Kwa miongo kadhaa, raia wa Jamhuri ya Gongo walipambana dhidi ya uwongozi uliokuwepo ili kuleta mabadiliko. Walipigana mchana na usiku, jua na mvua, ili mabadiliko yapatikane.

Adidi na Adodo walikuwa marafiki wakubwa na pia viongozi waliokuwa wakitaka madadiliko.

Na Salum Abdullah Salum
Na Salum Abdullah Salum

Katika uchaguzi mkuu, Adidi aligombea ukuu wa nchi. Kutokana na sera nzuri na umakini pamoja na ustadi wa kuzungumza, akapata umaarufu mkubwa na kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Baada ya kutangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi, Adidi akaapishwa kuwa mkuu wa nchi ya Jamhuri ya Gongo na baada tu ya kuapishwa, akamchagua Adodo kuwa waziri mkuu wa jamhuri hiyo na kuunda serikali.

Baada ya kuunda serikali, utaratibu ukawekwa wa kuajiri watu katika sekta mbali mbali. Ikaundwa wizara maalum inayoshughulika na ajira zote nchini humo.

Katika wizara hiyo kukawa na majengo mawili pacha na katikati baina ya majengo hayo mawili kukachimbwa bwawa kubwa la maji na msimamizi mmoja wa bwawa hili ambae amekamata jiti mkononi mithili ya mkuki.

Kwa vile ajira zilikuwa nyingi na lukuki kuliko hata idadi ya wananchi, serikali ilikuwa na uwezo wa kuajiri watu wote katika nchi hiyo.

Sharti likawekwa ambako ilimlazimu kila anayetaka ajira apitie wizara hiyo na kupeleka maombi ya ajira katika jengo la wizara hiyo lililokuwepo katikati ya nchi hiyo.

Ilimlazimu kila mmoja kupeleka maombi katika jengo la kwanza na baada ya maombi kupokelewa ilimlazimu muombaji kupika katika bwawa na kuchomwa jiti makalioni na msimamizi wa bwawa hilo na baada kuvukwa bwawa hilo muhusika anaenda jengo la pili hupangiwa ajira yake katika sekta husika kwa mujibu wa elimu yake.

Waziri Mkuu Adodo alimkanya mkuu wa nchi Adidi juu ya suala hilo na kumuonya kwamba litasababisha maadamano ya kuwatowa madarakani, Mkuu alimjibu jambo hilo halitotokea katika madaraka yake.

Lakini, muda si mrefu maandamano yalizuka, watu waliandamana mpaka katika kasri la Mkuu wa Nchi.

Umma wa watu ulilizunguka kasri kuu kiasi ambacho ulikuwa hujui watu wameanzia wapi na kumalizikia wapi.

Adodo akamuambia Adidi: “Unaona sasa? Si nilikwambia kuwa tusifanye haya? Unaona sasa, leo tunaondoshwa madarakani”. Adidi akumuambia Adodo: “Subiri tuone”.

Mkuu Wa Nchi aliyapokea maadamano hayo na kuwakaribisha wageni wake katika kasri lake na baada ya hapo aliwataka wachaguwe wawakilishi wao watano na kuwakaribisha katika  ukumbi rasmi wa wageni kueleza shida na matatizo yaliyowaleta hapo.

Wakakaribishwa kwa vyakula na vinywaji na baadaye Mkuu akawataka waeleze shida zao na lengo na madhumuni ya maadamano yao.

Kiongozi wa wawakilishi wa waandamanaji alimueleza Mkuu wa Nchi: “Bwawa limekuwa dogo na watia majiti hawatoshi, hivyo bwawa liongeze ukubwa na mtia majiti mmoja hatoshi waengezwe wawe wengi ili wananchi waajiriwe wengi na haraka kwa siku ili tatizo la ajira lishe haraka”.

Mkuu alilipokea ombi lao na kulifanyia kazi haraka, kiasi ambacho wananchi hata hawajaondoka ombi lao lilianza kufanyiwa kazi.

Baada ya wawakilishi kutoka katika kasri waliwaeleza waandamanaji kuwa ombi lao limekubaliwa na tayari limeanza kufanyiwa kazi na hivyo warudi majumbani na wajiandae kuajiriwa kwa wingi na kwa haraka.

Mkuu wa Nchi Adodo alimuelekea Waziri Mkuu Adidi na kumwambia: “Unaona? Nilikwambia subiri, hawa akili zao zipo mikononi mwetu. Tutakavyo, tutaziendesha na watatuunga mkono”.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.