“Man qalal balozi fahuwa labayka”, ndivyo uwendavyo msemo wa Kiarabu ukimaanisha chochote alichokwishasema mkubwa fulani, basi kitu hicho kwa vyovyote vile ni sahihi tu. Labda tuseme Kizungu chake ni “Yes, Boss!” na Kiswahili chake ni “Ndiyo Mzee!”

Sehemu wa wajumbe wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sehemu wa wajumbe wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni msemo unaoonesha kuwa akili na uwezo wa kufikiri wa baadhi ya wanaoogozwa huanza na kuishia penye pua ya wanayemfuata kama kiongozi wao. Kwamba kuna waongozwa ambao ni watu wa kufuata mkumbo mbele ya kiongozi wao, kiasi cha kwamba akili zao husita kufanya kazi mbele yake na ikawa kila alisemalo yeye, huwa ndilo hilo hilo hakuna jengine, ingawa jambo hilo hilo likisemwa na mwengine asiyekuwa kiongozi wao, huwa silo. Halifai.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Kwa Zanzibar, msemo huu wa Kiarabu una asili yake kwenye mfumo wa chama kimoja cha kisiasa wakati huo kukiwa na mabalozi wa nyumba kumi kumi, ambao walikuwa na sauti na nguvu ya ajabu kwenye maeneo yao licha ya kuwa walikuwa tu wajumbe wa ngazi za chini kabisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Watu hao, ambao tunaweza kusema hivi leo nafasi zao zimechukuliwa na masheha – wakiwa wameongezewa ukubwa wa maeneo na nguvu za kisheria kwa kuwa maafisa wa serikali.

Hiyo historia tuiwache kwa sasa lakini tubakie kwenye uhusiano wa msemo wenyewe na hali halisi iliyopo mbele yetu, ambapo CCM, viongozi na wafuasi wake wanaonekana dhahiri bado wao wako katika zama zile zile za “Man qalal balozi fahuwa labayka” hata kama mfumo huo uliondoshwa rasmi.

Bunge ni mahala pamoja ambapo hilo liko wazi, na wala hakuna haja ya kutoa mifano mingi kulithibitisha hili. Haraka haraka, hebu tuvute kumbukumbu (hansard) kupitia Bunge la Kumi. Ukienda katika kumbukumbu hizo, utakuta Kambi Rasmi ya Upinzani ilitoa rai nzuri ili kuzuia matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi, matumizi ambayo yasio na lazima kama vile safari za nje za kila mara za viongozi na hata kozi fupi za watendaji serikalini.

Lakini kwa kuwa hoja hii haikutolewa na kiongozi wa CCM, ikapingwa vikali sana na wabunge wa CCM. Wakati huo, Rais Pombe Magufuli naye alikuwa mbunge na waziri mwandamizi serikalini. Wakati alipokuja rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, kuponda kauli kama hiyo, wabunge wote wa CCM, hapana shaka, akiwemo Magufuli mwenyewe walipiga makofi na kushangiria hadi meza zikataka kuvunjika.

Cha ajabu ni kuwa Ijumaa ya tarehe siku ya 20 Novemba 2015, wakati rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pombe Magufuli, alipolihutubia Bunge la 11 katika sherehe ya ufunguzi wake, alisema kauli ile ile ambayo yeye akiwa mbunge kwenye Bunge la 10 ilikuwa hoja ya kambi ya upinzani. Alitangaza rasmi kufuta safari za nje kwa watendaji wa serikali bila dharura kubwa na maalum. Akaziponda safari hizo kuwa zimekula mabilioni ya pesa za walipakodi. Bila ya aibu wala haya, wabunge wale wale wa CCM ambao walikuwa wamebaki peke yao bungeni,  walishangilia kwa shangwe, vifijo na mayowe makubwa kauli hiyo, kama kwamba ni kitendo cha kishujaa zaidi na hakikuwahi kuchangiwa na mtu yeyote bungeni humo!!

Watanzania hawasahau haraka kama walivyo wabunge wa CCM, maana dakika chache baada ya tukio hilo, mitandao ya kijamii ikawa imejaa mishangao ya wananchi, wakikumbuka kuwa wapinzani kwa akili zao za ubunge tu walishawahi kufikiria na kulieleza hadharani na bungeni jambo hilo, lakini Rais Magufuli  ilimuhitaji kwanza apate  mafunzo ya kiraisi, ndipo akili yake iweze kulifikiria hilo na kulitolea maamuzi yasiyopingika kwa wabunge wa CCM ambao hao hao ndio waliopinga hoja hiyo hiyo ilipoletwa na wabunge wa upinzani.

Laiti kama wabunge wa CCM katika Bunge la 10 wangekubali hoja ya kambi ya upinzani na kuzuia safari za nje kama alivyotangaza Raisi Pombe, nchi ingeweza kuokoa kiwango kikubwa cha fedha zilizotumika kulipia safari hizo, fedha ambazo zingelipia gharama nyengine za kimaendeleo kwa taifa. Lakini kwa kuwa aliyesema wakati ule hakuwa “Balozi” wao, wakaipinga hoja ile na kutoa kauli chafu dhidi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Sasa ndipo nami ninapopata suali la kuwauliza waheshimiwa wabunge wangu wa CCM: huu mfumo wa “Man-qaalal balozi fahuwa labayka” hadi lini?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.