Yakaribia miezi miwili sasa tangu Uchaguzi wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba 2015 uingie katika jaribio la kufutwa kupitia kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, ambapo wanasheria wabobezi katika fani ya sheria, vyama takriban sita vilivyoshiriki uchaguzi, waangalizi wa uchaguzi wa nje na wa ndani, jumuiya za kimataifa kama vile “European Union”, “Common Wealth”, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na hata mabalozi wa nchi za nje waliopo Tanzania, wote wanapingana vikali na maamuzi hayo ya Jecha kwa kuwa wote wanathibitisha uchaguzi huo ulikuwa wa haki na uhuru wa hali ya juu kuliko chaguzi zote zilizowahi kufanyika katika Zanzibar, sambamba na kukosoa kwamba Jecha pekee hakuwa na mamlaka kisheria kuufuta uchaguzi huo.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Maamuzi hayo ya Jecha aliyatoa pekee yameleta taharuki kubwa katika visiwa vya Zanzibar, ambapo mijadala kuhusu hatua hiyo ya ndugu Jecha bado haijakoma, hali za maisha ya Wazanzibari kila kukicha yanazidi kuwa magumu, bidhaa muhimu zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu, kiasi ambacho kwa raia wa kipato cha chini na cha kati wanashindwa kupata mahitaji yao ya msingi.

Kumekuwa na mazungumzo yanayoendelea kusaka suluhisho la mgogoro huo uliotokea baada ya ufutwaji huo wa uchaguzi, hatua hiyo imeanza tangu vyama viwili vikuu visiwani Zanzibar kuwa na misimamo tofauti juu hatua hiyo, yaani Chama cha Mapinduzi (CCM) na kile cha Chama cha Wananchi (CUF) ambacho pia kilikuwa ni mshirika mdogo katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoasisiwa mwaka 2010. Kwa upande wao, CCM kwa nyakati tofauti wamekuwa wakielezea msimamo wao ni kurudia uchaguzi kwani uchaguzi wa awali ulishafutwa kisheria, licha ya kwamba hawaonyeshi kipengele au kifungu hasa cha Katiba ya Zanzibar na ile Sheria ya Uchaguzi juu ya uhalali wa kufutwa uchaguzi huo na Jecha kama alivyofanya. Halikadhalika, CUF wanasimamia madai yao yanayopingana na maamuzi ya Jecha, kwa kile wanachokieleza kwamba kada huyo wa zamani wa CCM hakuwa na mamlaka kisheria kufuta uchaguzi huo kama alivyofanya.

Pamoja na mazungumzo hayo yanayoendelea kuchukuwa muda mrefu sasa yakiwashirikisha wagombea wawili wakuu wa nafasi ya urais, ambao ni Dk. Ali Moh’d Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF, na pia marais wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – Dk. Amani Abeid Amani, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Dk. Salmini Amour Juma, bado wananchi wengi wana matumaini ya kupatikana suluhu, licha  ya kwamba hakuna kiongozi wa upande wowote ambaye amewaeleza wanachama na wafuasi wake juu ya wanachokijadili na hatua waliofikia hadi sasa.

Katika hatua nyengine, tegemeo jengine katika kupata suluhu ya haki katika mgogoro huo ni kupitia Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, kasi yake katika utendaji imewavutia kidogo Watanzania wa upande wa Zanzibar kitendo ambacho kimewafanya wawe na matumaini ya kwamba ataushughulikia mgigoro huu na atatenda haki.

Nikiikumbuka hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa katika sherehe za uzinduzi wa Bunge la 11 katika awamu hii ya tano ya Urais, basi sina budi kuungana na Watanzania wa Zanzibar katika kujenga matumaini hayo sambamba na kumkumbusha amiri jeshi huyu mkuu juu ya ahadi alizozitoa kwa wananchi wa Tanzania na Wazanzibari wa ujumla aliposema bungeni humo:

“Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani. Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu.

“Aidha, kwa kushirikiana na SMZ na wadau wa siasa, hususan vyama vya CUF na CCM, tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.

“Serikali nitakayoiunda itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuendelea kuimarisha Muungano wetu. Nina faraja kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais anao uzoefu mkubwa kutokana na nafasi yake ya awali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, na pia akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mimi pamoja na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein tutahakikisha tunasimamia na kuimarisha Muungano wetu.”

Hivyo kwa nukuu hiyo ni kusema, pamoja na kula kiapo kwa Rais Magufuli juu ya kuulinda Muungano wa Tanzania na kuudumisha, endapo atapuuzia au ataruhusu kuendelea kudumu kwa muda mrefu mgogoro na mkwamo huu wa kisiasa na kisheria unaoendelea kuitafuna Zanzibar na Wazanzibari ambao ni washirika muhimu katika Muungano, basi azma na lengo lake hilo halitatimia, kwani yale ambayo ameyaahidi yatokee katika utawala na uongozi wake ikiwemo kuwafanya wananchi wa Tanganyika na Wazanzibari wafurahie matunda ya Muungano na kuondolea vikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu, yatazidi kwa Wazanzibari kuendelea kunung’unika na kulalamika na kutokuwa na imani na amani na Muungano wenyewe.

Kwa kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli, nina imani ndani ya siku chache zijazo atautatua mgogoro huu kwa haki, kwa salama na amani ikiwa anataka aifikishe Tanzania pazuri. Kitendo cha tarehe 21 Disemba tayari kinaashiri ameanza kuitekeleza ahadi hiyo aliyoiweka ya kuutatua mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar kwa kumualika Maalim Seif katika ofisi yake hapo Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu baada ya mazungumzo hayo ya masaa mawili, Rais Magufuli alipata kujua hatua iliyofikiwa katika mazungumzo ynayoendelea Zanzibar na akayapa baraka zake. Kasi hii aliyoanza nayo kiukweli ni ya kuridhisha ukilinganisha na awamu nne zilizotangulia kabla yake.

Hivyo nimuombe, Rais wangu Magufuli kwamba aharakishe kulimaliza jaribio hili kwa salama na amani, kabla fitina haijaingia katikati na kumuharibia kama ilivyowaharibia wenziwe waliotangulia. Lakini pia namuusia atende haki katika maamuzi yake bila ya kusuasua. Aongeze kasi ya kulishughulikia ili limalize haraka kwani Wazanzibari wameshasubiri sana. Subira yao isijaribiwe tena baada ya hapa maana nao ni binaadamu.

Iwapo kasi ya Rais Magufuli haikutumika kuwatatulia Wazanzibari mkwamo huu, basi utawala wake unapaswa kujuwa kwamba kuna siku wanyonge hawa watachoka kuwa watulivu na wavumilivu kama alivyowapongeza wakati alipozungumza na Maalim Seif. Na watakapochoka watu waliodhulumiwa kwa kipidi kirefu kama hawa, basi zile sifa njema ambazo Tanzania inajivunia kuwa ni kisiwa cha kutunza amani sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kutatua mizozo na migogoro mbali mbali inayozikumba nchi jirani, itaharibiwa vibaya.

Tunakuombea Rais Magufuli umalizie vyema kama ulivyoanza vizuri.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.