Ushabiki unaoendelea kufanywa na wengi wetu kwa makeke yaliyoonyeshwa siku za karibuni na Rais mpya wa Tanzania Pombe Magufuli ni wa kuangalia upande mmoja tu wa sarafu. Lakini kwa maoni yangu upande wa pili wa sarafu hiyo unathibitisha maneno ya JK alompa Magufuli jina la TINGATINGA yaani utumiaji nguvu tu wa kusomba chochote kilichoko mbele, kiwe kibaya au kizuri na chenye faida au madhara.

Magufuli karithi serikali iliyooza ya JK. Na hayo anayofanya anayafanya kutaka kuthibitisha hilo. Lakini yeye alitarajia nini katika ziara zake za kushtukiza kwenye Wizara ya Fedha na Hospitali ya Muhimbili zaidi ya aliyoyakuta? Hayo si mapya, ni mambo ya kawaida katika Tanzania yetu na anayajua hata Mmachinga wa Kariakoo.

Kama kiongozi, inatakiwa kwanza aunde serikali yake, tuone hizo sura za baraza lake la mawaziri akiwemo waziri mkuu (maana uteuzi aliofanya wa Mwanasheria Mkuu umeonesha hana mpya) kisha atoe changamoto kwa mawaziri wake wote waunde wizara makini kiutendaji na kuwapa muda wa siku 100 wa kuonesha utendaji wao, kisha ndipo aanze kufanya hizo ziara zake za kushtukiza ili ajipime yeye mwenyewe na serikali aliyounda kuona ina ufanisi wa kiwango gani. Lakini anachokifanya sasa ni aina mpya ya USANII tu na kuwafanya mhanga na mbuzi wa kafara baadhi ya watu.

Kama kweli Magufuli ni kiongozi anoelewa vipaumbele vya majukumu yake alipaswa alishughulikie kwanza suala la uchaguzi wa Zanzibar ambako chama chake kimeshindwa lakini kimeamua hata kuvunja katiba ya nchi kwa kuzuia kukamilishwa mchakato wa uchaguzi.

Kabla ya kumrudia Magufuli niliseme hili kwanza, kwamba aliyeifikisha Zanzibar hapa ilipo ni JK si mtu mwengine yeyote. Maana kama alivyosema Fatma Karume, aliyewanyima Wazanzibari haki yao ya kikatiba ya kuchagua Rais wamtakaye ni yule aliyetuma jeshi la Muungano TPDF au JWTZ likazingire bwawani na kumzuia makamu mwenyekiti wa ZEC asikamilishe kutangaza matokeo ya uchaguzi. Si Jecha, Kificho wala Ali Muhammed Sheni .Tukio lile la kiharamia halikufanywa na vikosi vya SMZ ni vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo Amiri Jeshi wake Mkuu ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete, wakati ule.

Ifahamike pia kwamba iliyopinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar ni CCM ambayo hadi wakati huu tunaozungumza kabla ya kukabidhiwa hatamu JPM kama anavyoitwa, inaongozwa na Mwenyekiti Taifa Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa hiyo ni yeye aliye na kauli ya mwisho ya kuamua kama chama chake kikubali au kikatae kuwa kimeshindwa katika uchaguzi wa Rais wa Zanzibar. Tukumbuke  pia kuwa baada ya amri aliyotoa JK ya Mapinduzi dhidi ya uchaguzi wa kidemokrasia uliofanyika Zanzibar na ambao umepongezwa na dunia nzima wakiwemo hata wasimamizi wa ndani, JK hakutoa tamko lolote wala kuchukua hatua yoyote mpaka siku moja kabla ya kuondoka madarakani ndipo alipokubali kuonana na Maalim Seif Sharif Hamad ili eti akabidhiwe nyaraka za kuthibitisha ushindi wa cuf. Na yeye akasema, kwa kuwa kabakiwa na saa 24 tu akiwa Rais atamkabidhi suala hilo mrithi wake yaani Magufuli. Upeo wa usanii!
Ni kubwaga manyanga, kama alivyonambia ndugu yangu mmoja.

Nimalizie kusema kwamba JK ameifikisha Zanzibar mahala pabaya zaidi ya pale alipoikuta 2005 alipoingia madarakani, mahala ambapo endapo hazitofanyika jitihada za Watanzania wote na wa vyama na asasi zote huenda isipatikane njia ya kutoka kwenye mkwamo huu ila baada ya kutokea maafa makubwa ya roho za watu; namuomba Mungu ajaalie tusifike huko.

Kwa hiyo namueleza Rais mpya wa Tanzania kwamba jukumu la kwanza ambalo alipaswa  kulitekeleza mara baada ya kuapishwa TU lilikuwa ni kukutana na Maalim Seif Sharif Hamad na kushauriana naye jinsi ya kuiongoza Tanzania katika mfumo mpya wa uongozi, wa kuwa na vyama viwili tofauti vinavyotawala katika pande mbili za Muungano, na si kuwadharau Wazanzibari kiasi hiki kwa kuendelea kufanya usanii wa utingatinga tunaoushuhudia hivi sasa.

Rais Magufuli anajua, kama anavyojua JK, kuwa CCM imeshindwa Zanzibar katika uchaguzi halali zaidi ya ule uliompa yeye Magufuli uhalali wa kuwa rais wa Tanzania lakini imeamua kutumia vyombo vya dola kuzuia ushindi wa CUF.

Nimalizie kwa kukumbusha tu kwamba hata Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amemhutubu moja kwa moja Magufuli katika barua yake ya kuipongeza Tanzania kwa kumaliza uchaguzi salama kuwa achukue hatua ya kuhakikisha matakwa ya Wazanzibari walio wengi yanaheshimiwa. Kwa hivyo na mimi namwomba tena JPM, kuwa badala ya kuvamia wizara au taasisi nyengine ya umma alishughulikie kwanza jukumu hilo muhimu zaidi alilonalo kama Rais wa Tanzania.

Makala ya Abdulfattah Mussa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.