Mnamo tarehe 10 Juni 2015, niliandika makala iitwayo “CCM Zanzibar haina uhalali kujinasibisha na mapinduzi” nikionesha jinsi mwakilishi wa zamani wa jimbo la Mwanakwerekwe, Waziri Kiongozi Mstaafu, waziri wa zamani wa mambo ya ndani na pia ya ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha, alivyotumia moja ya mikutano yake ya hadhara kwenye jimbo hilo kuwakumbusha wana-CCM wenziwe mambo ambayo endapo wakiyapuuzia, basi itatokezea siku Wazanzibari watawakosesha uhalali wa kuongoza nchi, kwa maana nyengine wananchi wangekuja kukichagua chama ambacho kimebeba matumaini ya kupatiwa ufumbuzi yale mambo ambayo Nahodha aliyatanabahisha.

Kwa kifupi, katika mkutano huo, Nahodha aliwaambia wenzake kuwa Wazanzibari si wasahaulifu na wana mambo ambayo kwao ni muhimu zaidi kwenye maisha ya siku kwa siku, ambayo yamesahauliwa kabisa na uongozi wa juu wa nchi, tafauti na wakati wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Karume.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

“Nawaomba viongozi wa CCM na wanachama na wapenda amani tujiulize masuala yafuatayo: la kwanza, Mzee Karume aligawa ardhi heka tatu tatu kwa wanyonge ili wajiendeleze kwa kilimo. Mimi nauliza kweupe, je ardhi hizi zipo na kama hazipo zimekwenda wapi? La pili, Mzee Karume alifanya elimu bure mwaka 1972. Mimi nauliza leo elimu ni bure kama alivyoacha Marehemu Mzee Karume? Kama hapana, mimi na nyinyi tujiulizeni kwa nini imekuwa hivyo? La tatu, afya bora. Je, kwa sasa afya ni bora kama alivyoziacha Hayati Mzee Karume? Kama hapana, kwa nini? Haya ndio masuala ya watu wenye hekima na busara, wanachama na viongozi wa CCM wayapatie majibu. Tusipotoa majibu, siku moja tutapoteza uhalali wa kuongoza.” Alionya Nahodha kwenye mkutano huo, ambao kama ungelikuwa umefanyika leo penye msamiati mpya wa “umagufulishaji”, tungelisema “Nahodha alimagufulika kwa kupasua jipu”.

Alichokisema Nahodha kilikuwa kweli miezi sita iliyopita kama kilivyo kweli leo hii. Ndio maana, hadi hivi leo kila pakitokezea jambo ambalo linawakera sana, utawasikia Wazanzibari wakijiuliza: “ingekuwaje kama mwenyewe Mzee Karume angelikuwepo?”

Nahodha aliwapa wenzake changamoto ya kusaka majibu kwa wananchi, majibu ambayo yalishasubiriwa dahari nyingi baada ya kuuwawa kwa Mzee Karume. Pakuwa na majibu hadi wananchi wanakwenda kwenye visanduku vya kura tarehe 25 Oktoba 2015. Wazanzibari si wasahaulifu kama wanavyosahau viongozi wa CCM. Kiukweli, Wazanzibari wanamkumbuka Mzee Karume kila uchao kuliko viongozi hao wa CCM wanaojinasibisha eti kuwa ni wao pekee ndio warithi halali na wa pekee wa Mapinduzi ya 1964.

Kama nilivyotanguliwa kusema, kila mara Wazanzibari huhoji: “ingelikuwaje kama Mzee Karume hakuuwawa? Je, haya yanayotendeka na CCM yangelitendeka?” Wanaamini jawabu lake ni hapana, kwani katika miaka yake michache aliyodumu na kuhudumu kama Rais wa Zanzibar, aliwafanyia mengi mazuri wananchi wake bila ubaguzi kama ilivyo sasa.

Kwa kifupi ni kuwa hakuna haja ya kusakana uchawi kwa kilichotokea tarehe 25 Oktoba. Hakuna mzembe katika utendaji wa CCM. Hakuna msaliti wa chama. Hakuna wizi wa kura uliofanywa na Chama cha Wananchi (CUF). Kilichotokezea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 visiwani Zanzibar ni ule utabiri wa Nahodha.

Jipu alilolitumbua miezi minne kabla ya uchaguzi halikutoka usaha wala moyo wake. Liliwauma wenye nalo lakini wakabakia nalo. Licha ya kujiamsha yeye na kuwaamsha vingozi wenzake wa CCM na wafuasi wake, bado usingizi wao ulikuwa mzito mno na ukawapa takaburi za kujiona wao ndio wamiliki pekee wa Zanzibar hata kama wataikanyagakanyaga na kuipondaponda misingi halisi ya Mapinduzi na kuyatupilia mbali malengo yake.

Wazanzibari hawakusahau. Kwa dharau hizo na takaburi za CCM, Wazanzibari wakaamua bila ya kujali uzawa wao, bila kujali wametoka umbali gani na chama hicho kikongwe, kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa maalum. Waliupa jina la “Mwaka wa Maamuzi” na kwa kweli wakaamua uamuzi ambao umeibomoa CCM vibaya mno mjini na vijiji nina kuwaacha viongozi wake wakimtafuta mchawi na msaliti wa chama chao.

Hasira za viongozi wa CCM zikaangukia kwenye kumtaka Jecha Salim Jecha aufute uchaguzi wote. Masikini wanasahau haraka kwa sababu wao ni wasahaulifu wakubwa, akiwemo hata huyo mtoa tahadhari mwenyewe – Shamsi Vuai Nahodha. Ghafla wamesahau kuwa ni wananchi ndio walioikosesha CCM uhalali wa kuiongoza Zanzibar na sasa wanashinikiza eti uchaguzi mwengine. Azma yao ni kuwa watajipanga upya kuiba kura na kutisha wananchi ili wasiende vituoni kwa kuyatumia makundi yao ya mazombi na masoksi.

Masikini, CCM. Waliowakataeni ni Wazanzibari. Hata mukiitisha uchaguzi kila baada ya miezi mitatu, bado mutaendelea kukataliwa kwa sababu ya usaliti wenu dhidi ya malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar, dhidi ya uhuru kamili wa Mzanzibari.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.