Wiki mbili zilizopita nilikuwa Arusha kwa miezi takriban miwili nikifanya yangu. Moja katika siku zilizokuwepo huko, nilibahatika kukutana na kuzungumza na mtembeza watalii katika Mlima Kilimanjaro, niliyemuhoji mambo mengi nikitaka kujua hili na lile kuhusu kazi yake hiyo.

Katika maelezo yake, alinieleza kuwa suali maarufu ambalo amekuwa akikumbana nalo kutoka kwa watalii hao ni: “Kwanini nchi yenu ni masikini wakati zipo rasilimali nyingi?”na daima jibu lake huwa: “Tatizo ni uongozi wa nchi yetu ndio ambao umeshindwa kuzitumia rasilimali na kuifanya Tanzania kuwa tajiri”.

Swadakta! Nikampa heko kubwa, kwani kwa mawazo yangu anajibu suali ipasavyo. Kama ningekuwa nasahihisha masuali, basi nigempa alama zote, kwani yeye si miongoni mwa “waathirika na uongo wa Mwalimu Julius Nyerere” ambao amewaachia Watanzania.

Leo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakumbuka miaka 16 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, mmoja wa waasisi wawili wa taifa hili. Ombi langu kwao, ni kuwa wasikumbuke mazuri tu ya mtu wanayeamini kuwa “Baba wa Taifa” lao, bali wakumbuke pia hata ‘utumbo’ aliouwacha.

Hoja yangu ni kuwa kabla Mwalimu Nyerere hajaaga dunia, aliwaachia Watanzania uongo uliorikodiwa vyema na unaoenziwa na kunukuliwa na watu wengi kuanzia wanasiasa hadi watoto wadogo wa shule kiasi cha kwamba wako wanaoona kuwa ni ukweli mtupu na busara kuu ya kibinaadamu.

Wakati Watanzania wanaunukuu uongo huo kila uchao, wanasahau kuwa mwenyewe Nyerere aliusema kwa lengo tu la kukwepa lawama.

Kwa mfano, Nyerere aliposema: “Ujinga, maradhi na umaskini ndio maadui wa maendeleo”, alikuwa anakwepa lawama kwamba yeye akiwa kiongozi alishindwa kusimamia sera za maendeleo na badala yake kuamua kusingizia maradhi, ujinga na umasikini kuwa ni maadui. Kumbe ukweli wa mambo ni kuwa adui wa maendeleo ni uongozi mbovu aliouasisi.

Unaposema Tanzania haikupata maendeleo maendeleo kwa sababu ya umasikini, ujinga na maradhi, tafsiri yake pia ni kuwa Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete hawahusiki kabisa na tatizo la ukosefu wa maendeleo katika taifa hili, na badale yake anaeyehusika ni mbu wa malaria, mama masikini kule kijijini na mtoto aliyekosa kusoma.

Kusema kuwa maradhi ni adui wa mendeleo ni kutupia lawama zako kwa mbu na Virusi vya Ukimwi au hata kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini na wengi wao majumbani mwao.

Unaposema ujinga – kwa maana kuwa ukosefu wa elimu – ndiye adui wa maendeleo, tafsiri yake ni kuwalaumu vijana ambao wamekosa elimu pengine kwa kushindwa ada, ukosefu wa shule kwenye maeneo wanayoishi, au sababu nyengine yoyote iwayo.

Lakini tumlaumu nani kwa kijana aliyekosa elimu kwa sababu wazazi wake walishindwa kumlipia ada? Yeye au kiongozi wa nchi aliyeshindwa kuyafanya maisha ya raia kuwa mazuri?

Tumlaumu mama mgonjwa kitandani kwa malaria au tumlaumu anayeiongoza nchi kwa kushindwa kuleta madawa, kuboresha hudumu za afya na kushindwa kuwapa raia wake vyandarua vya kujikinga na mbu?

Hivi adui wa maendeleo ni maradhi au adui wa maendeleo ni viongozi wa nchi zetu ambao wameshindwa kuzitumia rasilimali za nchi kuwakwamua raia wao na umasikini?

Adui wa maendeleo ni kijana aliyekosa elimu au adui wa maendeleo ni kiongozi ambaye ameshindwa kutoa elimu bora kwa watu wake? Adui wa maendeleo ni umasikini au adui wa maendeleo ni kiongozi ambaye amewatia raia wake katika umasikini wa kutupwa hali ya kuwa nchi ina rasilimali nyingi tu za kuifanya nchi inawirike?

Huo ndio uongo ambao Nyerere aliwaachia watu, na ni uongo ambao unanukuliwa na wanasiasa wote wa chama tawala na upinzani. Sasa ukilaumu maradhi na umasikini tu, unamfanya hata Kikwete anayeondoka madarakani kutolaumika kwa umasikini wa Watanzania anaowaacha. Badala yake ya kulaumiwa ni malaria, Ukimwi, kaswende, vidonda vya tumbo, kichocho, minyoo, pepopunda, kifua kikuu na kadhalika. Hayo ndiyo mambo yanayoifanya Tanzania isiendelee.

Unamuacha kiongozi anayepewa misaada kutoka nje, anayepokea mikopo na kisha akasamehewa madeni hayo kwa ajili ya nchi na watu wake. Unamuacha kiongozi ambaye raia wake wanalipa kodi katika nchi yake iliyojaa kila aina ya rasilimali aporonyoke lawama za kutokuwa kweli kiongozi na unamkimbilia kijana aliyekosa elimu na ukosefu wake wa elimu unamwambia ndio sababu ya kukosa maendeleo.

Mwaka uliopita nilitengeneza makala ya redio juu ya watoto wanaojishugulisha na biashara ndogo ndogo katika manispaa ya mji wa Morogoro, na moja ya eneo tulilokwenda kukutana na watoto hao ni katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, Msanvu.

Ukweli wa mambo ni kuwa kila mtoto tuliyemuuliza kwanini ameacha shule kuuza vitumbua, jawabu yake ilikuwa sawa na ya mwenzake: nyumbani ni masikini sana na hakuna ada. Wakati mwengine mtoto anaishi na bibi yake au mama yake tu, hivyo yambidi auze machungwa ili amsaidie mzazi wake huyo.

Matokeo yake, kesi za watoto wa miaka 10 hadi 14 kuacha shule kwa tatizo la umasikini zipo nyingi. Kwa mapokezi ya Nyerere, sisi tunapaswa kumlaumu huyu mtoto masikini na sio kiongozi wetu wa nchi ambaye yeye na serikali yake wameshindwa kutumia rasilimali za nchi kumsadiia mtoto huyu. Tumuache kama alivyo hata kama serikali yake imeshidwa kuliondoa tatizo la umasikini.

Adui wa maendeleo si umasikini, bali ni kiongozi aliyeshindwa kuuondoa umasikini. Ndio maana ningemshangaa sana yule rafiki yangu mtembeza watalii kama angelijibu kuwa maradhi, ujinga, na umasikini ndio adui wa maendeleo yetu.

Wakati tukimkumbuka Nyerere, tuyakumbuke maneno ya uongo kama haya aliyotuambia, ambayo hakuyasema kwa bahati mbaya, bali kwa dhamira ya ‘kuwapoteza maboya’ Watanzania ili wasimtambue adui hasa wa maendeleo yao.

Kumbe adui wa maendeleo alikuwa Nyerere mwenyewe na uongozi wake mbovu ulioanza kutengeneza mafisadi, walarushwa, wizi walioila nchi nzima nzima na wanaoendelea kuimeza kavu kavu.

Umasikini ni janga linalosababishwa na kushindwa kwa uongozi wa nchi husika kujenga uchumi imara na kuzalisha kwa wingi, kwa hivyo adui wa maendeleo ya watu si umasikini wao, bali ni kiongozi wao waliyemkabidhi dhamana ya kuwaongoza lakini akashindwa kuwaongoza kuujenga uchumi imara kwa ajili ya raia hao.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Rashid Abdullah kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.