilikutana na waigizaji wenyewe. Mmoja wao ni Robert, ambaye kwenye Puma ndiye Mwalimu Kulungu anayekimbia hisia kali za mateso ya jana yake na kujificha nyuma ya hasira. “Mimi ndiye niliyebebeshwa dhamana nzima ya mchezo. Nilipaswa kuzitoa nguvu na hisia zangu zote ili ujumbe ufike kuwa haya yaliyotokea, basi tena. Imetosha!”

Kuna pia Janet, ambaye kwenye mchezo anacheza nafasi ya Truvera, mwanamke msakaji mali ambaye inamchukuwa muda kuujuwa ubinaadamu lakini anapoujuwa, anausimamia kwa nguvu sake zote. Yeye aliniambia mapenzi yake kwa sanaa ni makubwa mno kiasi cha kwamba ndio pumzi na uhai wake. “Nikipewa uhusika, huuingia ndani yake na nikaishi humo, hadi mtu akiniona njiani husema kuwa nilivyo jukwaani ndivyo nilivyo kwenye uhalisia.” 

Hili la kuuvaa uhusika na kuugeuza uhalisia, ndilo pia analosema muhusika Kolela, kijana wa miaka 20 aliyeigiza nafasi ya mtoto wa shule ya msingi, na kweli ukimuona sura yake na ukamsikia sauti yake jukwaani haikupitikii hasa kuwa si kitoto cha miaka 8.

 

“Yote inaanzia kwenye uzingatiaji. Kisha kitu cha pili ni kujiweka kwenye ule wakati wenyewe. Na jambo la tatu ni kufuatilia.”

Kuisimulia hadithi kama njia ya kuponya majeraha

Si jamii nyingi ulimwenguni zenye uthubutu wa kugeuka nyuma kuyaangalia madonda ya kihistoria yaliyosababishwa na ama mifumo yao ya kisiasa au kijamii. Badala yake, wengi huhiyari kuangalia mbele kwa kuamini kuwa kufukuwa makaburi kunaweza kuwa na maana mbaya kwa utulivu wa kijamii uliopatikana baada ya maafa kama yale ya Kenya ya mwaka 2006.

Hawa ni wale wanaoamini kuwa mtendwa ana wajibu wa kunyamaza, ikiwa kuyasema mateso aliyopitia kutamaanisha kuivuruga jamii yake. Huo si mtazamo wa Mkawasi, ambaye anasema lazima jamii iseme mikasa yake, watu wapewe nafasi kufunua madonda yao ili yaponywe. “Ni muhimu kusimamisha haki, maana bila ya haki hatuwezi kusonga mbele kama Wakenya na kama Waafrika. Hadithi zetu zitufanye tusisahau, kwani tukisahau tutarejea tena.”

Kwa hivyo, inahitaji ujasiri wa kiuandishi kuichukuwa hadithi chungu ya jamii yako na kuigeuza kuwa kipande cha sanaa, ambacho kinalenga kupaundaunda pale palipokwishabovuka.

 

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.