“Tutatafuta kujua ni kwa nini tumeshindwa. Hata hivyo, tunakubali matokeo bila masharti yoyote. Bado hatujajua matokeo kamili ya mwisho yatakuwaje”, kaimu mwenyekiti wa chama tawala kinachoungwa mkono na jeshi cha Myanmar (zamani Burma), Union Solidarity Development Party (USDP), aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), siku moja tu baada ya kura kupigwa.

Si mara ya kwanza kwa chama cha upinzani cha National League for Democrasy (NLD) kushinda. Kiliwahi kushinda uchaguzi wa mwaka 1990, lakini matokeo yalifutwa na badala yake kiongozi wake, mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel, Bi Aung San Suu Kyi, akawekwa katika kifungo cha nyumbani cha muda mrefu.

Hilo halitofautiani sana na ufutaji wa matokeo uliofanywa tarehe 28 Oktoba na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kwa shinikizo la wahafidhina wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa uchaguzi wa Zanzibar. La kushukuru ni kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa nafasi ya urais, Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), hadi sasa hajawekwa kwenye kifungo cha nyumbani, bali amekuwa kiguu na njia kusaka suluhisho la amani la mzozo uliozushwa kwa makusudi na usio na maana.

Myanmar kuna Rohingya, Zanzibar kuna Uamsho

Siku zote utawala wa kijeshi nchini Mnyanmar chini ya chama cha USDP, umekuwa ukikosolewa kwa ukatili. Ulikuwa utawala wa kidikteta ambao kwao haki za raia ni kitu adimu sana, hasa Waislamu wa kabila la Rohingya.

Hapa petu unaweza kulifananisha hili la Waislamu wa jamii ya Rohingya na hadithi ya viongozi wa Uamsho ambao wamewekwa korokoroni kwa sababu za kisiasa, na pia kesi yao inapigwa danadana kila siku chini ya utawala wa CCM. Kuna mateso na udhalilishaji mkubwa ambao viongozi hao wamefanyiwa wakiwa katika magereza ya Tanzania Bara, kama vile ambavyo mateso na udhalilishaji vimekuwa vitu vya kawaida kwa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Kwa Rohingya chini ya utawala wa kijeshi, hali imekuwa mbaya zaidi, kwani wanakumbana na mauaji, mateso, kupigwa, kuharibiwa mali zao, nyumba zao zinachomwa moto na mambo mengine mengi ambayo wanafanyiwa na Mabudha wenye itikadi kali chini ya utawala wa USDP. Bahati mbaya, hata upinzani wa NLD nao unalaumiwa kwa kunyamaza kimya kwenye suala hili.

Mauaji na ufukara kote kuwili

Sambamba na mauaji dhidi ya jamii moja ya Rohingya, wapinzani kwa ujumla wao hawako salama nchini Myanmar chini ya utawala wa kijeshi. Kuna visa vingi vya watu kupigwa na kuuawa au kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha kwenye taifa hilo la Asia ya Kusini. Hata hivyo, ni nadra kwa wahusika wa mauaji hayo kufikishwa kwenye mikono ya sheria, kwani wanakuwa ni wale wale wenye mikono yenyewe, kwa maana ya vyombo vya dola.

Hapa petu, mnamo tarehe 20 Aprili 2002, shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Human Rights Watch (HRW) lilichapisha ripoti yake, kwa jina “Risasi Zilinyesha Kama Mvua”, inayozungumzia jinsi vikosi vya ulinzi na usalama chini ya serikali ya CCM vilivyofanya mauaji ya takribani watu 35 na kuwajeruhi zaidi ya 600 visiwani Zanzibar pamoja na kuwasababishia maelfu ya wengine kukimbilia nchi jirani .

Ripoti hiyo inasema kuwa licha ya ushahidi wa wazi wa vikosi vya serikali kutumia risasi kuwauwa watu, kutesa na kuwanyanyasa wa kijinsia, ikiwemo ubakaji, hadi inatoka “hakuna hata mmoja katia ya wahusika ambaye amefikishwa katika vyombo vya sheria.” Ni miaka mingi tangu ripoti hiyo itoke na hadi dakika hii hakuna ambaye amechukuliwa hatua.

Kama ilivyo CCM, nayo USDP inasifika kwa uongozi wa mkono wa chuma. Wapinzani wa kisiasa na jamii ya Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakinyanyaswa kupita kiasi, na kama ilivyo Tanzania, nayo pia ina hali mbaya sana kiuchumi.

Baada ya miaka 20, USDP yasema basi, baada ya miaka 50 CCM yasema bado

Licha ya kufanana kwa mengi, mwaka huu wa 2015 umeonesha kuwa USDP na CCM zinaweza kuwa na mambo ya kuwatafautisha. Wanajeshi wa USDP wamesema miongo miwili wanaamini inatosha kwa vile tayari uchaguzi umeshamtoa mshindi na wao wanakubali kushindwa. CCM wapo tangu enzi za Afro-Shirazy Party, miaka nenda miaka rudi, nusu karne sasa, lakini likija suala la kufanya uchaguzi na kushindwa hilo halipo kabisa vichwani mwao.

CCM ambayo imeitia nchi katika umasikini kama vile USDP walivyoitia Mnyanmar, kwa kuwa pana uhusiano mkubwa baina ya utawala wa kikatili na kurudi nyuma kwa nchi kimaendeleo, CCM bado haioni ulazima wa kubadilika na kufuata matakwa ya umma.

Kufutwa uchaguzi Zanzibar ni matokeo ya kukosekana kwa bao la mkono ambalo CCM wamezoea kupiga. Huko nyuma wameiba sana na wala hukusikia uchaguzi ukifutwa, na yametokea mapungufu mengi mno lakini uchaguzi hawakuufuta, lakini mara hii umefutwa kwa sababu njia ya kuiba ilikosekana.

USDP, yenye mizizi ya moja kwa moja kwenye jeshi la Myanmar, imewahi kufuta uchaguzi pia ambao ulikuwa umempa ushindi mpinzani, lakini baada ya kukaa na kutafakari sasa ikaona wakati wa kuusikiliza umma umefika. CCM, ambayo kijuujuu ni chama cha wakulima na wafanyakazi na wakwezi na wakulima na sio cha kijeshi, hujisifu kuwa haitotoa nchi waliyoipata kwa mapinduzi kwa vikaratasi vya kura. Kiukweli ni kuwa CCM ni chama cha kijeshi kwa maana ya ufanyaji kazi wake, kwani hutumia vikosi vya usalama kuuwa, kupiga na kutesa na kukilinda ili kiendelee kuwepo madarakani.

USDP imeamua kukubali kushindwa ni uungwana, jambo ambalo CCM limewameshida hadi dakika hii. Wakati USDP ikikubali kupoteza kwenye uchaguzi wa kidemokrasia na kuahidi kujitathmini ilivyoshindwa, CCM ya Zanzibar safari hii imeshindwa kuiba kura za wananchi na badala yake imeamua kufuta uchaguzi!

 *Makala ya Rashid Abdullah

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.