Napenda kuelezea machache tu kwa wale wote ambao ni wepesi wa mioyo yao na wanajisahau kuwa sisi Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla tupo katika mapambano na harakati za kimageuzi katika nchi yetu.

 

Vijana wa Kizanzibari wakiwa kwenye hamasa za kudai mamlaka kamili ya nchi yao kutoka kwenye Muungano.
Vi

Kwa kutambua hilo kwanza, basi hatuna budi kabisa kujiridhisha kua sio kazi rahisi kama wengi wanavyodhania kuondoa tawala ambazo zimekaa kwa muda mrefu na ambazo bado zinashikilia mihimili mikuu ya mageuzi ya kweli, vikiwemo vyombo vya ulinzi, fedha na tume za uchaguzi. Tukumbuke kuwa chama kinachotawala ndicho kilichoshikilia dola, ambayo ndani yake kuna watu wenye maslahi yao na ambao hawapendi kukatishiwa utamu wa ladha ya kutawala.

Na Dhamir Ramz
Na Dhamir Ramz

Baada ya kutambua yote hayo, nafikiri sasa utapata picha ni ugumu gani ambao upo katika mapambano yetu ya mageuzi katika kuelekea kubadilisha mfumo mzima na kutandika misingi ya sheria na utawala bora pamoja na kulinda rasilimali za wananchi na kutengeneza taifa la uchumi ambao unakua kwa kasi na wenye kuendana na ushindani uliopo duniani chini ya dhana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Historia imetufundisha kuwa mafanikio katika mapambano kama haya ya kimageuzi sio rahisi na wala si ya miaka michache. Wengi wetu ni mashahidi wa namna wamageuzi mbalimbali duniani, akiwemo marehemu Mzee Nelson Mandela wa Afrika Kusini, walivyopata tabu hata kufanikiwa kuleta mageuzi katika nchi zao. Mfano wa Mzee Mandela ni wa kuigwa kwa sababu alivumilia mateso na hata kufungwa kwa miaka 27, lakini hakukata tamaa na alifanikiwa kuitoa Afrika ya Kusini kutoka kwenye mikono ya utawala wa kibeberu na wa kibaguzi, na hatimae kuwa rais wa mwanzo kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia aliyeapishwa tarehe 10 Mei 1994 baada ya zaidi ya miaka 40 ya mapambano.
Mfano huu unakwendana vyema na hali ya Zanzibar. Vyama vyetu vya kimageuzi vilianza harakati zake tokea mwaka 1992, na kwa upande wa Zanzibar, chama cha CUF kilishiriki uchaguzi wake wa kwanza mwaka 1995 na kufanikiwa kupata viti 24. Kwa mara ya kwanza katika historia, chama tawala cha CCM kilipoteza idadi kubwa ya viti katika Baraza la Wawakilishi. Katika Uchaguzi wa mwaka 2000, CUF ilivuna zaidi kwa kupata viti Unguja, sehemu ambayo CCM ilikuwa inajivunia kama ni ngome yake.

Wakati tunaingia kwenye uchaguzi wa 2005, CUF ilijiongezea kitu chengine ambacho ni kuweza kuingia kwenye Tume ya Uchaguzi na kuwakilishwa na makamishna wawili. Mwaka 2010, CUF ilifanikiwa kuishawishi serikali iliyokuwepo madarakani kupitia Muafaka wa Kisiasa na kupelekea kupigwa kura ya maoni ambayo wananchi kwa asilimia 66.7 walikubali kuleta mabadiliko ya kikatiba na kuweka misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo huo, CUF iliendelea kupata viti zaidi kwa upande wa Unguja kwa kufanikiwa kuvuna viti vinne. Pia ilifanikiwa kuingia katika Serikali ya Umoja wa kitaifa, ambapo ilisimamisha makamu wa kwanza wa rais, mawaziri watano na manaibu waziri wawili, ambao pia walikuwa ni wajumbe wa Baraza la Mapinduzi. CCM, licha ya kushinda urais, kura za mgombea wake wa urais zilizompita wa CUF zilikuwa 3,000 tu.

Katika uchaguzi uliofanyika 25 Oktoba 2015, CUF imeendelea kuimarika zaidi na safari hii kwa mafanikio makubwa, hasa baada ya majumuisho na matokeo rasmi katika vituo vya kupigia kura kuonyesha imepata jumla ya viti 9 kwa Unguja, ambayo ni ngome ya CCM na pia kuonyesha imeshinda matokeo ya urais kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na mawakala wa chama hicho, ambazo pia zilisainiwa na mawakala wa vyama vyengene vilivyoshiriki uchaguzi, na kutolewa tamko na mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, siku ya tarehe 26 Oktoba 2015.  Matokeo hayo yanaonesha Maalim Seif aliongoza kwa zaidi ya kura 20,000. Waangalizi wote wa ndani na nje ya nchi waliusifu uchaguzi mzima kuwa ulikwenda kwa uhuru na haki kwa kiasi kikubwa zaidi kulinganishwa na chaguzi nyengine zilizowahi kufanyika.

Ushindi huu wa CUF ndio ulioifanya CCM, ambayo imeonekana kuwa imekwisha kupoteza uchaguzi huu, kumshinikiza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuyafuta matokeo yote ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani tarehe 28 Oktoba 2015 ikiwa ni kinyume na sheria zote za nchi.

Hii inaonesha ni kwa kiasi gani dhana ya mabadiliko sio jambo la mara moja, na limeambatana na ugumu na mikikimikiki mengi sana. Kwa hivyo, uvumilivu mkubwa unahitajika ili kufikia mafanikio kama yaliyopatikana na chama cha ANC kule Afrika ya Kusini chini ya Marehemu Mzee Nelson Mandela.

Historia imeendelea kutuonyesha kuwa CUF na vyama vyengine vya siasa vinaendelea kuongezeka nguvu kila mwaka, na vipi CCM inaendelea kudhoofika hapa Zanzibar na Bara.

Kila uchaguzi unaokuja, CCM huwa inapoteza zaidi kuliko uliotangulia, na badala yake hubakia kutumia ghiliba, nguvu na uhuni kusalia madarakani. Lakini hizo mbinu zina mwisho wake. Na mwisho huo ni kwa mabadiliko kushinda. Tusivunjike moyo.

Imehaririwa – ZD

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.