Kauli ya Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, mbele ya mkutano mkuu wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kule Dodoma ya kuwataka wana-CCM wenziwe “wasiwe kama samaki” inawakhalisi wahusika kwa mengi kutokana na matendo na kauli za watu hao. Na hapa nitasema kwa nini.

Dk Ali Mohamed Shein
Dk Ali Mohamed Shein

Miongoni mwa sifa za samaki ni kusahau. Uchaguzi huru na wa halali ulifanyika na kumalizika Zanzibar mnamo tarehe 25 Oktoba 2015, ambapo uhalali wake ulitajwa na wagombea wakuu wawili wa urais, Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF) kabla na baada ya kupiga kura zao na pia waangalizi wa ndani na nje ya nchi. Vile vile, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iliutambua hivyo tangu kwenye matayarisho yake mpaka tarehe 27 Oktoba 2015. Lakini kufikia tarehe 28 Oktoba, mwenyekiti tume hiyo, Jecha Salim Jecha, akajitokeza peke yake na kwa matakwa yake na ya CCM kuufuta uchaguzi huo kwa njia za haramu ambazo zimeidhalilisha katiba pamoja na sheria zote zinazosimamia uchaguzi za Zanzibar na utawala wa nchi kwa ujumla.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

CUF, ambacho kilikuwa mshirika mdogo kwenye serikali ya umoja ya kitaifa iliyokuwa madarakani kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, kiliamua kuacha madaraka ya kiserikali kwa kuwa muda wa viongozi wake serikalini ulimalizika tarehe 03 Novemba 2015. Lakini CCM  wanasema ni halali kubakia madarakani na wanaipindisha katiba na kuipa tafsiri watakavyo wao ili wajipe uhalali huo.

Sikubaliani na hoja zao wanazozitoa kujihalalisha, lakini kwa maslahi ya makala hii sitaki niwapinge ili nithibitishe “usamaki” wao. Baada ya Dk. Shein kusitisha shughuli zake za urais tangu kumalizika kwa uchaguzi na baada ya shinikizo la wanaojiita wanasheria wa CCM kupitia vituo vya televisheni, hasa Channel Ten, kumlazimisha kiongozi huyo akalie kiti cha urais kinyume na katiba, kuanzia Jumamosi ya tarehe 21 Novemba 2015, Rais Shein alianza rasmi kufanya shughuli za kiurais kwa kukagua miradi ya maendeleo ili kuonyesha uhalali uliokuwa ukizungumzwa na wanasheria wa chama chake.

Baada ya Jecha kufuta uchaguzi kwa njia ya mazingaombwe, kumekuwa na mazungumzo yanayoendelea juu ya khatma ya Zanzibar na uchaguzi alioufuta Jecha, ambayo washiriki wake ni Dk. Shein mwenyewe, Maalim Seif na baadhi ya marais wastaafu wa Zanzibar, lakini kinachoshangaza ni kwamba CCM wanatuaminisha lazima tukubali kwamba Dk. Shein ni rais halali kwa kusema sheria inamruhusu aendelee hadi rais mwengine atakapoapishwa, lakini hapo hapo, wao mwenyewe CCM wanamkataa Rais Shein kuwa si rais halali wa Zanzibar, japokuwa hawatamki hadharani.

Kwa nini? Ijumaa ya tarehe 20 Novemba 2015, CCM walikuwa na mkutano na waandishi wa habari, ambapo Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Bibi Waride Bakari Jabu alipoulizwa na mmoja kati ya waandishi waliohudhuria mkutano huo kwamba anazungumziaje mazungumzo yanayoendelea baina ya Dk. Shein na Maalim Seif pamoja na marais hao wastaafu, alijibu: “Wanayozungumza na hao wastaafu ni yao wenyewe sisi hatulijui (CCM) na haliko kwetu na haliko ‘official’ (rasmi).”

Sasa hapa CCM tuipe nafasi gani? Ikiwa wanatuaminisha Dk. Shein ni rais halali wa Zanzibar, lakini hapo hapo wanamuharamisha kupitia mazungumzo yanayomshirikisha yeye, Maalim Seif na baadhi ya marais wastaafu juu ya uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015 pamoja mkwamo wa kisiasa uliopo, tena mazungumzo hayo yanafanyika katika ofisi zake za kirais (Ikulu). Kama ni halali anashiriki nini kwenye mazungumzo?

Imehaririwa – ZD

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.