Licha ya kuwepo mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba katika visiwa vya Zanzibar, kuanzia tarehe 3 Januari 2016, Dk. Ali Mohammed Shein pamoja na viongozi wote wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walianza harakati za kuadhimisha sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutembelea na kufungua miradi mbali mbali iliyoanzishwa na serikali ya awamu iliyomalizika.
Akiwa kisiwani Pemba, siku ya tarehe 6 Januari kwa nyakati tofauti, Dk. Shein alisikika akisema kwamba yuko madarakani kihalali na kwamba yupo pamoja na uongozi wote wa serikali yake, akiwataja makamu wake wa kwanza na wa pili na mawaziri, huku akiwabeza mawaziri wa Chama cha Wananchi (CUF) waliosema wamejiuzulu kuwa “hao wanaodai kujiondoa serikalini huo ni uamuzi wao wenyewe”.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Dk. Shein anaamini kuwa yeye na serikali anayoingoza kuendelea kuwepo madarakani wapo hapo “si kwa uamuzi wake” na wala yeye hana “ubavu” wa kujiweka madarakani bali ni katiba ambayo imempa nguvu hiyo, ambayo kama kuna mtu anaipinga basi akafanye hivyo mahakamani.
Alichokikusudia Dk. Shein ni kupingana na wanoharamisha uwepo wake akiwa kama rais wa Zanzibar, kwa kile wanachokiamini kwamba muhula wake ulimalizika kwa kunukuu Kifungu 28(2) cha Katiba ya Zanzibar, ingawa hoja yake inasimamia Kifungu 28(1), ambacho ni hicho cha 28(2) kwa kanuni za kutafsiri sheria.

Lakini Dk. Shein akasahau kwamba ukimya wake juu ya mgogoro mzima unaoendelea kuitafuna Zanzibar na Tanzania, tangu ulipofutwa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na Jecha Saluma Jecha, pamoja na uhalali wake wa kuendelea na madaraka baada ya kufutwa kwa uchaguzi, ilikuwa ni njia salama kwake kubakia na madaraka hayo japo kwa njia za magube.

Yumkini Dk. Shein alikuwa anasuburi mamlaka husika zinazopaswa kutoa tafsiri za kisheria na katiba, ili zitoe tafsiri juu ya migogoro hii yote ndiyo maana akawataka wanompinga yeye kubakia madarakani kama rais wa Zanzibar basi wafungue shauri Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Kuwatamkia watu hadharani kwamba yeye ndiye rais halali, bado kunaonesha kuwa Dk. Shein hajiamini kuwa kweli ndiye rais na kwa hakika hakujampa uhalali wa kisheria wa kuwa rais. Kifungu 28(2) cha Katiba ya Zanzibar kinamkalia kooni na kumuambia kwamba yeye siye.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.