Dkt. Ali Mohamed Sheni ndie Makamo mwenyekiti wa CCM, ambapo kwa upande wa Zanzibar yeye ndiye mtendaji mkuu kupitia chama hicho kikongwe ambacho katika uchaguzi wa 25 Oktoba 2015 kilonekana kilipitwa kwa tofauti ya kura zaidi ya 20,000 na chama cha wananchi (CUF), mbali ya wadhifa huo kichama pia ndiye aliyekuwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Serekali iliyomalizika muda wake kikatiba, ambayo ilianza 03/11/2010 hadi 02/11/2015.

Licha ya kuwa na nyadhifa zote hizo kwa wakati mmoja ambapo akitoa tamko lake basi huwa linapewa uzito wa hali ya juu kichama, halikadhalika, iwapo akitamka kabla ya muhula wake wa urais kumalizika basi hio huwa ni sheria na wananchi hawana budi kutii agizo hilo.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Wapo wanaolazimisha kusema kwamba Dkt. Ali Mohamed Sheni yupo kihalali, licha ya katiba ya Zanzibar kutamka bayana katika kifungu cha 28(2) cha katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, ingawa kifungu hichi kinapigwa chenga na wahafidhina wa CCM Zanzibar na wanasheria wao na kuzingatia zaidi kifungu cha 28(1), ambapo uwepo wa kifungu na nambari 28(2) kisheria 28(1)huwa kimezidiwa nguvu kwa kuwa 28(2) kinaendelea kutolea ufafanuzi wa kifungu cha 28(1).

Lakini niseme hawakipuuzi kifungu hicho kwa kutokujua, la hasha, wanafanya hivyo kwa makusudi ili kuendeleza mradi wao wa kusalia madarakani kinyume na sheria, ambapo athari za kutawala kinyume na katiba tayari zimeanza kuonekana, idadi ya wageni/ watalii imeanza kupungua kuja Zanzibar baada ya watalii hao kupewa maonyo katika nchi zao kwa kuelezwa kwamba “If you go to Zanzibar, just go by your own risk because there is no legal government” wakimaanishiwa kwamba Zanzibar hakuna serikali inayotawala kisheria chochote kitakachowatokea wakiwa Zanzibar ni juu yao wenyewe.

Hivyo tumewasikia mara kadhaa watu walio chini ya Dkt. Sheni kichama na Serikali iliyomaliza muda wake wakihubiri uchaguzi wa marudio utadhani jambo hilo halina mamlaka yake maalum ambayo ni tume ya Uchaguzi ya Zanzibar -ZEC, licha ya kuepo chombo hicho chenye mamlaka ya kuendesha shughuli za kuichaguzi katika nchi kutokuwa na maandalizi yeyote ya uchaguzi kama walivyoeleza watendaji wa Tume hio ya ZEC kupitia Mkurugenzi wake na Msemaji wa Tume hio wiki chache zilizopita, lakini hata Dkt. Sheni na yeye kwa upande wake, hana taarifa ya kurudiwa kwa uchaguzi baada ya ule wa 25 Oktoba 2015 kusitishwa matokeo yake na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ZEC Ndugu Jecha Salim Jecha, ambapo alitokeza kwenye luninga ya taifa ya ZBC kutoka mahala pasipojulikana na kudai ati amefuta uchaguzi wote ambapo kufanya hivyo ni kinyume na sheria.

Nasema Dkt. Sheni hajawahipo kuzungumzia habari ya uchaguzi wa Marudio nikiwa nauhakika wa hilo, kwa kuwa Dkt. Sheni  ameonekana mara kadhaa akizungumza katika televisheni ya ZBC lakini hakuna siku amezungumzia kwamba uchaguzi utarudiwa mbali ya uwepo wa mazungumzo yanayoendelea Ikulu ya Zanzibar, ambayo kimwonekano yanatafuta uhalali wa Jecha kufuta Uchaguzi wote.

Kutokana na wafuasi wa CCM wa chini kutoa kauli na habari ambazo zina lengo la kupotosha umma wa wazanzibari na ulimwengu kwa ujumla  ndio mana tarehe 26/12/2015 , ambapo kwa waumini wa dini ya kikristo siku hii ni siku Maalum kwa kugaiana na kupeana Zawadi ya Chrismass, ndipo Dkt. Sheni akaamua kukata mzizi wa fitna kwa hao wanajaribu kuuhubiria umma visivyo ndivyo, akiwa mbele ya Dkt. Magufuli, Dkt. Sheni hakuzungumzia habari ya marejeo ya Uchaguzi hata kwa bahati mbaya, alichokizungumza ni kuwaambia na kumwambia Dkt magufuli kwamba kuna mazungumzo yanayoendelea, na maendeleo ya Mazungumzo ni mazuri muda mfupi ujao mazungumzo yatamalizika.

Ambapo kila Mpenda haki, amani na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania akiwemo Rais Magufuli anajua kumalizika kwa mazungumzo yanayoendelea ikulu ya Zanzibar chini ya Dkt .Sheni ni kumpatia haki yake aleyeshinda uchaguzi wa 25 Oktoba 2015 na si vyenginevyo kama wanavyopotosha watu waliochini ya Dkt. Shein.

Hatua hiyo ya kuwapatia haki walioshinda katika uchaguzi huo itaiwezesha Zanzibar abakie salama na amani na kuanza upya harakati za kuleta maendeleo ya kweli na kuondoa ugumu wa maisha, pia itamuezesha Dkt. Magufuli  kuendelea na kasi yake ya utendaji aliyoanzanayo vizuri na kwa ufanisi zaidi, kwani shirika la MCC la Marekani limeshamuahidi Raisi Magufuli, pindipo akimalizia kutoa matokeo ya Uchaguzi yaliyositishwa Zanzibar kupitia uchaguzi wa 25 Oktoba 2015 basi atapatiwa shilingi trilioni moja ya Tanzania ili aweze kutatua changamoto zinazoikali nchi yetu, na Dkt. Magufuli ameahidi kufanya hivyo mara kadhaa na hata juzi akiwa katika ibada ya Xmass mbele ya waumini na maaskofu wa kanisa LA mtakatifu Peter jijini Dar es Salam, Dkt. Magufuli aliiahidi hadhara iliokuwa hapo, kwamba hayuko tayari kuiona Tanzania inakosa misaada na yeye kuzuiliwa safari za nje ya nchi eti kwa kwa mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar.

Naamini katika masomo ya menejimenti ambapo siku zote yanaeleza kwamba amri hazitoki chini zikapanda juu, bali hutoka juu zikashuka chini na kufanyiwa utekelezaji, na sio kutoka chini kwenda juu kumuamrisha mkubwa azifanyie Kazi.

Napenda niwape nasaha  wana CCM, muachwe kuburuzwa, mkubaliane na waliyozungumza viongozi wenu siku ya tarehe 26/12/2015 huko Ikulu Dar es salaam kwamba kuna kamati  imeundwa ambayo ni ya watu sita, ambapo washiriki wake ni yeye Dkt. Ali Mohamed Shein, Maalim Seif Sharif Hamad, Dkt. Amani Abeid Amani Karume, Dkt. Salmini Amour Juma, Ndugu Ali Hassan Mwinyi na Balozi Seif Ali Idd, na kwa kauli ya Dkt. Shein wakisha kukamilisha makubaliano yao watatoa tamko la pamoja.

Chakufurahisha na kusikitisha, awali kabla ya mazungumzo baina ya Maalim Seif Sharif Hamad na Dkt. John Pombe Magufuli wiki moja iliyopita na kile kilichofanyika tarehe 26/12/2015 IKulu ya Dar es Salam baina ya Dkt. Magufuli ambaye ni Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamo mwenyekiti CCM Dkt. Ali Mohd Shein, viongozi hao waliochini ya Dkt. Shein walitoka hadharani na kudai kwamba hawayatambui mazungumzo yanayoendelea, lakini kwa cha kushukuriwa hapa ni kwamba tayari viongozi wao wameshatanabahishwa kwamba wao si lolote si chochote mbele ya Tanzania na Watanzania, Zanzibar na Wazanzibari, Dkt. Magufuli, Dkt. Shein Maalim Seif Sharif Hamadi na kamati ambayo ameundwa na wajumbe sita.

Hivyo ni kusema muamuzi juu ya mkwamo wa kisiasa na kikatiba uliotekea baada ya Ndugu Jecha Salim Jecha kudai amefuta uchaguzi huru na haki wa tarehe 25/10/2015, hautoamuliwa na matamko kutoka Makao Makuu ya CCM Zanzibar (Kisiwandui), bali ni kamati Maalum yenye wajumbe sita niliowataja hapo awali, kamati ambayo kuanzia tarehe 27/12/2015, CCM Tanganyika na Zanzibar wameitambua rasmi kwa kuitolea tamko lilitamkwa na Bi Waride Bakari Jabu ambaye ndiye msemaji wa chama kwa upande wa Zanzibar kwa sasa, pamoja na kwamba tamko lake pia amegusia kuwaambia wana – CCM wajitayarishe na uchaguzi wa marudio,  lakini niseme kinachotakiwa sasa na tangu hapo awali kuhusu mustakabali wa Uchaguzi wa tarehe 25/10/2015 ni kusubiri maamuzi ya kamati na sio matamko ya waliochini ya Dkt. Ali Mohamed Shein.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.