Mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu ambapo tarehe 25 Oktoba, wananchi wa Zanzibar walishiriki katika kuwachagua Viongozi kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uchaguzi Mkuu ulitanguliwa na kampeni za vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo na wananchi walishiriki kwa wingi katika kampeni zake.

Uchaguzi wa Viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliosimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umemalizika na Chama cha Mapinduzi kimepata ushindi mkubwa. Nampongeza Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais. Kwa upande wa Zanzibar Tume ya Uchaguzi uliufuta uchaguzi huu hapo tarehe 28 Oktoba, 2015, baada ya kubainika kutokea kwa kasoro kadhaa kama zilivyoelezwa na Tume hiyo.

Aidha, uamuzi huo wa Tume ulitangazwa katika Gazeti Rasmi la Serikali la tarehe 6 Novemba, 2015 kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeyafuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kwamba uamuzi wa Tume wa tarehe nyengine ya kurudiwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utatangazwa baadae.

Aidha, katika suala zima la hali ya kisiasa ya Zanzibar, iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu, viongozi wenu tulishauriana tukutane ili tufanye mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa njia ya amani, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano. Hatimaye tulikubaliana tuanze mazungumzo hayo.

Mazungumzo haya yanatuhusisha viongozi sita. Viongozi hao ni mimi nikiwa Mwenyekiti, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wakiwa wajumbe. Wajumbe wengine ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Tano Dk. Salmin Amour Juma na Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karume. Mazungumzo hayo yamefikia hatua kubwa na bado yanaendelea. Taarifa kamili ya mazungumzo hayo itatolewa mara tu yatakapokamilika.

Namaliza risala yangu, kwa kukukumbusheni kwamba kesho tarehe 1 Januari ni siku yetu ya kujitokeza sote kufanya mazoezi. Tujitokezeni kwa wingi. Nakutakieni kheri ya mwaka mpya viongozi wote, wananchi, nchi marafiki, washirika wetu wa maendeleo pamoja na mashirika ya Kimataifa kupitia mabalozi na wawakilishi waliopo nchini.

Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kheri, baraka na neema nyingi katika mwaka mpya wa 2016. Atuzidishie amani, umoja na masikilizano. Atujaalie uwezo zaidi wa kuitekeleza mipango yetu kwa ufanisi ili kuimarisha uchumi na ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.

*Sehemu ya hotuba ya Dk. Ali Mohammed Shein kuuaga mwaka 2015 akiukaribisha mwaka 2016

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.