Moja ya mafanikio makubwa ya Rais Kikwete ni kuimarisha uhusiano wa Tanzania na mataifa makubwa hususan Marekani na China. Rais Kikwete alifanikisha Tanzania kupata msaada mkubwa wa Millennium Challenge Corporation – MCC wa dola milioni 698 kutoka serikali ya Marekani uliogharamia miradi mingi ya sekta ya usafiri, nishati na maji katika kipindi cha miaka 5 kati ya 2008 – 2013.

Naunga mkono azma ya Rais Magufuli ya kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa nchi yetu kuwa tegemezi wa misaada ya nje. Pamoja na lengo hilo ni muhimu kuyalinda na kuyatumia kwa manufaa ya taifa matunda ya diplomasia ya JK.

Na Prof. Ibrahim Lipumba
Na Prof. Ibrahim Lipumba

Serikali ya awamu ya nne ilifanikisha maandalizi ya kupata msaada wa pili wa dola milioni 472.8 ambao utajikita katika kuimarisha sekta ya nishati ili kuhakikisha kupatikana kwa umeme wa uhakika. Uamuzi wa kuweka kipaumbele sekta ya nishati ulitokana na utafiti wa vikwazo vya uchumi uliobainisha kuwa ukosefu wa umeme wa uhakika ni kikwazo kikubwa kinachozuia ukuaji wa uchumi.

Msaada huu wa pili unaojumuisha dola milioni 58.6 zitakazotumiwa kuimarizha ZECO na sekta ya umeme Zanzibar uko hatarini kusambaratika ikiwa maamuzi ya wananchi wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 2015 hayataheshimiwa.

Serikali imeandaa mpango kabambe wa kurekebisha sekta ya umeme – Electricity Supply Industry Reform Strategy and Roadmap. Mpango wa pili wa MCC umejielekeza kusaidia kutekeleza mpango huu wa serikali. Utekelezaji wa mpango huu pia unalenga kuunganisha wateja wapya 300,000 wapate umeme wa uhakika. Msaada huu pia unatarajia kurekebisha sekta ya umeme ya Zanzibar na kuanzisha ufuaji wa umeme wa MW 5 kutumia jua au upepo.

Tarehe 17 Septemba 2015, Bodi ya MCC ilikutana katika kikao chake cha kila robo mwaka na ikatoa taarifa ya mjadala wake wa msaada wa pili kwa Tanzania wa dola milioni 472.8. Bodi iliunga mkono msaada huo kwani una lengo la kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika Tanzania. Msaada huu utaimarisha utendaji wa asasi zinazosimamia ufuaji na ugawaji wa umeme – TANESCO kwa upande wa Tanzania Bara na ZECO kwa upande wa Zanzibar.

Hata hivyo Bodi ya MCC ilikuwa na wasiwasi kuhusu rushwa na ufisadi nchini Tanzania. Ilisisitiza kwamba Tanzania lazima ifaulu kigezo cha kupambana na rushwa kabla ya kuamua kupitisha msaada huo. Bodi pia ilieleza kuwa ina matumaini ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa tarehe 25 Oktoba 2015 utakuwa huru na haki kwa kuwa MCC inaamini haki za kidemokrasia ni sehemu muhimu ya utawala bora.

Tarehe 26 Septemba MCC ilitoa tamko kuwa kufuatana na taarifa za kigezo cha kupambana na rushwa kinachotolewa na Benki ya Dunia katika chapisho lao la Worldwide Governance Indicators, Tanzania imefaulu kigezo hiki. Kwa hiyo Tanzania imefaulu vigezo vyote vya kitakwimu vinavyotumiwa na Bodi katika maamuzi yake. Tamko la MCC liliendelea kusisitiza matumaini yake kuwa uchaguzi wa tarehe 15 Oktoba 2015 utakuwa huru na wa haki.

Pamoja na mapungufu ya uchaguzi mkuu, Watazamaji wengi wa ndani na nje waliutathmini mchakato mzima wa uchaguzi kwa ujumla wake na kuridhishwa kwamba ulikuwa huru na wa haki, Tanzania Bara na Zanzibar. Watazamaji hawa walistushwa na kustajabishwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar. Ikumbukwe Zanzibar wamefanya uchaguzi wa Rais wa Muungano, Wabunge, Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani. Uchaguzi huu umetumia Daftari la Wapigakura la ZEC na vituo vya kupigia kura vilivyoandaliwa na ZEC. Itakuwaje matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Muungano na Wabunge ukubaliwe, lakini Uchaguzi wa Zanzibar ufutwe?

Tarehe 16 Disemba, Bodi ya MCC ilikutana na ikamua kutopitisha msaada wa pili kwa Tanzania. Hoja kubwa iliyoifanya Bodi isipitishe msaada wa dola milioni 472.8 ni kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar baada ya kufanyika uchaguzi mzuri na wa amani. Hoja ya pili ni matumizi mabaya ya sheria ya Makosa ya Jinai ya Mtandao wakati wa uchaguzi mkuu ambapo kuna baadhi ya watazamaji waliosajiliwa na Tume ya Uchaguzi walikamatwa na polisi kwa kutumia sheria hii.

Ni wazi kabisa kama matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar hayataheshimiwa, msaada wa pili wa MCC utafutwa.

Ikiwa msaada wa pili wa MCC utafutwa utaathiri utekelezaji wa mpango wa serikali wa kurekebisha sekta ya umeme na pia kuhujumu mpango wa Rais Obama wa Power Africa kwa upande wa Tanzania. Ziara ya Rais Obama nchini Tanzania iliambatana na uzinduzi wa Power Africa mpango wa Marekani kusaidia nchi za kiafrika kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 6 za mwanzo kufaidika na mpango huu. Marekebisho ya sekta ya umeme yatakayofadhiliwa na MCC yalitarajiwa kuwa motisha kwa wawekezaji wa sekta binafsi. Kwa mfano kampuni ya Symbion ambayo ilitekeleza baadhi ya miradi ya msaada wa kwanza wa MCC, ina mpango wa kuwekeza ufuaji wa umeme wa MW 600, mjini Mtwara na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa kupitia Songea. Mradi huu utagharimu zaidi ya dola bilioni 1. Ikiwa msaada wa MCC utafutwa mradi huu utakuwa mashakani kutekelezwa.

Ilani ya uchaguzi ya CCM inalenga kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa karibu mara tatu, kutoka MW 1308 za sasa mpaka kufikia MW 4915 mwaka 2020. Kuunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa na kuhakikisha asilimia 60 za kaya zote zinatumia umeme. Haya ni malengo makubwa sana yaliyojikita katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa serikali wa sekta ya umeme utakaosaidiwa na msaada wa MCC.

Kutoyakubali matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kutaathiri mahusiano yetu na nchi nyingine hasa za Jumuiya ya Ulaya. Hata Jamhuri ya Watu wa China inataka nchi yetu iwe na amani na utulivu wa kisiasa. Suala la Zanzibar la kuheshimu matokeo ya uchaguzi siyo la kusalimu amri ya Mataifa mengine bali la kuheshimu uamuzi wa Wazanzibari waliofanya kwenye uchaguzi ambao kwa ujumla wake ulihesabiwa kuwa ni huru na wa haki

Dk. Ali Mohamed Shein, rais aliyechaguliwa katika uchaguzi wa 2010 ana ufunguo wa tatizo hili. Akubali matokeo ya uchaguzi wa 2015 ya Zanzibar yakamilishwe na kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Ajiulize suala la msingi anataka kuleta vurugu za kisiasa Zanzibar? Anataka kuwapa fursa watu wenye siasa kali inayopinga demokrasia kuhamasisha vijana wa Zanzibar? Anataka kuharibu matunda ya diplomasia ya JK aliyoshiriki kuyaleta kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaania? Anataka kuvuruga uhusiano wa Tanzania na Marekani na mataifa mengine? Anataka kumuhujumu Rais Obama asifanikishe Mpango wake wa Power Afrika kabla hajan’gatuka mwaka 2016? Anataka kumuharibia Rais Magufuli asitekeleze sera zake za kupambana na rushwa na kujenga uchumi wa viwanda unaoongeza ajira na kutokomeza umasikini bali ashughulikie matatizo ya kisiasa na kiusalama ya Zanzibar na kushutumiwa kuwa anavunja haki za binadamu za Wazanzibari? Anataka Watanzania wa Bara tufanye maandamano ya kumshutumu kuwa anatuvurugia nchi na kuhujumu utekelezaji wa sera za Rais Magufuli?

Pamoja na mapungufu yetu, Tanzania inatazamwa kuwa nchi ya mfano kwa amani na utulivu na ujenzi wa demokrasia katika eneo letu la Afrika ya Mashariki na nchi za Maziwa Makuu. Tunategemewa kusaidia kusuluhisha migogoro ya nchi za jirani. Rais Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje, Dr Mahiga watawezaje kusuluhisha migogoro ya nchi za jirani ikiwa Zanzibar italipuka kwa sababu ya Dr Shein kukataa matokeo ya uchaguzi?

Hatari kubwa zaidi kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni vijana kuamini kuwa hatuwezi kuleta mabadiliko kwa njia za kidemokrasia. Watu wenye itikadi kali zisizoamini mfumo wa demokrasia watapata mwanya wa kuendeleza itikadi hizo na kupata wafuasi hasa vijana. Dr Shein jiulize unataka kutupeleka huko?

Tuwashukuru na kuwapongeza Wazanzibari kwa kuendelea kuwa watulivu na kuwa na matumaini ya kupatikana ufumbuzi wa haki. Lakini tuelewe uvumilivu wa Wazanzibari una kikomo. Kutangaza rasmi kurudia uchaguzi kunaweza kuwa chanzo cha vurugu za kisiasa zinazoweza kuleta maafa makubwa. Nani atakayesimamia uchaguzi huo ikiwa taarifa ya Mwenyekiti wa ZEC kuwa wajumbe wake wanadundana itakubaliwa kuwa ni ya kweli? Kama Tume na Sekretariati yake imeharibu uchaguzi wa Oktoba 2015 watawezaje kusimamia uchaguzi mwingine? Kama uchaguzi wa Zanzibar umeharibika kwa nini uchaguzi wa Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Zanzibar uhesabiwe kuwa ni halali wakati ulifanyika siku moja kwa kutumia daftari la ZEC na vituo vya kupigia kura vilivyoandaliwa na ZEC? Uchaguzi wa Zanzibar umekamilika. Matokeo yapo. Mchakato wake ukamilishwe na yatangazwe.

Watanzania hasa viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali, viongozi wa asasi za kiraia, viongozi wastaafu, vyombo vya habari na wapenda haki tusilifumbie macho tatizo la kisiasa la Zanzibar. Tumshauri Dr Shein akubali mchakato wa kutangaza matokeo ukamilishwe. Ni aibu kuulizwa na Marekani kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa shwari na wa amani kwanini matokeo yake yamefutwa? Kama CCM aiheshimu maamuzi ya Wapiga kura wa Zanzibar itaheshimu maamuzi ya Watanzania wote ikiwa itashindwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.