Nimesoma kwa kiasi kikubwa maoni ya watu kupitia mitandao ya kijamii na makala ya baadhi ya magazeti kuhusu hatua ya kukutana na mazungumzo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, na aliyekuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi – CUF (UKAWA), Maalim Seif Shariff Hamad.

Kwa kiasi kikubwa maoni yanatofautiana, wapo waliopongeza na kuona kwa hatua hiyo basi ukurasa mpya wa siasa za Zanzibar umefunguliwa, lakini wapo waliobeza na kukashifu hatua hiyo huku wakipaza sauti ya maoni yao kuwa, hakuna jipya na hatua hiyo haiwezi kubadilisha chochote, kwa kile wanachoamini CCM ni ile ile na Magufuli ni yule yule.

Na Ally Mohammed
Na Ally Mohammed

Kwanza tukubaliane kimsingi hii ndiyo hulka ya binaadamu, kwamba hakuna jambo litafanyika duniani halafu sote tufanane mawazo, hakuna, hakuna, hakuna na mpaka kiama kitasimama hulka yetu itaendelea kuwa hivyo kwa sababu ndiyo asili tangu wakati wa Mitume (kwa wanaoamini), suala la kutofautiana mtazamo ni jambo la kawaida ingawa wakati mwengine unaweza kutofautiana na mwengine kwa kujenga hoja madhubuti zenye kueleweka.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 jumlisha na baadhi ya marekebisho yake, inampa madaraka makubwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuliona hilo Rais wa kwanza wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema kwa namna Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyo, basi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaweza kuwa DIKTETA kama akiamua kufanya hivyo, hii ni kutokana na madaraka makubwa aliyonayo kikatiba.

Nataka niseme kwa hali ya mgogoro wa kisiasa ilivyo visiwani Zanzibar, Rais Dkt. Magufuli anayo madaraka makubwa ya kuingilia kati na dakika kumi tu zinamtosha kufanya maamuzi kuhusu huu mgogoro, narudia dakika kumi tu Magufuli anaweza kuamua kuhusu Zanzibar, ukitaka kupinga hili naomba utambue madaraka ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi unaweza kunielewa kwa haraka.

Hata hivyo kwa mazingira ya Zanzibar jumlisha na historia yake ya huko nyuma, alichokifanya Rais Dkt. Magufuli na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad ni njia sahihi na timilifu (mtazamo wangu), maamuzi ya kibabe na kukurupuka kwa Zanzibar hayawezi kuleta ustawi mwema katika utatuzi wa kile kinachoitwa “mgogoro wa kisiasa”, yumkini hata kile kinachoelezwa kuwa ni mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi huu mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar ni hatua kubwa na haipaswi kubezwa kwa namna yeyote ile.

Mtakumbuka yaliyotokea katika kipindi cha mwisho cha uongozi wa Rais wa awamu ya sita Zanzibar, Dkt Aman Abeid Karume, alikutana na Maalim Seif Shariff Hamad, katika aina ya mazungumzo kama yanayoendelea sasa katika Ikulu ya Zanzibar (kinadharia), kwa maana ni vikao vinavyofanana na hivi vya sas na hatimae walipomaliza ndipo ripoti ya mazungumzo yao ikatoka hadharani.

Maalim Seif Shariff Hamad, licha ya kupendwa mno na wafuasi wake lakini alikoswakoswa mawe na kuambulia mvua ya matusi pale alipotoka hadharani katika mkutano wa hadhara wa CUF, Kibandamaiti na kutangaza kumtambua rasmi Dkt. Karume kuwa ni Rais halali wa Zanzibar( kabla ya hapo CUF hawakuwahi kumtambua Karume kama ni Rais halali).

Ni mazungumzo yale yale mpaka leo kwa kiasi kikubwa yakaja na marekebisho ya kumi ya mwaka 2010 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, yaliyoruhusu kura ya maoni kwa Wazanzibari kuhusu muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Umoja wa Kitaifa.

Zaidi ya asilimia 63 (63%) ya wananchi waliopiga kura walikubaliana kuwepo mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ambayo kwa kiasi kikubwa sana imechangia kuzika chuki za kisiasa na kufungua ukurasa mpya wa siasa za Zanzibar.

Tukubaliane hapa kuwa mfumo huu wa Serikali hapa ulipingwa na unaendelea kupingwa hadharani na baadhi ya viongozi wa CCM Zanzibar, lakini hawakuwa na nguvu ya kuzuia, umewahi kujiuliza hivi Dkt. Karume alipata wapi nguvu ya kufanya maamuzi ambayo baadhi ya viongozi wa Chama chake waliyapinga bila kificho? Umejiuliza kwa nini CUF wamekuwa wakimuona Dkt. Karume kama shujaa wa Zanzibar na wakati huo huo kuna baadhi ya viongozi wa CCM Zanzibar wanamuona kama msaliti?

Unajua kwa nini kile kinachoitwa mazungumzo ya Ikulu ya Zanzibar kinapingwa na kuna viongozi wa upande mmoja wa mazungumzo hayo wametamka mbele ya ‘lenzi’ za kamera kuwa wao kama chama HAWAYATAMBUI MAZUNGUMZO YANAYOENDELEA IKULU YA ZANZIBAR, (rejea kauli za Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ndg. Vuai Ali Vuai ).

Nataka niseme hatua ya kukutana na mazungumzo ya Rais Dkt. Magufuli na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi – CUF, Maalim Seif Shariff Hamad ni njia sahihi na timilifu, hoja kubwa ni kuwa watu wanaamini kuwa CCM ni ile ile na Magufuli ni yule yule, hivyo hakuna jipya katika mkutano ule.

Ukweli kuna mambo makubwa matatu ambayo yanatofautisha mkutano wa Magufuli na Maalim Seif na mikutano mengine waliyowahi kufanya watangulizi wa Rais Dkt. Magufuli kwa maana ya Mkapa na Kikwete ambao wengi waliwaona kama ni ‘wasanii’ (kumradhi), tofauti ya kwanza Dkt. Magufuli amekutana na Katibu Mkuu wa CUF wakati yeye si Mwenyekiti wa Chama, hii inamtafautisha kwa kiwango kikubwa na watangulizi wake, lakini ili ubaini hili ni lazima uangalie kwa jicho la tatu.

Jengine ni dhamira, hii ni hoja pana ingawa kuna watakaosema hawaamini kama upande wa pili wa Muungano (Tanganyika) wanaweza kwa dhati kuona Zanzibar ikipata dawa ya utulivu wa kisiasa, lakini ni lazima tusome tulipotoka, tulipo na tunapokwenda, tulipotoka hakufanani na tulipo.

Tukumbuke Maalim Seif amekutana na Dkt. Magufuli wakati ambao vimefanyika vikao zaidi ya nane katika Ikulu ya Zanzibar, unachotakiwa kusoma hapa ni kauli za “HATUYATAMBUI MAZUNGUMZO YA IKULU” wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli amepokea taarifa ya mazungumzo hayo na amebariki huku akisisitiza yaendelee na kumalizika kwa haraka sana ili maisha ya wananchi wa Zanzibar yaendelee.

Mazungumzo yanayoendelea Ikulu ya Zanzibar kuna kikundi cha wachache hawataki kusikia na wanaendelea kutoa msimamo wa kuyapinga lakini hawana njia ya kufanya yasiendelee kwa sababu tayari yana baraka kutoka mamlaka za juu, na pengine washasoma upepo wa matokeo ya mazungumzo hayo ndiyo maana wanatapatapa.

CUF msimamo wao ni “Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuendelea kukamilisha kutangaza matokeo ili mshindi atangazwe na aapishwe (rejea tamko la Baraza Kuu CUF-Taifa walilolitoa Zanzibar), CCM msimamo wao ni “uchaguzi lazima urudiwe na tayari wanawatayarisha wafuasi wao wajiandae na uchaguzi wa marudio ( rejea kauli za Naibu Katibu Mkuu waCCM Zanzibar, Ndg. Vuai Ali Vuai ).

Nataka niseme kwa hali ya mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar na ukitizama misimamo hii ya vyama pekee vyenye nguvu Zanzibar ni wazi utulivu mkubwa unahitajika kabla ya tamko la mwisho, kwa tafsiri hii ni lazima mazungumzo yaendelee na inajuulikana wazi kuwa mwisho wa mazungumzo hayo ni lazima hoja moja kati ya hizo mbili itakufa, kwa maana wapo watakaofurahishwa na maamuzi ya mwisho ya Mazungumzo ya Ikulu ya Zanzibar na wapo watakaochukizwa na maamuzi hayo, ingawa naamini watakaochukizwa ni wachache kuliko watakaofurahia.

Tuyape muda kwa siku hizi zilizosalia na baadae hakuna shaka tamko rasmi litatoka tena si muda mrefu, kudhihaki na kukashifu eti mkutano wa Mallim na Dkt. Magufuli hauwezi kusaidi chochote katika hili si sahihi hata kidogo (mtazamo wangu), lazima tusome mazingira tuliyonayo.

Ukisikia baadhi ya viongozi wa vyama wanaponda mazungumzo haya na Mkuu wa Nchi anabariki na kupongeza mazungumzo hayo kuna cha kujifunza hapa!

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua-pepe ya allymohammed01@gmail.com

One thought on “Kwa la Zanzibar, Magufuli apewe nafasi kabla lawama”

  1. he is to slow for zanzibar issue the mass is suffering why delay people made theie choice must b respected
    do not politised the country on politician favour

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.