INSAFU ni kito na johari yenye thamani adhimu. Kama wewe ni miongoni mwa watu waliojaaliwa kuwa na johari hiyo katika kuhukumu mambo, soma maelezo yafuatayo, kisha jibu suali la maelezo hayo kwa insafu.

Mwaka 1995 wakati ilipodhihirika kuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameshinda uchaguzi, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Ameir Mohamed, alitamka kuwa chama chake kisingeyakubali matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya visiwa hivyo (ZEC). Hatimaye baada ya kimya kirefu na cha ajabu, ZEC ikamtangaza mgombea urais wa CCM, Salmin Amour Juma, kuwa mshindi kwa wingi mduchu wa kura. Kulalama kwa CUF hakukusaidia kitu.

Mwaka 2000, Zanzibar kilifanyika kitu katika zoezi la uchaguzi ambacho waangalizi wa kigeni, badala ya kukiita kwa Kiingereza ‘election’ walikipa jina la ‘shambles ‘ yaani vurumai, mchafukoge, shaghalabaghala.

Askari polisi walibeba masanduku ya kura na kukimbia nayo. Uchaguzi wa majimbo kadhaa ukafutwa, na yaliyotokea Januari 2001 ya maafa ya roho za watu siyakumbushi tena nikatonesha vidonda. CUF ililalama na kulalama lakini matokeo yakatangazwa na rais akaapishwa. Alikuwa ni Amani Karume.

Ya 2005 ya watu waliofunga Ramadhani kuwekewa mzingiro Mtendeni kwa muda wa siku tatu na adhabu na mateso waliyopata raia kwa jeshi la polisi anayakumbuka kila anayefuatilia chaguzi za Zanzibar.  Yote hayo yalitokana na malalamiko ya CUF dhidi ya matokeo ya uchaguzi. Pamoja na yote hayo, matokeo yalitangazwa na rais akaapishwa kwa wakati na shughuli za nchi serikali na nchi zikaendelea kama kawaida.

Ni 2010 tu na baada ya maridhiano ya kihistoria yaliyopata ridhaa ya Wazanzibari kisheria na kikatiba ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na licha ya kutoridhishwa tena na jinsi ZEC ilivyohesabu kura na kupanga matokeo, mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye inajulikana rasmi kuwa alinasihiwa kwanza ayakubali matokeo hayo, alimpongeza Dk. Ali Mohamed Sheni wa CCM kwa kutangazwa mshindi wa urais.

Suali la maelezo hayo mafupi linakuja sasa, nalo ni hili: kwa jinsi uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu ulivyofanyika katika upigaji kura, na zoezi la kuhesabu kura lilivyofanywa katika majimbo yote ya Unguja na Pemba na kuidhinishwa rasmi na maafisa wasimamizi wenyewe wa ZEC majimboni, na baada ya waangalizi wote wa ndani na nje kuridhishwa na uchaguzi huo; kwa kuzingatia uzoefu wa chaguzi zote zilizopita, laiti kama mahala pa ulalamikaji walipokuwa wamekaa Pandu Ameir Kificho, Vuai Ali Vuai na Shamsi Nahodha wangekaa Seif Sharif Hamad, Nassor Ahmed Mazrui na Ismail Jussa Ladhu je, Jecha Salim Jecha angeufuta uchaguzi mzima wa Zanzibar na kutaka urejewe tena?

Na je hadi leo hii kungekuwa kunaendelea kufanywa vikao vya marais wastaafu kutafuta mwafaka wa uchaguzi?

Nakuomba ulijibu suali hili kwa INSAFU bila kujali kama wewe ni kiongozi, mwanachama au mkereketwa wa chama fulani cha siasa. Nakuomba pia kama inayumkinika ulifikishe suali hili kwa viongozi wa CCM waliokuwepo Bwawani Oktoba 27 pamoja na wale walioshiriki kwenye vikao vya Ikulu.

Kama watalijibu suali hili kwa INSAFU naamini watapata busara kubwa ya kuumaliza mgogoro BANDIA wa uchaguzi alioufinyanga, Jecha binafsi au kwa kutumwa na kikundi kidogo cha watu fulani.

*Makala ya Abdulfattah Mussa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.