Tukiwa tunaeleke kwenye Sherehe za Mapinduzi ambazo zimekuwa zikifanyika kwa miaka yote tokea kutokea kwa Mapinduzi ya 1964. Maana halisi ya sherehe hizo ni kukumbuka na kuadhimisha ukombozi wa Wazanzibari na matumaini ya mabadiliko ya hali za wananchi wa Visiwa hivi.
Kwa bahati mbaya moja katika jambo ambalo Mapinduzi hayakufanya ni kuleta maridhiaano (reconciliation) baina ya watu ambao walipita katika siasa za ukinzani na uhasama mkubwa. Mbinu a maridhiano zilizofanywa kama vile kuleta ndioa za pamoja hazikuwa sahihi kwa sababu hapakuwa na hoja hiyo maana watu walikuwa wakioona karne na dahari ila ulikuwa ni uchu wa watu waliotaka kuishi na Wazanzibari wa ngozi nyeupe.

 

By Ally Saleh
By Ally Saleh

Pia hatua nyengine ya maridhiano ilojaribiwa ya kuchukua ardhi kwa waliokuwa nayo kwa wingi kiasi cha ekari 90,000 na kugawa kwa wasiokuwa nayo ilikuwa pia ni ya msingi lakini ilikosa mipango na maelekezo kiasi ambacho ilipoteza maana na hivi sasa, bila ya utafiti wa kina, mtu aweza kusema sehemu kubwa ya ekari hizo zimerudi kwa wale wale wenye kipato.
Miaka kadhaa ya awali ya Mapinduzi tulishindwa kama nchi kuunganisha Zanzibar kama taifa. Bado rangi, asili na kabila vikawa ni vichocheo vya mitizamo yetu na maamuzi yetu. Mapinduzi yakashindiwa kuzama katika nyoyo za watu na kukawa na mgawanyo wa wazi wa hawa ndio na hawa sio na kwa sababu hilo lilileta manufaa ya kisiasa likapigiwa chapuo na kuendelezwa. Chuki iliyopandwa mwanzo wa Mapinduzi inaendelea hadi leo.
Tumejiweka kama nchi na taifa katika mawazo-pingu. Kijana mdogo wa leo amejazwa fikra kale kiasi ambacho uwezo wake wa kufikiri anafikiri kama mtu wa miaka ya 1950 au 1960. Kwa mfano si ajabu kumkuta kijana, tena pengine msomi kulazimisha hoja za Hizbu na Afro Shirazi, hoja za utumwa, hoja za madhila ambao kwa vyovyote sio Zanzibar tu waliopitia, bali ni mfumo wa kijamii na kiuchumi ambao ulikuwepo wakati fulani.
Ila matukio hayo yamejazwa miongoni mwa watu wetu kiasi cha kuamini kuwa Zanzibar ni nchi ya kutawaliwa na tabaka fulani tu la Wazanzibari ambao hao huwa wanajikusanya chini ya chama kimoja na kuwa wao ndio wenye haki na sauti. Pamoja na nchi kuingia katika vyama vingi, ambapo maana yake ni kuwa upo uwezekano wa chama chochote kushika dola, lakini ndani ya vilango vya nyoyo zao hilo halipo na halitakuwepo na maana kukawa na msemo maarufu wa kuwa “nchi haitoki kwa vikaratasi.”
Na kweli nchi imekataliwa kutolewa kwa vikaratasi mara kadhaa ikiwemo 1995, 2000, 2005 na 2010. Lakini yalitokea 2015 ndio hitimisho kamili kuwa nchi hii haina haja kabisa ya mfumo wa ushindani wa vyama maana hakuna nafasi kabisa wa chama chochote kushinda uchaguzi isipokuwa kimoja tu.
Kilichotokea 2015 ni mapinduzi baridi, uhuni wa kisasa na upokaji na ubakaji wa demokrasia katika jua la adhuhuri. Ni ubabe wa kisiasa, umwamba wa watawala na kuwa na kutokuwepo kwa woga wa kufanywa chochote na yeyote (impunity). Hakuna chengine cha kuelezea kilichotokea zaidi ya hilo neno.
Jumanne ijayo tunafanya Sherehe za Mapinduzi kuadhiisha miaka 52 lakini nchi ikiwa katika mgogoro mkubwa wa kiasa. Ikiwa imegawika pande mbili kuliko ilivyotokea wakati wowote tokea turudishe mfumo wa siasa za ushindani mwaka 1992. Imezama, imejinamia, inasononeka kwa kukosa suluhu ya utumiaji wa mabavu wa watu ambao japo wanaimba demokrasia lakini bado hawajakuwa tayari nayo kabisa.
Tunafanya sherehe huku kukiwa na kiza. Huku kukiwa na mvutano ambao ni wazi utaendelea kuigawa nchi miezi na miaka kadhaa baada ya sherehe hizi iwapo suluhu ya kweli na ya kudumu haitapatikana. Tunaambiwa kuna mazungumzo yanaendelea na tunaomba yatoe suluhu lakini tumeanza kuwa na wasi wasi kwa kauli zinazotolewa na viongozi wakati mazungumzo yakiendelea.
Na ndio maana baadhi yetu tunaona sherehe hizi za kuadhimisha Mapinduzi zitatumika vibaya. Zitatumika kwa kuhalalisha utawala uliopo madarakani kwa maana ya kujichimbia ( entrench) na hivyo kujijengea uhalali wa kuwa una haki ya kuendelea madarakani pamoja na tata kadhaa za kisheria na kikatiba lakini kifungu 28(1) kimekuwa kikifanywa ni mjarab kukamilisha dhamira hii.
Tunaamini sherehe hizi zitatumika kuhamasisha wanachama wa chama chao kuwa ni wao walio madarakani na kama tulivyoambiwa hawataondoka mpaka apatikane Rais ataechaguliwa. Na wakati suala la utata wa uchaguzi likiwa juu ya meza, matamko kinzani yamekuwa yakitolewa.
Kwa fikra zangu sherehe hizi zinaweza kutumika kabisa kuua mazungumzo. Naona hivi hivi mabango yatakayobebwa katika sherehe hizo Uwanja wa Amani yakija na lugha ngumu na za vitisho na kukataa chochote kile kinachoendelea…naona mabango ya kimapinduzi kuwa ndio yatayotawala.
Rais Dk John Pombe Magufuli naamini mpaka sasa ana nia ya kutaka kushiriki sherehe hizo. Naamini atakuja pia kwa sababu ni chama chake ndio chenye kufanya sherehe hizo. Na pia ni mgombea wa chama chake ndio aliye katika utata wa kisheria na kikatiba na angetaka kuonyesha kumuunga mkono hadharani.
Lakini kuna tatizo kubwa la kupelekea ujumbe ( message sending) iwapo Dk Magufuli atahudhuria sherehe hizo nalo ni lile la kutoa leseni ya hadharani ya kuwa anabariki utawala huo ambao umeweza kuthubutu kuendelea kuwa madarakani kwa miezi mitatu bila ya Baraza la Wawakilishi chombo muhimu sana katika nchi yoyote ya kidemokrasia.
Dk. Magufuli, pengine hawajui Wazanzibari kama ninavyo wajua mie, ajue kuwa akishiriki sherehe hizo itakuwa ndio kufa kwa mazungumo maana watu wa chama chake hawatakuwa na hawataona umuhimu wa kuendelea nayo. Na naamini wakipata nguvu hiyo na utambulisho (power and recognition) wanaweza moja kwa moja wakatangaza kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.
Kila mtu anajua kuwa uchaguzi wa marudio hauna maslahi na Zanzibar maana hautatatua tatizo liliopo hivi sasa kwa sababu nani ataamini marudio wakati donda la sasa halijatibiwa. Lakini Dk. Magufuli bado Wazanzibari wana imani na wewe kuwa una nia ya kulimaliza tatizo hili, lakini watapoteza imani na wewe kwa kushiriki na kuja kubariki.
Kitu kimoja nina hakika hutafanya makosa. Hutafanywa uamini kuwa chama chako ndio kila kitu Zanzibar na kwamba kila inachotaka kufanya inaweza kufanya bila kujali haki ya vyama vyengine. Kwamba eti uchaguzi utafanyika hata chama kikuu cha upinzani kikisusia kwa sababu kuna vyama vyengine.
Kwa sasa uko katika nafasi ya kujua kuwa CUF wameibiwa uchaguzi mara nne na hii ya sasa ni ya tano na kuwa wamekuwa wavumilivu ukitoa maandamano ya 2001. ila uvumilivu unaweza kuwa na mwisho au kutafuta njia mbadala au kama wakishindwa yote wanaweza kuamua kutoshiriki kabisa katika mfumo wa siasa za ushindani maana hauna maana wala faida kwao.
Jitayarishe miaka mitano yako hii, kama itakuwa ya mwanzo au utaendelea, na moja katika hilo, maana haki ya kutawala si ya kundi moja au chama kimoja tu hapa Zanzibar.

Makala hii imechapishwa kwa mara ya kwanza za gazeti la Mtanzania la tarehe 6 Januari 2016.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.