NITAANZA makala yangu ya wiki hii kwa kurejea swali nililoliuliza mwishoni mwa ile ya wiki iliyopita:Je, nakisi ya usafi na kithiri ya ufisadi ni kutokana na nafsi au nafasi? Mtu aliye “msafi” akijikuta katika nafasi inayompa fursa za kuwa fisadi na nafsi yake isimsute, atabaki kuwa msafi au atageuka na kuwa fisadi? Na je, mtu mwenye nafsi ya ufisadi akijikuta katika nafasi isiyomwachia mwanya wa kutenda ufisadi ataendeleza ufisadi wake? Au atabadilishwa na hali halisi ya nafasi anamojikuta ambamo nafsi yake ya kifisadi inafifishwa na nafasi yake mpya?


Swali hili nimeliuliza katika jitihada za kubainisha jinsi tunavyodanganyika kwa kuangalia alama za juu juu wakati tunapotakiwa kufanya uamuzi uliosimama juu ya misingi ya uchambuzi na haki. Ninajua kwamba imezoeleweka kwamba, katika siasa, muonekano ndiyo hali halisia (perception is reality), lakini hatuna budi kufanya tahadhari ya kuwaachia uhalisia huo watu wasiojisumbua kufikiri sana katika masuala yanayohusu mustakabali wao.

 

Na Jenerali Ulimwengu
Na Jenerali Ulimwengu

Muonekano tuliojengewa na watawala juu ya kampeni zinaozendelea hivi sasa ni kwamba “mafisadi wameondoka CCM, kwa hiyo mambo ni mazuri.’ Sasa huo muonekano unaweza kuwa na hali ya uhalisia kwa wale wanaotaka mambo yawe hivyo. Isitoshe, kwa CCM, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisakamwa na Watanzania kuhusu ufisadi, hii imekuwa ni hirizi itakayowaepushia balaa.
Wanaivaa hirizi hii kwa tambo, na wanataka kuwaaminisha watu wote kwamba hirizi hii inaweza kupunga mapepo yao yote. Kwa maneno mengine, wanataka watu waamini kwamba Edward Lowassa, mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, ndiye fisadi mkubwa kuliko wote nchini, na akiisha kuondoka CCM, chama hicho kinakuwa safi kama theluji. Huu ni uongo.
Ni uongo, si kwa sababau ninayo nia ya kumtetea au kumsafisha Lowassa. Mimi si mahakama ya kumhukumu, na wala mahakama ya aina yoyote haijawahi kufanya kazi ya kumhukumu, na hili amelisema mwenyewe mara kadhaa.
Suala la mahakama linachukua umuhimu mahsusi katika kipindi hiki kwa sababu moja nzito. Mawaziri wawili wa zamani wamekuwa mahakamani kwa muda mrefu, na hatimaye wamehukumiwa kifungo, na wako gerezani hivi sasa. Mashitaka yao yalihusu hasara waliyoisababishia serikali kwa uamuzi waliofanya wakiwa watumishi wa serikali hiyo.
Shutuma zinazoelekezwa kwa Lowassa zinahusu kuisabababishia serikali hasara kwa uamuzi aliofanya akiwa waziri mkuu. Ni nini tofauti kati ya makosa ya wale mawaziri wawili na makosa anayoshutumiwa nayo Lowassa? Kama hakuna tofauti baina makosa ya wote hawa, ni kwa nini, basi, wale wawili walishitakiwa na wakafungwa, na Lowassa hajashitakiwa ili akipatikana na hatia afungwe naye?
Je, ni kwa sababu hasara aliyosababisha kwa uamuzi wake haikuwa kubwa kama ile waliyosababisha wale mawaziri wawili? Au ni kwa sababu ushahidi wa makosa ya Lowassa haukupatikana au, kama ulipatikana, ulionekana haungekuwa na nguvu ya kutosha mbele ya uchunguzi wa kimahakama?
Au hao mawaziri wawili walio jela walionewa, na kilichowafanya washitakiwe ni kingine na wala si hicho kilichodaiwa mahakamani? Au kuna/kulikuwa na woga kwamba Lowassa angefikishwa mahakamani, utetezi wake ungewahusisha wengine ambao hawataki kuhusishwa na Richmond?
Inakuwa vigumu kwa yeyote anayefuatilia mienendo ya mifumo ya utoaji haki kuona makosa yanayofanana yakishughulikiwa kwa njia zinazotofautiana. Hiyo nayo ni dalili ya ufisadi, kwa sababu kwa kufanya hivyo, watawala wanaweza kumuadhibu wanayetaka kumwadhibu na kumsamehe wanayetaka kumsamehe, bila kufuata misingi ya haki.
Ni kwa nini serikali ya CCM imeshindwa kumshitaki Lowassa, lakini leo hii CCM iko msitari wa mbele kumsema Lowassa kama fisadi. Kama kweli hiyo ndiyo njia ya kuwashughulikia mafisadi, ni kwa nini hawakuwaachia wale mawaziri wawili walio jela, wasiwashitaki, na kisha wakawafuatilia katika kampeni zao na kuwazomea kama mafisadi? Si ndicho kilichofanyika kwa Lowassa?
Nasema tena kwamba sina nia ya kumtetea wala kumsafisha Lowassa, na bila shaka anayo matatizo yake, kama mimi na wewe tulivyo na matatizo yetu kibao! Ninachosema ni kwamba tuache kusema uongo kwa lengo la kuwaumiza watu tusiowapenda au tusiowataka kwa hili au lile.
Hili limesemwa lakini linahitaji kusemwa tena: Ikiwa kuondoka kwa Lowassa ndiko kunaifanya CCM iwe safi kiasi kwamba mgombea wake, Magufuli ananadiwa kama “muadilifu,” je kashfa zote zilizoikumba CCM wakati Lowassa hayumo serikalini tena zilikuwa zake pia? Ikiwa hivyo, Lowassa anazo nguvu za ajabu za kuweza kuendesha mambo serikalini akiwa alikwisha kuondoka kitambo?
Tangu Lowassa aondoke serikalini tumekuwa na kashfa kadhaa ambazo sote tunazijua, na ni hizi kashfa zilizomlazimisha Rais Jakaya Kiwete kubadilisha baraza la mawaziri kila ilipotokea kashfa (Rais Kikwete hajawahi kubadilisha baraza kutokana na utendaji mbovu au dhaifu; amebadilisha mara kadhaa kutokana na mashinikizo ya Bunge tu)
Kashfa zote hizi, hadi hii ya mwisho kabisa ya Escrow, haikumhusu Lowassa, lakini tunaambiwa kuondoka kwa Lowassa kuna maana ufisadi umeondoka CCM! Ndiyo maana nikaanza na ule msemo wa “Mnyonge mnyongeni, na haki yake mpeni.”
Ni muhimu kuwa wakweli na kujali kutendeana haki. Lowassa ameifanyia kazi serikali ya CCM, na hakuna ubishi kwamba serikali hiyo imejaa ufisadi. Lowassa na mimi tulikuwa pamoja bungeni wakati nilipoamua kuleta bungeni hoja kuhusu maadili ya viongozi, naye akiwa waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu John Malecela, hakuitaka wala Malecela mwenyewe na wakuu wengine wa serikali. Ilipitishwa kwa nguvu za lile kundi lililokuja kujulikana kama “G-55”.
Tangu sheria iliyotokana na hoja yangu kuandikwa na kupitishwa na Bunge, kila aina ya hila zimefanywa ili sheria hiyo isiwe na nguvu yoyote. Wakuu wa serikali hao wamekuwa msitari wa mbele kujilimbikizia mali “kama hawana akili nzuri.”
Alipoingia madarakani, Rais Benjamin Mkapa alitoa tamko la matumaini pale alipotangaza mali zake zote. Alipoondoka baada ya miaka 10 akawa kimya, utadhani si yule yule tuliyemsikia miaka kumi kabla. Isitoshe, tukaja kugundua kwamba katika kipindi hicho alikuwa kaigeuza Ikulu kuwa anwani ya kampuni yake na kwamba alikwisha kujitwalia mgodi mzima, mali ya serikali.
Mwanzoni mwa utawala wake, Mkapa aliunda tume ya kuchunguza rushwa nchini, na akamteua Joseph Warioba kuiongoza. Kama kawaida yake, Warioba na timu yake wakafanya kazi nzuri mno, lakini kama mazoea ya watawala wanaopenda kumtumia Warioba (naye anavyokubali kutumiwa bila kinyongo) matokeo yake yamebaki ni karatasi za kufungia maandazi sokoni. Ufisadi umezidi kuongezeka serikalini kwa kiasi kisicho mfano.
Lakini mfano mmoja mkubwa unaweza kutuonyesha ni vipi watawala wetu wanafikiri juu ya ufisadi na bidhaa zitokanazo na ufisadi. Katika hatua iliyowashangaza wengi, serikali ya Mkapa iliamua “kuuza” nyumba za serikali miongoni mwa watumishi waliokuwa wakiishi ndani yake. Huko hakukuwa “kuuza” bali ilikuwa ni kugawana kwa wale “waliobahatika”.
Ni kugawana, na wala si kuuza, kwa sababu thamani ya viwanja vya nyumba hizo kwa wajuao thamani, ni mabilioni ya shilingi kwa kila moja, lakini waliogawiwa nyumba hizo walilipa hadi shilingi milioni thelathini, tena baada ya nyumba zenyewe kukarabatiwa kwa mamia ya mamilioni!
Uamuzi huo wa kihuni ulifanyika chini ya urais wa Mkapa, na waziri aliyesimamia zoezi zima alikuwa ni John Pombe Magufuli. Kama huu si wizi, ni kitu gani? Ni ujasiri gani huu unaowafanya wakuu wa serikali waiibie serikali yao wenyewe? Nakumbuka Dk. Harrisona Mwakyembe akisoma hotuba yake bungeni kuhusu “kashfa ya Richmond” mwaka 2008, na akatumia maneno “ujasiri wa kifisadi”. Nadhani maneno hayo yangefaa zaidi kuelezea wizi wa nyumba za serikali.
Nasema hivyo kwa sababu, kama Lowassa kweli alilipwa kwa ajili ya Richmond, fedha hizo atakuwa alizificha katika benki, hapa nchini ama nje. Lakini hakuna njia ya kuweza kuficha nyumba 400 zilizoko Oyster Bay, Isamilo na Raska Zone na “Uzunguni” katika miji yetu yote.
Nyumba hazihamishiki, hazifichiki. Mtu hawezi akaibeba nyumba aliyoipata kwa njia haramu akampelekea shangazi yake amwekee hadi hapo msako wa polisi utakapoisha. Nyumba ipo pale pale; ubomoaji unaofanywa na wale waliouziwa (kwa bei ya kweli sasa) unaonekana wazi; ujenzi wa majumba makubwa ya biashara unafanyika mchana kweupe.
Hapa ndipo unaonekana “ujasiri wa kifisadi” alioutaja Mwakyembe kuhusu kesi ya Richmond. Maana yake ni kwamba watu wameamua kufanya jambo lao, wanajua wananchi watajua, lakini hawajali. Kwani wananchi watafanya nini?
Hiyo ndiyo hali ya ufisadi aliyoisimamia Magufuli chini ya serikali ya CCM. Haishangazi sana kwamba katika kampeni hataki kujitambulisha kama mgombea wa CCM. Anayajua ‘madudu’ ya CCM kwani ameyashiriki. Kwa sababu hii, Magufuli amekuwa ni mgombea wa Magufuli.
Lakini kwa wale tunaotaka kufikiri angalau kidogo, hata kama ni hatari kufanya hivyo, usafi wa Magufuli na ufisadi wa Lowassa ni kitendawili kinachosubiri kuteguliwa.

 

TANBIHI: Makala hii ya Jenerali Ulimwengu imechapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 14 Oktoba 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.