Sasa ni mwaka 52 tangu Uhuru wa Disemba 1963 na Mapinduzi ya 1964 ambavyo, kwa njia moja ama nyengine, vilitarajiwa kuwapatia Wazanzibari fursa ya kujitawala wenyewe. Sijiweki kwenye ubishani wa kipi kilikuwa halali kati ya viwili hivyo, maana nikiwa kijana niliyezaliwa miaka ya mwishoni mwa miaka ya ’80, ubishi huo hauna maana yoyote kwangu na nayachukulia yote mawili kuwa ni matukio ya kihistoria ya nchi yangu.

Badala yake, najikita kwenye ukweli kuwa matarajio ya Wazanzibari walio wengi kwamba uwezo wa kujitawala ungeleta manufaa makubwa kwa wananchi walioteseka kwa muda mrefu chini ya unyanyasaji na ukandamizwaji. Wengi walitumaini kuyafaidi “matunda ya kuwa huru”, ikiwa ni pamoja na kuona haki zote za kiraia, kiuchumi na kijamii zinalindwa na serikali inayokaa madarakani kwa niaba na ridhaa yao.

 

Na Khelef Nassor
Na Khelef Nassor

Lakini miaka hii 52 imeshuhudia uvunjwaji mkubwa wa haki hizo na upondwaji wa demokrasia na Zanzibar iliyopaswa kuongoza mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Kati kwa rikodi yake ya kihistoria, imekuwa ikiwa “kituko” cha kuchekwa na kudharauliwa na wengine – kisa cha karibuni kabisa kikiwa ni mgogoro wa kisiasa unaoendelea baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuamua kuufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwa utashi wake na Chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Wengine wanaipa jina hali hii ya Zanzibar kuwa ndio “utamaduni wa kisiasa” wa visiwa hivi, wakishingizia historia ya kabla ya Uhuru wa 1963 na Mapinduzi ya 1964. Mimi kijana niliyezaliwa zaidi ya miaka 20 baada ya matukio hayo mawili, sitaki kukubali kuwa, kwanza, huu ni utamaduni wetu Wazanzibari na, pili, ikiwa matukio ya sasa yana mafungamano na hayo ya nyuma. Kilichopo na ninachokiona ni kuwa wale wanaofaidika na huu wanaouita “utamaduni wa kisiasa” wanayatumia matukio ya kihistoria kuhalalisha maovu yao dhidi ya visiwa hivi.

Na walianza mbali. Tangu uchaguzi wa kwanza wa mwaka 1995 uliofanyika miaka mitatu tokea kuja tena kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, hadi uchaguzi wa karibuni kabisa, miaka zaidi ya miaka 20 baada ya Katiba na sheria za nchi kuruhusu uwepo wa mfumo huu wa kisiasa. Mazingira yaliyojengwa na CCM kuulea mfumo huu wa vyama vingi hayajawahi kuwa ya kuridhisha tangu hapo. Katika uchaguzi huo na nyengine zilizofuatia hapo, upinzani visiwani Zanzibar umekuwa ukinyimwa haki ya kimsingi ya kufanya siasa.

Vipindi vya uandikishaji, kampeni, upigaji kura na hata kwenye ukusanyaji na utangazaji matokeo, CCM haijawahi kuwa na dhamira njema na haki za kisiasa za Wazanzibari, na imekuwa ikitega kila mitego kuhakikisha kuwa wananchi walio wengi hawafanyi maamuzi juu ya hatima yao kiutawala.

Matokeo yake, watu wengi wenye haki ya kujiandikisha kupiga kura huwa hawapewi haki hiyo, huku wakipewa nafasi  wasiokuwa na haki hiyo ili kupunguza idadi ya kura za wagombea wa upinzani na kuwaongezea mgombea wa CCM.

Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar inampa haki Mzanzibari Mkaazi kuwa mpiga kura, lakini ili kuwa mkaazi ni lazima kukaa kwenye eneo husika ndani ya kipindi cha miaka mitatu mfululizo, ambako nako lazima kuridhiwe na ngazi ya chini kabisa ya utawala, ofisi ya sheha, ambayo daima imekuwa ikila njama za kuwanyima Wazanzibari wengi wanaoaminika kuwa wapinzani haki hiyo.

Upinzani unapovuuka kwenye uandikishaji – na kwa kuwa ni wengi huwa wanavuuka – hukamatwa kwenye kipindi cha kampeni. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na makundi ya kihuni kama yale yaliyopewa majina ya Janjaweed na Mazombi, hufanya kila lililo kwenye uwezo wao kuyafanya mazingira ya kampeni kuwa magumu na ya kukatisha tamaa kwa vipigo, mashambulizi, vifungo na mateso mengine.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya serikali – redio, televisheni na gazeti – ambavyo vinalipiwa kwa kodi ya wananchi wote, hugeuka kuwa idara ya habari na uenezi ya CCM tangu mwanzo hadi mwisho, tayari kuandaa na kurusha taarifa, habari, makala au vipindi vyovyote vyenye kila aina ya upendeleo kwa CCM na kila aina ya chuki kwa upinzani, ukiwemo uongo, uzushi na fitina.

Katika chaguzi zote zilizopita tokea ule wa 1995 hadi wa 2015 tumeshuhudia vituko vingi vikifanywa na CCM ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu wapigakura wao kupiga kura mara zaidi ya mara moja, kupenyeza kwa masanduku ya kura feki kwenye vituo na zaidi ya yote kutumia nguvu za dola kwa kuwatisha mawakala wa CUF pale wanapoona wanatendewa ndivyo sivyo kwenye vituo na mwishowe humalizika kwa mgombea wa CCM kutangazwa mshindi.

Taasisi nyingi za uangalizi wa uchaguzi za ndani na zile za kimataifa zimekua zikiripoti na kutamka wazi wazi kwamba chaguzi hizo hazikuwa huru na haki na kuna haja ya kuitishwa uchaguzi mwengine mpya, lakini ushauri huo ulibakia kwa taasisi hizo zenyewe, kwani CCM – ambayo ndiyo mtendaji wa uharibifu huo na pia mfaidika wake – huwa inatangazwa mshindi katika kila uchaguzi.

Mfumo wa utawala wa CCM umekuwa ukiwanyima wananchi wa Zanzibar uhuru wa kudai haki zao za kikatiba na kidemokrasia, hasa pale ambapo wamedhulumiwa, viongozi wamebaki kuwa juu ya sheria na hata pale wananchi wanapodhulumiwa haki zao, Serikali hubaki kimya bila ya uetezi wowote kwa wananchi.

Kwa mara ya kwanza tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya 1964, Zanzibar ilishuhudia mauaji ya kutisha ya tarehe 26 na 27 mwaka 2001 ambayo kimsingi yalitokea mara baada ya wananchi wa Unguja na Pemba kufanya maandamano ya amani kwa lengo la kupinga matokeo ya Uchaguzi wa 2000 yaliyomueka madarakani Rais Amani Abeid Karume.

Maandamano hayo ambayo yalilenga kudai haki ya wapiga kura kwa upande mmoja na kuuthibitishia ulimwengu kuwa haki haikutendeka kwenye uchaguzi mkuu kwa upande mwengine, hayakuzaa matunda mengi na badala yake yalisalia kuwafanya watu wapoteze maisha yao na kuacha vizuka na mayatima majumbani kwwani Serikali ya CCM iliwaamuru jeshi la Polisi pamoja na vikosi vya SMZ kuwamiminia risasi waandamanaji kadiri walivyoweza.

Kuandamana huko hakukuwa ni jambo la ajabu kuwahi kufanywa na Wazanzibari kwani hata katika nchi nyengine duniani ambazo hufuata mfumo wa demokrasia na siasa ya vyama vingi, hutumia njia hii katika kudai haki yao ya kikatiba na kidemokrasia hasa pale wanapoona watawala wanaipora haki hiyo, na katika nchi zinazojali na kuthamini demokrasia, huwasikiliza wananchi hao wanataka nini na hivyo hufikia makubaliano. Lakini kwa upande wa Serikali ya CCM hali hiyo ilikuwa kinyume chake kwani waliwavamia wananchi kwa mitutu ya bunduki na kuwamiminia mvua ya risasi hali iliyipelekea watu wengi kupoteza maisha na kwa mara ya kwanza Tanzania hususan Zanzibar ilijitia aibu kwa kutoa wakimbizi waliokwenda nchi jirani kutafuta hifadhi.

Vyombo vya habari ambavyo huripoti kinyume na matakwa ya watawala hufungiwa na hata waandishi wa habari hupigwa na kuteswa ambapo wengine hutishiwa kuuliwa. Katika siku za hivi karibuni makundi ya vijana wa Janjaweed na Mazombi wanaokisiwa kuwa ni zaidi ya watu 20, wakiwa wamejifunika nyuso zao, kwa nyakati tofauti walivivamia vituo viwili vya redio ya Coconut FM na Hits FM na kuwapiga waandishi waliokuwemo vituoni humo na wengine kutishiwa uhai wao huku kituo cha redio cha Hits FM kikichomwa moto hali ambayo ilisababisha hasara kubwa kwa mmiliki wa kituo hicho na wafanyakazi.

Mbali na matukio hayo, matukio mengine yaliyofanywa na vijana hao ni pale kundi hilo la vijana walipovamia eneo la Mwanakwerekwe na kupiga watu wasio na hatia. Katika tukio hilo, Bwana Ali Salum wa mtaa wa Nyerere alikamatwa na vijana hao huku akiwekwa chini ya ulinzi na kupigwa kupita kiasi hali ambayo ilimfanya apate maumivu makali na kupelekea kufikishwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Licha ya matokeo hayo maovu na yenye ukiukwaji mkubwa wa demokrasia na haki za binaadamu, ikiwemo haki na uhuru wa wananchi kuripotiwa na vyombo vingi vya habari vya ndani na vile vya kimataifa, hakuna juhudi zozote zilizochukuliwa na serikali ya CCM katika kukemea na kuwakamata wale wote waliohusika na uovu huo.

Pamoja na yote hayo, bado wananchi wa Zanzibar wanaendelea kukosa uhuru na haki yao ya msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka. Pamoja na viongozi mbali mbali visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupanda majukwaani na kuhubiri demokrasia na utawala wa sheria, hatua hiyo imebaki kuwa ya kinafiki na yenye kuwadharau wananchi wake.

Tarehe 25 Oktoba 2015, wananchi wa Zanzibar walipiga kura kuchagua viongozi wa ngazi mbali mbali watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Katika uchaguzi huo wananchi walifanya maamuzi yao kwa kumchagua Maalim Seif Sharif Hamad ili awaongoze kwenye nafasi ya urais. Lakini kwa kusimamia sera yake ya kutokukubali haki ya wananchi kujiamulia, CCM ilimtumilia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha, kuufuta uchaguzi huo kwa kisingizio cha kuwepo kwa hitilafu nyingi.

Hatua hiyo imepelekea hali ngumu ya maisha kwa wananchi walio wengi huku wachache wakiendelea kufaidika wao na familia zao.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.