ZIMESALIA siku 11 kuanzia leo (Oktoba 14) hadi Oktoba 25, siku ya siku, Watanzania watapopiga kura kwa mara ya tano tangu urejelewe mfumo wa vyama vingi vya siasa 1992 na uchaguzi wa mwanzo uliofanywa chini ya mfumo huo 1995. Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni wenye kusisimua zaidi ya chaguzi zote nne zilizopita.

Katika medani ya siasa siku 11 ni siku nyingi mno. Mengi yanaweza yakatokea katika kipindi hicho. Na yakitokea yanaweza yakayapangua yaliyopangwa au yakauparaganya mkondo wa mambo uendavyo.
Hali kadhalika, pana uwezekano pasizuke jambo lolote kubwa la kushitua na uchaguzi ukaendelea kama ulivyopangwa. Sidhani kama katika kipindi hiki kuna wengi wataobadili msimamo wa nani watayempigia kura awe rais, mbunge, mwakilishi (kwa Zanzibar) au diwani. Kwa sasa walioamua wamekwishaamua, ni wachache sana wataobadili uamuzi wao ifikapo Oktoba 25.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Jumla ya Watanzania milioni 24 wamesajiliwa kupiga kura na inatazamiwa kwamba mwaka huu idadi ya watu wataotumia haki yao hiyo ya kidemokrasia itakuwa kubwa kushinda waliopiga kura katika chaguzi zilizopita. Hilo ni tokeo moja la msisimko wa uchaguzi huu.
Katika uchaguzi wa 1995, watu milioni sita na laki nane walipiga kura; idadi iliongezeka na kuwa watu milioni nane na laki tano mwaka 2000; ikaongezeka zaidi na kuwa milioni kumi na moja na laki nane mwaka 2005; na ilianguka 2010 na kuwa milioni nane na laki sita, ikiwa laki moja tu zaidi ya idadi ya waliopiga kura 2000.
Takwimu hiyo ilikuwa ishara kwamba tukiiacha Zanzibar, ambako takriban asilimia 90 ya waliosajiliwa kupiga kura walipiga kura katika chaguzi zote, siasa za Tanzania, kwa jumla, zilikuwa zimepwaya.
Labda wengi wa wapigakura wa Bara hawakuingiwa na raghba ya kupiga kura kwa vile wakihisi kwamba Rais Jakaya Kikwete atashinda tu uchaguzi. Na kushinda alishinda, ingawa kura alizopata zilipungua sana zikilinganishwa na alizopata alipochaguliwa mara ya kwanza 2000.
Pengine kuna na wengine waliotafakari wakaona kwamba upinzani uliogawika, wa vyama vilivyokuwa vikishindana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wakati huo huo vikishindana vyenyewe kwa vyenyewe, haukuwa na uwezo wa kuking’oa CCM kutoka kwenye madaraka.
Safari hii mambo ni tofauti kabisa. CCM ina mgombea mpya wa urais Dk. John Magufuli aliyepatikana kwa njia zenye kutatanisha. Namna Magufuli alivyoibuka kuwa mgombea kumewaudhi baadhi ya vigogo na kuwasababisha wakipige pande chama chao na wahamie upinzani.
Hawakwenda kwenye vyama vilivyo dhaifu lakini wamekimbilia kule wanakoamini kuwa watakuwa na nguvu za kuitikisa na kuiangusha CCM. Wamekimbilia kwenye Chama cha Demokrasiana Maendeleo (Chadema) kilicho chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wenye kukiunganisha chama hicho na vingine vitatu vya upinzani. Navyo ni Chama cha Wananchi au Civic United Front (CUF), National Convention for Construction and Reform-Mageuzi (NCCR-Mageuzi) na National League for Democracy (NLD).
Huko ndiko walikokwenda mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Frederick Sumaye, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Lawrence Masha, naibu waziri wa kazi na ajira Makongoro Mahanga pamoja na wabunge wawili wa zamani Ester Amos Bulaya na James Lembeli.
Hao si peke yao. Kuna vigogo wengine wa CCM katika ngazi za wilaya pamoja na wanachama wengi wa chama hicho ambao nao pia wamehamia Chadema.
Wengine, kama Kingunge Ngombale-Mwiru, aliyekuwa na kadi nambari nane ya CCM, wamejitoa kutoka chama hicho ingawa Kingunge hajajiunga na chama chochote kingine. Hata hivyo, amekuwa akimpigia debe Lowassa, aliyekipata Chadema alichonyimwa na CCM, yaani kuwa mgombea wa urais. Mgombea mwenza wake ni Juma Duni Haji, gwiji wa siasa kutoka Zanzibar mwenye kuwavutia wengi anapopanda jukwaani.
Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vitatu vingine vinavyoshirikiana na Chadema katika Ukawa, anampa taabu kubwa sana Magufuli. Mchuano kati yao ni mkali na, kwa mara ya kwanza katika historia ya chaguzi za Tanzania, hakuna uhakika kama mgombea urais wa CCM ataweza kushinda, hasa anavyokabiliwa na wimbi kubwa la wananchi wenye kutaka mabadiliko ya chama kinachoiongoza serikali.
Kuteuliwa Lowassa awe mgombea urais wa Chadema kumesababisha Ukawa nao ukimbiwe na vigogo wawili wa upinzani, Dk. Wilbrod Slaa, aliyejiuzulu ukatibu mkuu wa Chadema na kukihama chama hicho, na Profesa Ibrahim Lipumba, aliyejiuzulu uenyekiti wa CUF. Hata hivyo, hatua hizo za Slaa na Lipumba hazionyeshi kama zimeuathiri hivyo Umoja wa Ukawa zikilinganishwa na jinsi Lowassa alivyoipasua na kuijeruhi CCM.
Hata zile tuhuma za ufisadi anazotuhumiwa Lowassa na CCM, siku nenda siku rudi, hazielekei kama zimemuumiza mtuhumiwa. Bado maelfu ya watu wanavutiwa naye na wanafurika katika mikutano yake ya kampeni, ishara kwamba wanazipuuza shutuma za ufisadi.
Kwa mujibu wa ripoti moja iliyotolewa na Umoja wa Mataifa karibuni suala la ufisadi haliwashughulishi sana wapigakura wa Tanzania. Asilimia 59 walilitaja suala la afya kwamba ndilo suala kubwa linalowashughulisha likifuatiwa na maji safi (46%), elimu (44%), umasikini (34%), miundombinu (32%) na halafu ndio linakuja suala la ufisadi (28%).
Masuala mingine yaliyotajwa nikukosekana usalama au kuzuka machafuko ya kisiasa (13%), ukosefu wa ajira (11%), upungufu wa chakula/ukame (9%) na kilimo (5%).
Fedha chungu nzima zimemwagwa kusaidia kufanikisha shughuli za uchaguzi ujao kwa sababu uchaguzi huo unazingatiwa kuwa ni mchakato muhimu wa kuistawisha demokrasia Tanzania. Umoja wa Mataifa pekee umetoa dola za Marekani zisizopungua milioni 30. Lengo ni kuziwezesha taasisi zinazohusika, kama kwa mfano Tume za Uchaguzi, mahakama, ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Siasa, zitekeleze majukumu yao na pia kusaidia kufanya mageuzi ya kisheria yatayoimarisha utekelezwaji wa majukumu hayo.
Vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari, ni miongoni mwa wadau wengine waliosaidiwa ili nao waweze kuyakuza na kuyastawisha mazingira ya kidemokrasia nchini.
Msaada mwingine uliotolewa ni kuyawezesha makundi maalum kama ya wanawake, vijana na ya walemavu yashiriki kikamilifu katika uchaguzi na katika shughuli za kisiasa, kwa jumla.
Kadhalika, jitihada zimefanywa kusaidia kulikinga taifa lisitumbukie katika machafuko na fujo kutokana na mabishano yatayoweza kuzushwa na uchaguzi.
Uwezekano wa kuzuka vurugu na matumizi ya nguvu ni mkubwa hasa wakati wa kutangazwa, na baada ya kutangazwa, matokeo ya uchaguzi. Kwa hivyo, ni muhimu vyombo vinavyohusika visicheleweshe matokeo ya uchaguzi kujulikana na viwe vinaendesha shughuli zao kwa njia za uwazi.
Polisi na vyombo vingine vya usalama vina dhima kubwa ya kuhakikisha kwamba havitumiwi na serikali iliyopo madarakani kukipendelea chama chake kwa kuwabughudhi na kuwaonea wapinzani. Kwa upande wao, wapinzani nao wana jukumu la kuyakubali matokeo ikiwa yatakipa ushindi chama kinachotawala, ilimradi uchaguzi uonekane kuwa ulifanywa kwa haki, kwa uwazi na bila ya mapendeleo. Pande zote, serikali na upinzani, hazina haki ya kulazimisha ushindi.
Safari hii matokeo, si ya urais tu bali hata ya uchaguzi wa wabunge, wawakilishi (kwa Zanzibar) na wa madiwani, hayatabiriki. Kuna mengi yaliyobadilika tangu vyama vinne vikuu vya upinzani vikubaliane kushirikiana chini ya Ukawa.Waliokuwa wakisema kwamba Ukawa hautokuwa wamekosea.
Umoja huo haukusambaratika ijapokuwa umekabiliwa na changamoto nyingi, zikiwa pamoja na njama za CCM za kuwafitinisha viongozi wa Umoja huo na za kujaribu kuwatumia mchwa waule ndani kwa ndani. Mpaka sasa Umoja huo umesimama imara na haielekei kwamba utaweza kuporomoka katika siku hizi chache zilizobaki kabla ya uchaguzi.
Si siri tena, kwa mfano, kwamba viongozi wa CCM wamelemewa na wanaiona hali kuwa ni ngumu, hususan huko Zanzibar ambako katika chaguzi zilizopita chama cha CUF kimekuwa kikilalamika kwamba kilikuwa kikipokonywa ushindi katika matokeo ya urais. Safari hii, kutokana na mambo mbalimbali, ikiwa pamoja na mshikamano wa Ukawa, hali imezidi kuwa nzito kwa CCM.

Kwa mujibu wa habari tunazopashwa kutoka ndani ya makao makuu ya CCM-Zanzibar viongozi wa hapo wanaiona hali kuwa inazidi kuwa si nzuri kwao hata kidogo. Tunasikia kwamba watu wenye asili ya Bara wanaoishi sehemu za mashamba wameingiwa na woga.
Wanasema wanaendewa usiku mashambani na kutishwa na viongozi wa CCM kuwa yeyote anayetuhumiwa kuwa hakiungi mkono chama hicho atanyang’anywa kadi ya kupiga kura na atarudishwa Bara. Wanatishwa hivyo kwa sababu, kinyume na ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita, hivi sasa wanashukiwa kuwa miongoni mwao kuna waliogeuka na kukiacha mkono CCM wakiwa wanamuunga mkono Lowassa na Ukawa.
Hiyo ni tathmini ya mkutano wa siri uliofanywa wiki iliyopita wa viongozi wa chama hicho ambao haukuhudhuriwa na naibu mwenyekiti wa CCM, Rais Ali Mohamed Shein, aliyekuwa ziarani Pemba. Kwa mara ya mwanzo lakini mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa wilaya. Kwa kawaida, wao huwa hawaalikwi katika mikutano kama hiyo.
Katika mkutano huo ndipo ilipozidi kudhihirika kwamba hali ndani ya chama imebadilika baada ya kutambulikana kuwa majina yaliyofutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) yalikuwa ni ya wale “waliopitishwa kwa milango ya nyuma”.
Inasemekana kuwa kuna waliojiandikisha mara mbilimbili na wengine mara tatu tatu. Wengi walikuwa wafuasi wa CCM na wengi ni wenye asili ya Bara. Takwimu zilipoangaliwa kwa makini zilionesha kwamba pengo baina yao na CUF litakuwa kubwa sana. Hatari iliyopo ni kwamba itakuwa taabu kuiba kura na ili kuzuia matokeo mabaya kwa CCM lazima lipite jambo la kuparaganywa kila kitu.
Iwapo CCM itashindwa katika uchaguzi, tatizo litalowakabili viongozi wake wa Zanzibar ni namna ya kuwatuliza wafuasi wao waliofanywa waamini, na wanaoamini, kwamba ushindi ni wao.

TANBIHI: Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 14 Oktoba 2015.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.