Hivi karibuni, Balozi Seif Ali Iddi alisikika akisema mbele ya waandishi wa habari kwamba licha ya kuwa hajui kilichozungumzwa kati ya Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad tarehe 21 Desemba 2015, wala kati ya Rais Magufuli na Dk. Ali Mohammed Shein siku tano baadaye huko Ikulu ya Magogoni, lakini anachojua yeye Rais Magufuli amewaambia waje warejee uchaguzi.

Hapana shaka, kauli hiyo imewachanganya wananchi walio wengi kwa kuwa wanachokijua ni tafauti na alichokizungumza yeye Balozi Iddi juu ya mgogoro wa kisiasa ulioanzia tarehe 28 Oktoba 2015 baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kuufuta uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Wazanzibari, Watanzania na dunia kwa ujumla inajua kwamba kuna kamati maalum yenye wajumbe sita ikiongozwa na Dk. Shein, na kuhudhuriwa na Maalim Seif, Rais Mstaafu Amani Karume, Rais Mstaafu Salmin Amour Juma, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na yeye, Balozi Idd. Kwa mujibu wa Dk. Shein, Rais Magufuli na Maalim Seif, kamati hiyo inaendelea vizuri na mazungumzo na wakimaliza kazi yao, watatoa taarifa rasmi kwa wananchi.

Ikiwa alichokizungumza Balozi Iddi si cha kweli juu ya kilichoagizwa na Rais Magufuli, basi Balozi Iddi atakuwa amepotoka kiuongozi, na mwenyewe ajipime kama kweli anafaa kiongozi katika wakati ambapo nchi imo kwenye mgogoro.

Hadi sasa, hakuna aliyezungumzia juu ya kufanyika kwa uchaguzi huo kati ya Rais Magufuli, Dk. Shein na Maalim Seif, lakini yeye Balozi Iddi anapita akiutangazia umma kuwa huo ndio muelekeo wa mazungumzo, tena kama kiongozi wa serikali na siyo tu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Kwa sababu sote tunafahamu kwamba uchaguzi wa marudio ni msimamo wa CCM Zanzibar na Jecha Salim Jecha na wala si wa ZEC wala CUF.

Kwa kujizusha mbele ya umma akitumia ofisi ya serikali, kunawapa hisia tofauti wananchi kwamba labda Rais Magufuli amezungumza na Balozi Iddi alipokutana naye, kitendo ambacho kinawatoa imani wananchi kwa Rais Magufuli. Kwa kuwa hadharani akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Ulinzi na Usalama, na mtu anayependa ukweli na anayechukia unafiki kama anavyosikika mara kwa mara katika hutuba zake, hakusikilikana akitamka maneno hayo aliyoyasema Balozi Iddi, basi sasa Rais Magufuli atuweke wazi.

Ikiwa Balozi Iddi aliyasema haya kwa utashi wake na wenzake wachache visiwani Zanzibar ili tu kumgeuza Rais Magufuli kituko na kumfanya aonekane mnafiki mbele ya Wazanzibari, Watanzania na dunia kwa jumla, basi ni nafasi ya Rais Magufuli kumuonya Balozi Iddi, kwani inaonekana kuwa ni mazoea kwa balozi kusema maneno kwa waandishi wa habari ikisha akarejea kukanusha kile alichokizungumza.

Rais Magufuli, wewe ni mtu wa Mungu, unampenda Mungu, unayemaini baraka za mapenzi ya Mungu kwa wasemao kweli. Nasaha zangu kwako ni kuwa uchukue hatua kwa wanokunafikisha ili ubaki katika mapenzi ya Wazanzibari na Watanzania na ili ufanikiwe na kaulimbiu ya yako ya “Hapa Kazi Tu”, kwani ili kauli hiyo itekelezeke unahitaji ukweli kwa kiwango chote na kusiwe na hata chembe ya kinafiki.

Sambamba na hilo, Dk. Shein na Maalim Seif munapaswa kuingilia kati pia. Ikiwa Dk. Shein ataipuuzia kauli hii iliyotolewa na msaidizi wake, basi Wazanzibari, Watanzania na dunia wana haki ya kutokukuelewa kama walivyokuelewa vizuri ulipofanya mazungumzo na Rais Magufuli. Na Maalim Seif naye kama ataipuuzia kauli hii iliyotolewa na mtu ambaye mnashiriki naye mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo Zanzibar, basi pia Wazanzibari, Watanzania na dunia hawatamuelewa kama ambacho walimuelewa vyema alipofanya mazungumzo na Rais Magufuli.

Wito kwa Rais Magufuli, Dk. Shein na Maalim Seif ni kuwa lazima watoke hadharani kupinga au kuitilia mkazo kauli ya Balozi Iddi ili waweweke sawa wananchi, kwani kila kukicha akili zao zinaparaganywa na makundi ya watu na kauli zinazotafautiana. Huu ni wajibu wa uongozi kuonesha njia na kutokuruhusu jamii kuparaganyika, tukizingatia kwamba wao wananchi ndio wenye nchi na ni haki yao kujua ukweli wa nchi yao

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.