Kuna kitu kinapotoshwa kama si kwa bahati mbaya basi ni kwa kukusudia, Kamati Maalum ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, imekutana kujadili hali ya kisiasa Zanzibar, taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Bi. Waride Bakar, ni kuwa, kikao hicho kimeunga mkono mazungumzo yanayoendelea Ikulu ya Zanzibar, kuhusu mwafaka wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Aidha Waride amewataka wana-CCM kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwa vile uchaguzi uliofanyika ulikuwa na dosari kubwa….niishie hapo kwa Bi. Waride.

Na Ally Mohammed
Na Ally Mohammed

Baada ya taarifa hiyo mitandao ya kijamii imetawaliwa na taarifa eti imekubalika kuwa Uchaguzi wa Zanzibar urejewe na tarehe ya marejeo itatangazwa baadae na Tume ya Uchaguzi, ni hivi, kikao cha Kamati Maalum ya Chama Cha Mapinduzi kilichokutana leo (jana) kwanza hakina maamuzi ya kuamua kuhusu uchaguzi, pili maamuzi yake hayana uhusiano hata chembe na mazungumzo yanayoendelea Ikulu ya Zanzibar yanahusisha wajumbe sita tulioambiwa, tatu maamuzi yao hayana athari yeyote kuhusu mazungumzo yanayoendelea.

Inawezekana sijaeleweka, ngoja nitoe mfano ulio hai, Baraza Kuu la Uongozi CUF – Taifa, lililokutana Zanzibar kujadili mgogoro wa kisiasa na kutoka na maazimio, pamoja na mambo mengine, waliazimia (AZIMIO SIO PENDEKEZO), matokeo yaendelee kutangazwa na mshindi atangazwe na kisha aapishwe ili aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ni hivyo hivyo kwa kwa Kamati Maalum ya CCM walichokitolea taarifa leo kwa kuwataka wana-CCM wajiandae na uchaguzi wa marudio pale tarehe ya uchaguzi itakapotangazwa.

Mantiki ni kuwa, hiyo ndiyo misimamo ya vyama hivi, CCM wanataka itangazwe tarehe ya uchaguzi wa marudio na CUF wanataka matokeo yaendelee kutangazwa yalipoishia na mshindi atangazwe, sasa kipi cha ajabu hapa mpaka watu wanapotoshwa kuwa sasa imeamuliwa uchaguzi unarejewa? Tangu yalipoanza mazungumzo ya Ikulu mpaka naandika taarifa hii hakuna tamko lolote rasmi lililotangazwa kuhusu kurejea uchaguzi wala kuendelea na matokeo.

Jana (juzi), aliyekuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM ), Dkt. Ali Mohammed Shein, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar na wakati akitoka taarifa fupi ya mazungumzo hayo kwa waandishi wa habari, Dkt. Shein alisema mara baada ya mazungumzo hayo kukamilika itatolewa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari na wananchi watajuulishwa, kwa muptadha huo taarifa zozote zinazotolewa kwa sasa kuhusu uchaguzi ni taarifa za taasisi (vyama) tu lakini hazina NGUVU ZA KIMAMLAKA.

Narudia kusema hapa tusubiri kauli ya pamoja ya kilichozungumzwa na kukubaliwa katika mazungumzo yanayoendelea Ikulu ya Zanzibar na si vyenginevyo, kauli hizi za vyama vya siasa ni kutokana na misimamo yao juu ya hili lakini halihusu msimamo wa mazungumzo ya Ikulu, ambayo kimsingi ndiyo kiini na ufumbuzi wa huu mgogoro uliopo kwa sasa.

Hakuna haja ya kupata taharuki na matamko ya vyama, tuendelee kuwaombea wanaoendelea na mazungumzo wamalize salama na busara yenye muunganiko wa kujenga Umoja na mshikamano kwa lengo la kuwaweka Wazanzibari katika mustakabali ulio mwema wa maisha yao na kututoa hapa tulipo.

Nimalizie kwa kusema hayo matamko hayana na hayatokuwa na uhusiano wala athari yeyote na yanayoendelea Ikulu ya Zanzibar, watakachokubaliana ndiyo taarifa rasmi na itabakia katika utekelezaji tu!

Ally Mohammed pia anapatikana kwa barua-pepe ya allymohammed01@gmail.com

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.