Afrika yasonga mbele. Hilo halina shaka. Tafiti kadhaa za mashirika makubwa ya kimataifa zinaonesha kuwa Afrika inasogea kwa kasi kwenye ukuwaji wa kiuchumi na vijana wake wanazidi kugundua fursa za kujituma na kutumia nishati na akili zao kuleta mabadiliko kwa jamii na bara lao.

Lakini kuna hadithi nyengine pia. Ukuwaji wa uchumi na upanukaji wa fursa hizo hauendani na kiwango cha ushiriki wa wananchi kwenye masuala yanayohusu hatima yao. Haulingani na namna serikali zinavyowatawala wananchi hao. Haulingani na heshima kwa haki za binaadamu. Mambo ambayo kwa pamoja tutayaita “Utawala wa Sheria.”

Ndivyo inavyobainisha Faharasa ya Ibrahim juu ya Utawala Barani Afrika (AIIG) ya mwaka 2015, ambayo ilichapishwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Oktoba jijini London na Wakfu wa Mo Ibrahim unaojihusisha na utawala bora barani Afrika. Kwa kauli nyepesi na rahisi, unasema wakfu huo, “utawala bora barani Afrika umedumaa”.

Maoni Mbele ya Meza ya Duara katika Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle  inajaribu kusaka jawabu ya swali moja kuu – je, kwa nini uwiano huo haupo? Kwa nini matumaini ya Afrika kusonga mbele yawe yanatamaushwa na kutoimarika kwake kwenye uongozi bora na utawala wa sheria? Je, katika kuelekea ukuwaji wa kiuchumi, haki za binaadamu, ushiriki wa wananchi, uhuru wa kuamua na kuchagua vina nafasi gani hasa?

Ungana nami nikiongoza mjadala unaohudhuriwa na Dk. Foum Kimara akiwa Zanzibar, Prof. Kingo Mchombu wa Chuo Kikuu cha Windhoeck, Namibia, na mtaalamu wa uchumi, Abdulrahman Mohammed akiwa London, Uingereza.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.