OKTOBA, 1987, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alihutubia Baraza la Mapinduzi la Zanzibar juu ya kile kinachoweza kuelezewa kama “Mzimu wa Watu wa Kale” unaosumbua mustakabali wa siasa Visiwani Zanzibar kwa zaidi ya nusu karne sasa. Na kama ulivyokuwa msemo wa enzi za utawala wa Sultani karne ya 19, kwamba “Wapigapo chafya Visiwani Zanzibar, Bara huugua mafua”; ndivyo ilivyo hadi leo, kwamba, “Zanzibar inapochafuka kisiasa, Muungano wa Tanzania huugua”.

Mwalimu aliwaambia hivi: “Mapinduzi ya Zanzibar ya umwagaji damu yasingetokea, mwaka 1964, kama Waingereza na Serikali ya Sultani wangeendesha uchaguzi huru na wa haki. Chaguzi zote zilichakachuliwa kuwapa ushindi ZNP/ZPPP, hivyo wananchi hawakuwa nalingine ila kuchukua mapanga kuiondoa Serikali ya mseto ya ZNP/ZPPP”, iliyoingia madarakani Desemba 10, 1963”.

Na Joseph Mihangwa
Na Joseph Mihangwa

Ni katika uchaguzi wa mwisho uliofanyika Julai, 1963, Vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) cha Ali Muhsin (wakati mwingine huitwa HIZBU kwa makosa, kwa sababu Chama cha “Hizbul Watan Ratatul Sultan” – NPSS – HIZBU; kwa maana ya “Chama cha Kitaifa cha Watawaliwa wa Sultani”, kilichoanzishwa Kiembe Samaki na kikundi kidogo cha Wakulima, kilikufa baada ya kuundwa kwa ZNP mwaka 1955) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP]) cha Mohamed Shamte, vilipoungana kupambana na nguvu ya Afro Shirazi Party (ASP) cha Abeid Amani Karume, na kushinda kwa wingi wa viti vya Bunge na kukabidhiwa Serikali chini ya Mohamed Shamte kama Waziri Mkuu.

Kisha Mwalimu akaelezea kile kilichofuatia baada ya Mapinduzi, akasema: “Kusema kweli, (Rais Abeid Amani) Karume alikuwa kielelezo cha ukatili na ukandamizaji Visiwani; alitawala kwa mkono wa chuma. Nasema, kilichotokea ni kile nilichobashiri kingetokea; kwamba Wazanzibari wakaanza kuuana wao kwa wao, na baadhi yenu hapa mnayajua majina ya watu wasio na hatia waliouawa kikatili na ambao hawakuwa wanachama wa HIZBU wala Chama chochote, bali ASP; waliuawa mmoja baada ya mwingine, hovyo hovyo na kwa ukatili wa kutisha!”.

Akilituhumu Baraza la Mapinduzi kwa kuridhia ukatili huo, Mwalimu alisema: “Hamuwezi kuepuka dhambi ya umwagaji damu huu, vitisho na vurugu; wala Baraza hili haliwezi kuwatumikia vyema Wazanzibari kwa kuwa limeghubikwa na ukatili mkubwa dhidi ya baadhi ya Wazanzibari”.

Mwalimu akasema, ilikuwa ni ujinga usio kifani, kwa watu kujengeana chuki na mauaji kwa misingi ya vyama vya kisiasa vya enzi za harakati za uhuru; akasema: “Sisi Bara tulikuwa na vyama pia; tulikuwa na TANU (Tanganyika African National Union), tulikuwa na “Congress” (African National Congress), tulikuwa na AMNUT (All Muslim National Union of Tanganyika), tulikuwa na UTP (United Tanganyika Party); lakini shughuli zetu za kisiasa hazikuhusu kuinuliana mapanga; tulivishinda (sisi TANU) vyama hivyo kimoja baada ya kingine hadi vikasambaratika. Kisha tukawaambia baadhi ya Viongozi wa vyama hivyo wajiunge na TANU na wakafanya hivyo. Leo hatuvikumbuki na hatuna sababu ya kufanya hivyo, vyama hivyo mfu ila pale tu tunapoandika historia. Lakini kwa misingi ya siasa za leo, hiyo ni historia tu”, alisema.

Huku akiwakazia macho Wajumbe wa Baraza hilo, Mwalimu alisema kwa kuhoji: “Sasa mnataka tuongoze nchi hii (Zanzibar) kwa mtizamo na mihemuko ya jana au ya leo? Tutizame nyuma kiasi gani tunapoongoza nchi hii? Je, tumhukumu mtu kwa matendo yake ya jana au kwa yale ya leo?”

“Mungu husamehe; ni wangapi kati yetu tutastahili kuwa na matumaini ya Paradiso kama Mungu atang’ang’ania dhambi zetu wakati wote?” alihoji Mwalimu.

Akasema: “Leo watu wanakumbushwa kijinga kabisa, kwa kuambiwa “Wewe ulikuwa HIZBU” na wengine wanakumbushwa, “Baba yako, kama si pamoja na Babu yako, walikuwa HIZBU”. Sasa nizipeleke wapi dhambi za Baba au Babu yangu? Huu ni ubaguzi mbaya na wa kijinga”.

Akaonya akisema: “Msiturejeshe nyuma; wala isiwe hamu yenu kuturejesha nyuma kwenye HIZBU, ZPPP; Vyama hivi ni mfu. Kwa jina la mbingu, kwa nini HIZBU mfu itughadhabishe leo kana kwamba juzi ndiyo leo? Mnasumbuliwa na kivuli cha wafu, mizuka na mizimu ya waliokufa na kujaribu kutugawa bila ya sababu za msingi”, alionya Mwalimu.

Hotuba ya Mwalimu ingali muhimu na hai hadi leo tunapozungumzia siasa za Zanzibar ambazo zimewagawa wananchi kwa misingi ya vyama mfu vya enzi za harakati za uhuru, ambapo Chama cha Wananchi (CUF) Visiwani kinachukuliwa kama mzimu unaowakilisha HIZBU, na CCM Zanzibar, kuwa mzimu unaowakilisha ASP.

Chimbuko la mgawanyiko na chuki hizi, alibaini Mwalimu, ni Mwasisi wa Taifa hilo, hayati Abeid Amani Karume ambaye, kufuatia Mapinduzi ya 1964, aliapa na kupitisha Sheria (decreed) kwamba, pasingekuwa na uchaguzi Visiwani kwa miaka 50. Ni kusema kwamba, kama Karume angekuwa hai, uchaguzi wa kwanza Visiwani ungefanyika mwaka 2014, hatua ambayo Mwalimu aliifananisha na kusimika Usultani Visiwani.

Karume aliagiza kupitia “Agano” (Covenant?) kwa hati ya siri ambayo ndilo kibuyu cha mizimu ya kale kinachosumbua Zanzibar na Muungano hadi leo kwamba, Wazanzibari waliowahi kuwa wanachama wa vyama vya siasa mbali na ASP Visiwani pamoja na jamaa zao, wasipewe nafasi za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na katika Serikali ya Muungano.

Siri hii ilivuja mwaka 1982, wakati Dakta Salim Ahmed Salim, alipoteuliwa na Mwalimu kuwa Waziri wa Mambo ya Nje; pale Mawaziri wawili Waandamizi Wazanzibari katika Serikali ya Muungano, Mabwana Abdullah Natepe (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Usalama wa Taifa) na Ali Mzee (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais), walipokwenda kwa Waziri Mkuu wa wakati huo, hayati Edward Moringe Sokoine, na kudai kwamba, walitumwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe na Seif Bakari, kuitaka Serikali ya Muungano (Nyerere) ifute uteuzi wa Salim kwa sababu ulikiuka matakwa ya hati hiyo ya Siri ya enzi za Karume.

Salim Ahmed Salim, alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa Umma Party (UP) cha Abdulrahman Babu, kilichoratibu kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa, Mapinduzi ya Januari 1964, na kufuatia Mapinduzi hayo, Babu aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, na Salim akawa Balozi wa Zanzibar nchini Misri.

Sokoine, Waziri Mkuu ambaye hakuvumilia upuuzi wa aina hiyo, aliwafukuzia mbali mawakala hao wa mizimu, na nyota ya Salim Ahmed Salim ikazidi kung’ara ndani ya nchi na Kimataifa.

Chuki ya Karume kwa Wazanzibari waliowahi kuwa wanachama wa vyama vya siasa mbali na ASP pamoja na wasomi ilikuwa dhahiri. Na katika hali ya ukatili uliotokana na kuhofia nafasi yake, Karume aliamini kwamba “Mwanamapinduzi” wa kweli ni yule asiye na elimu.

”Miongoni mwa Wanamapinduzi, hakuna hata mmoja mwenye elimu ya darasa la 12. Nitatoa zawadi ya pauni 5,000 za Uingereza, kwa yeyote atakayejitokeza kunionesha mtu wa aina hiyo”, alisikika siku moja akitupa changamoto kwa wasikilizaji wake.

Mmoja wa “Wanamapinduzi” wa Karume mwenye kuvaa sare, alikuwa Kanali Seif Bakari, kiongozi wa mauaji kwa “Wapinzani” wa Karume na wanachama wa zamani wa ZNP/ZPPP na Umma Party.

Siku chache kabla ya kuuawa, Karume alikuwa ametupa gerezani watu 19 (“wachunga ng’ombe” walivyoitwa kiusalama) kwa tuhuma za uhaini. Mara tu Karume alipouawa, Bakari aliwatoa gerezani na kuwaua wote kwa risasi kama mwendelezo wa sera za siasa na ukatili wa Karume.

Kanali Seif Bakari, ambaye kwa fikra za waabudu mizimu ya vyama mfu Visiwani, alionekana ndiye mrithi sahihi wa Karume asiyehojika, aliikosa nafasi hiyo baada ya Mwalimu kucheza vizuri sana karata za kisiasa ambapo, Mwalimu mwenzake kitaaluma, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, aliukwaa urais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kabla ya hapo, Jumbe alikuwa Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais akishughulikia Muungano.

Mzania wa Kisiasa haujabadilika

Mzania wa siasa Visiwani haujabadilika tangu enzi za harakati za uhuru, kati ya vyama vishiriki kama inavyothibitishwa na matokeo ya chaguzi za kila mara Visiwani. Na kama ilivyokuwa enzi za harakati za uhuru, ambapo vyama vya ASP na ZNP/ZPPP vilionesha nguvu sawa na kuipasua nchi katikati kisiasa na kijamii, ndivyo ilivyo hivi sasa, ambapo CCM Zanzibar na CUF Zanzibar vimeipasua nchi vipande viwili kisiasa na kijiografia na kuzaa kile kinachoweza kuitwa kisiasa kama “deadlock” au mtanziko.

Mtanziko huu umeibua mambo makuu matatu, hasa kufuatia kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa: (a) Kwamba si CCM Zanzibar wala CUF Zanzibar ni Chama cha kitaifa; vyama vyote vina nguvu sawa na hivyo vimeigawa nchi katikati (b) Kwamba Mzani wa kisiasa haujabadilika tangu miaka ya 1950 ya enzi za harakati za uhuru na kufufua vidonda vya kale (c) Kwamba uhasama wa kisiasa wa kale umefufuliwa kufuatia mfumo wa vyama vingi nchini, na uongozi uliopo hauoneshi kuwa wa aina ya unaoweza kuupatia suluhisho kwa manufaa ya nchi ila kujitapa tu kwa “ukada” na umamluki wa kivyama, badala ya kuwekambele maslahi ya nchi.
Ni historia kujirudia?

CUF kimedai mara nyingi kupokonywa ushindi naCCM kwa mbinu chafu kama ilivyozoeleka hapo kale, kwa ASP kupokonywa ushindi kila mara na ZNP (baadayeZNP/ZPPP) enzi za harakati za Uhuru.

Hata kama tutakubali hivi leo “nembo” za kuchonga, uhasama na kuchafuana miongoni mwa Wazanzibari kwa misingi ya “mzimu wa watu wa kale”, kwamba CUF Zanzibar ni mtoto wa ZNP/ZPPP, na CCM Zanzibar ni mtoto wa ASP ndani ya vazi jipya; vipi leo CCM Zanzibar kifurahie mkuki kwa nguruwe (CUF) na kwake (CCM) kione uchungu, kinapokataa kukiri nguvu ya CUF na kuachia demokrasia na amani vitawale?

Matamko ya baadhi ya viongozi yenye kukera, kama vile, “Uhuru wa Zanzibar hauwezi kukabidhiwa kwa wapinzani” au “Tuko tayari kufungua sanduku la silaha za Mapinduzi, kwa maana funguo tunazo”, hayaashirii siasa za kistaarabu na usawa Visiwani bali ni ishara ya kupagawa na nguvu ya mizimu ya watu wa kale.

Tanzania Bara nayo haisameheki kwa vioja hivi. Miaka kadhaa iliyopita, ilipoonekana nguvu ya kiongozi wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, kutikisa mhimili wa siasa Zanzibar na kuonesha uwezekano wa kushinda kuwa Rais wa Zanzibar na hivyo kuwa pia Makamu wa Rais wa Muungano; Serikali ilijiuliza: Itakuwaje siku moja Hamad wa CUF akawa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati Bara kuna CCM? Je, mambo yatakwenda kweli?.

Haraka haraka, ikateuliwa Tume ya Jaji Mark Bomani iliyopendekeza na kukubalika kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano, kwamba Rais wa Zanzibar asiwe tena Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano, na badala yake awe mmoja tu wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano. Haya yote ni udhaifu kwa kukataa kukiri ukweli na nguvu ya demokrasia kwa watawala.
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kufuatia uchaguzi wa mwaka 1963 kabla ya uhuru wa Zanzibar. ASP kilishinda kwa wingi wa kura, ingawa Muungano wa ZNP/ZPPP walishinda kwa uwingi wa viti vya Bunge na kukabidhiwa Serikali. Mara ZNP/ZPPP waliposhika madaraka, walikataa kutafuta suluhu kwa mtanziko wa kisiasa ulioendelea kuvuma.

Na kama tunavyojua, badala ya kukiri na kukubali hali halisi ya mambo na kuunda Serikali ya Kitaifa na wapinzani wakati hali ilikuwa bado inaruhusu, lakini kwa ujinga wao, ZNP/ZPPP waliendeleza matumizi ya nguvu za dola kuzima upinzani, wakiwaona ASP kama raia daraja la pili.

Matokeo ya hayo sote tunayajua; kwamba Serikali ya Shamte haikudumu madarakani kwa zaidi ya wiki tatu, ilipopinduliwa na “wanaharakati” wazalendo wasio mateka wa vyama vya siasa bali kwao ilikuwa “Taifa kwanza, siasa baadaye”.

Ilivyo sasa, hali ya kisiasa Visiwani haifurahishi. Yaliyotokea, kwa maana ya kitendo cha kufuta uchaguzi kinyemela mwaka huu na yanayoendelea kutokea sasa yanaweza kugeuka historia kujirudia kwa kuruhusu kibuyu cha “mzimu wa watu wa kale” kuvuruga demokrasia na amani. Ni mahoka, mizuka na mizimu inayowasumbua Wazanzibari kwa kujiruhusu kuwa “washirikina” na “ushirikina” wa aina hii ni sumu kwa Zanzibar, Wazanzibari na kwa Muungano pia.
Lazima tukubali ukweli, kwamba katika nchi yenye kutekeleza demokrasia ya kweli, raia wote ni sawa; hakuna raia daraja la kwanza na raia daraja la pili. Ikiwa hivyo, nini maana ya demokrasia, haki za raia na za mwananchi?
Viongozi makini siku zote wajaribu bila kuchoka, kutafuta suluhisho kwa hali kama hii kabla ya mikasa na maafa kutokea.

Na kwa kuwa Katiba ya Zanzibar (ibara 9) ya 1984 inatamka wazi kuwa, “Zanzibar itakuwa ni nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii”, na kwamba, “Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe”, basi, mgogoro wa kisiasa unaoisibu nchi kufuatia kufutwa kwa uchaguzi kinyemela na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), hauna budi kutatuliwa na Wazanzibari wenyewe, si kwa kuongozwa na “mzimu wa watu wa kale”, bali kwa njia ya “demokrasia” kwa tafsiri na maana halisi ya neno hilo.

*Makala ya Joseph Mihangwa kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 30 Disemba 2015

One thought on “Wazanzibari kataeni kuabudu mizimu”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.