Tokea Chama cha Mapinduzi (CCM) kupata kipigo cha kihistoria katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 ambapo kilizidiwa na Chama cha Wananchi (CUF) kwa kura 25,831 kimekuwa kikiweweseka kwa madai ya kwamba kimeibiwa kura kisiwani Pemba na hivyo kutoa mashindikizo kwamba matokeo ya uchaguzi huo yafutwe.

Sisi CUF tulikuwa tukiwaeleza ukweli tokea wakati wa kampeni kwamba kuzidiwa kwa CCM katika oganaizesheni na mikakati ya kuendesha kampeni za kisasa kunatokana na timu mbovu ya viongozi wao wa Chama na Kamati yao ya Kampeni. Mara zote walikuwa wakikasirika sana kila tulipowaeleza hili na baada ya matokeo ya uchaguzi kuwaendea vibaya wakaja na nyimbo ya kudai wamehujumiwa na kuibiwa kura.

Na Ismail Jussa
Na Ismail Jussa

Wahenga walisema “kweli ikidhihiri uongo hujitenga.” Juzi kupitia kikao chao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar, wajumbe walieleza waziwazi kwamba kushindwa vibaya kwa chama chao kumesababishwa na ukweli kwamba Kamati Tendaji (Sekretarieti) iliyopo haina uwezo wa kisiasa na kwamba imeshindwa kusimamia malengo ya kuimarisha uhai wa chama na kupelekea kudhoofika kwa oganaizesheni ya chama hicho visiwani Zanzibar.

Kutokana na ukweli huo, kikao kimewateua wajumbe wengine wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwa wasaidizi kwenye Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu na Idara zote za chama. Walioteuliwa ni:

1. Dk. Khalid Salum Mohamed (Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu);
2. Hamad Omar Bakari (Idara ya Oganaizesheni);
3. Moudline Castico (Idara ya Itikadi na Uenezi);
4. Ali Karume (Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa); na
5. Maalim Kombo (Idara ya Uchumi na Fedha).

Ukweli wa mambo ni kwamba maamuzi hayo ambayo hayakutangazwa yalikuwa ni kuthibitisha kwamba wajumbe wa Kamati Maalum ya CCM wanajua kwamba kilichowafanya washindwe kwenye uchaguzi si hujuma wala wizi wa kura bali waliyosababisha washindwe vibaya ni viongozi dhaifu wasio na uwezo wa Sekretarieti iliyokuwepo ambao ni Vuai Ali Vuai, Waride Bakari Jabu, Hamad Yusuf Masauni, Haji Mkema Haji na Seif Shaaban Muhando.

Taarifa za ndani zinaeleza kwamba hao walioitwa wasaidizi ndiyo wanaoandaliwa kuchukua nafasi baada ya kupata idhini ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho lakini katika hali ya sasa ya kisiasa na mfadhaiko uliosababishwa na makundi na mgawanyiko mkubwa imeonekana kwanza waliopo wapoozwe mpaka wakati muafaka ukifika.

Nimeyaandika haya ili kuwataka CCM Zanzibar waache unafiki na waache kujitetea mbele ya wanachama wao kwa kuwaambia uongo kwamba CUF iliwashinda kutokana na hujuma na wizi wa kura. Badala yake ukweli huu walioukiri kwenye vikao waueleze hadharani na hatimaye waheshimu maamuzi ya wananchi wa Zanzibar huku wakisubiri uchaguzi mwengine wa 2020 na wajaribu tena bahati yao.

Nilikwambieni na nakwambieni tena CCM hamna manusura.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.