JUMAMOSI iliyopita, Edward Lowassa, aliwakuna Wazanzibari. Akiuhutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Mnazi Moja, Unguja, Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Tanzania wa Chama cha Maendeleo (Chadema), anayeungwa mkono na vyama vitatu vingine vya upinzani, alitangaza kinaga ubaga kwamba yeye ni muumini wa muundo wa Muungano wa Serikali tatu utaoirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili.
Ahadi hiyo ya Zanzibar kurejeshewa mamlaka kamili imekwishawahi kutolewa mara kadha wa kadha na Maalim Seif Sharif Hamadi, Katibu Mkuu wa CUF, anayeugombea urais wa Zanzibar kwa niaba ya chama chake na anayeungwa mkono pia na vyama vitatu vingine vya upinzani.
Ahadi ya kurejeshewa mamlaka kamili imekuwa kama simaku inayowavutia maelfu kwa maelfu ya Wazanzibari wakiunge mkono chama cha CUF. Hata baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na baadhi ya viongozi wao wanaiunga mkono dhana hiyo, ingawa wanafanya hivyo kisirisiri kwa vile inapingana na sera ya chama chao.

 

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Raja

Kwa kuiunga mkono dhana hiyo, hadharani na bila ya woga, makada wawili wakuu wa CCM, Hassan Nassor Moyo na Mansour Yusuf Himidi, walibidi watimuliwe kutoka chama hicho. Mansour, ambaye baadaye alijiunga na CUF na sasa ni mshauri wa katibu mkuu wa chama hicho, anawania uwakilishi wa jimbo la Chukwani.
Watetezi wa “mamlaka kamili” ya Zanzibar wamekuwa wakihoji kwamba dhana hiyo inaungwa mkono na wengi wa wananchi wa Zanzibar, kama alivyokiri Jaji Joseph Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba. Kwa mujibu wa Warioba, tume yake ilipofika Zanzibar iligundua kwamba asilimia 60 ya Wazanzibari waliotoa maoni yao kuhusu aina ya Katiba waitakayo walisema kwamba wanataka Muungano wa Mkataba wakidai kwamba muundo wa sasa wa Muungano wa serikali mbili hauwafai. Waliotaka muundo huo ubakie kama ulivyo walikuwa asilimia 30 ya waliotoa maoni yao.
Hoja kubwa ya wenye kudai mamlaka kamili ni kurejeshewa Zanzibar baadhi ya yale yaitwayo “mambo ya Muungano” yatayoweza kuisaida Zanzibar ijikwamue kiuchumi na iwe na uwezo wa kuusimamia uchumi visiwa hivyo. Wanataka Tanganyika nayo irejeshewe serikali yake itayoshughulikia mambo ya Tanganyika.
Wakisema kwamba wanataka Muungano wa Mkataba ina maana kwamba wanautaka Muungano isipokuwa uwe wa muundo mwingine, utakaozipa nchi mbili zilizo katika Muungano huu (Tanganyika na Zanzibar) haki sawa na mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yao ya kimsingi.
Inasikitisha kuwasikia baadhi ya viongozi wa chama kinachotawala wakiendelea na njama zao za kuwatisha wananchi kwa kutumia hoja zisizo za kweli. Mfano mmoja ulishuhudiwa Septemba 27 kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi ya CCM huko Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini, Unguja.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein, akiwa mgeni rasmi, uliwasikia viongozi wa CCM wakidai kwamba wenye kutaka mamlaka kamili wana dhamira ya kumrejesha Sultani aitawale Zanzibar kwa mlango wa nyuma.
Hiyo ni hoja nyingine ya kitoto, tena ya uongo, inayotolewa na viongozi hao kuwadanganya wapigakura. Ikiwa Muungano hautovunjika huyo sultani atarudi vipi? Na hata kama utavunjika wako wapi wenye kutaka kumrejesha sultani atawale? Mbona hatuwasikii?
Seyyid Jamshid bin Abdullah al Said, aliyekuwa mfalme wa mwisho kutawala Zanzibar, amekuwa akiishi Portsmouth, kusini mwa Uingereza tangu baada yakupinduliwa Januari 12, 1964. Hivi sasa ana umri wa miaka 86. Hajihusishi na siasa za Zanzibar wala hakuna vuguvugu lolote au chama chochote, ndani au nje ya Zanzibar, chenye kufanya harakati za kumrudisha ili atawale tena.
Kwa hakika, ombi pekee la kumtaka arudi kwao liliwahi kutolewa kwenye mkutano wa hadhara na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dr Salmin Amour. Naye Salmin alichosema ni kwamba kwa kuwa ni Mzanzibari ana haki ya kurudi na kuishi kwao lakini akiwa kama raia wa kawaida na si mfalme.
Miongoni mwa waliowadanganya wananchi kwenye mkutano wa Mkokotoni kuhusu mamlaka kamili na kurejeshwa kwa utawala wa kifalme walikuwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Shamsi Vuai, aliyewahi kuwa waziri kiongozi katika serikali ya Zanzibar ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Bila ya shaka, kina Balozi Seif wanamtumbukiza na Lowassa katika kundi hilo la wenye kutaka kumrejesha Jamshid, kwa vile naye amekwishaahidi kuwa endapo atachaguliwa Rais wa Tanzania ataifufua Katiba ya wananchi iliyopendekeza Muungano wa serikali tatu utaoipa Zanzibar mamlaka kamili.
Aliyeshangaza zaidi kwa uongo aliousema Mkokotoni alikuwa mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kaskazini, Unguja, Haji Juma Haji. Huyu alithubutu kuongeza kwamba alisikitishwa na “kauli za CUF zinazoelezwa katika mikutano yao kuwa Zanzibar itaongozwa na wale walioondoshwa 1964.”
Huo ni uzushi mtupu. Hakuna hata siku moja ambapo kiongozi yoyote wa CUF aliyewahi kusema maneno kama hayo. Sijui pamezidi nini hata kwamba hawa viongozi wetu wakawa hawawezi kuendesha siasa zao bila ya kusema uongo.Ukweli una nini hata wakawa wanaukimbia namna hivi?
Toka lini kudai Zanzibar irejeshewe mamlaka yake kamili iwe sawa na kutaka kumrejesha sultani atawale?
Viongozi hao wa CCM/Zanzibar wamesahau kwamba wakati wa Zanzibar ya Sheikh Abeid Amani Karume ilikuwa ni nchi iliyokuwa na mamlaka kamili, hata baada ya kuungana na Tanganyika Aprili, 1964.
Ilikuwa na uwezo wa kutosha wa kuushughulikia uchumi wake na ilikuwa na nguvu za kutosha za kuusimamia usalama wake. Karume alikuwa na jeshi lake ambalo mpaka Mwalimu Julius Nyerere likimtia woga.Wala Karume hakuhitaji sultani aliyempindua arudi. Unaweza kuhoji kwamba yeye mwenyewe Karume alikuwa na nguvu zaidi ya zile alizokuwa nazo Sultan Jamshid.
Balozi Seif na wenzake pengine wanatumai kwamba uzushi wao utaweza kuwavutia watu wa sehemu za mashamba, hasa za Kaskazini mwa Unguja. CCM imekwishatambua kwamba matusi hayafai katika sehemu za watu walio wahafidhina kama za Mkoa wa Kaskazini. Ndio maana wameamua kutumia mbinu nyingine, ya kutapakaza hii sumu ya kurudi kwa usultani.
Hiyo ni ishara kwamba CCM imetambua kwamba imeishiwa na nguvu katika Mkoa wa Kaskazini na kwa hivyo lazima ibadili mbinu za kuwavutia watu. Ndio viongozi wake wakaamua kutumia kisingizio cha uongo cha kurudi kwa utawala wa kifalme. Na kufanya hivyo ni hatari.
Ni hatari, kwa sababu, wanaposema kurudi kwa usultani wanataka watu watafsiri kuwa ni kurudi kwa Waarabu. Na wanawatisha kwa kuwaambia kwamba hao Waarabu walio nje ya nchi na waliopokonywa mashamba yao baada ya Mapinduzi watarudi kuyadai.
Huo ni mchezo mchafu. Ni jaribio la kuwatisha wakazi wa Kaskazini na kuwafanya wakipigie kura chama cha CCM na mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli.
Pamoja na mbinu ya matusi, inavyoonyesha ni kwamba sasa CCM imeshaanza kuitumia na hii mbinu mpya ya kitisho cha kurudi kwa sultani. Huo ndio mkakati wake mpya zikiwa zimebakia kama wiki tatu kabla ya kufika siku ya siku, Oktoba 25.
Kuna vitisho vya aina nyingine ambavyo hutolewa pia na akina Balozi Seif. Katika mkutano huo huo wa Mkokotoni alidai, bila ya kutoa ushahidi, kwamba chama cha CUF kinanunua vitambulisho vya kupigia kura kwa wana CCM. Kama kweli hayo yanatendeka kwa nini basi wenye kufanya uhalifu huo hawatiwi mbaroni na kufikishwa mahakamani?
Balozi aliendelea kutisha kwa kusema kwamba CCM inayajuwa mambo mengi ya CUF ya kutaka kufanya vurugu siku ya uchaguzi na siku mbili baada ya hapo. Na kama hayo ni kweli kwa nini wenye kupanga njama hizo wasichukuliwe hatua hivi sasa kabla hawajaivunja amani? Badala yake aliwatisha wazee wa Kaskazini kwa kuwaambia kwamba “vyombo vya dola havichezewi”, kwa hivyo, aliwataka wawaambie vijana wao wasifanye vurugu au maandamano.
La kutisha zaidi ni pale Balozi Seif aliposema kwamba “CCM haichokoleki iko imara na ukifanya mchezo itakushughulikia.” Hivi CCM, chama cha siasa, kina uwezo gani kisheria wa kujifanya polisi na kuwachukulia hatua wanaoshukiwa kuwa ni wavunjaji amani?
Matamshi kama hayo ya Balozi Seif ni yenye kutisha na ni ya hatari. Ni matamshi yenye kuchochea chuki. Hiyo chuki nayo, kwa upande wake, inaweza ikachochea utumizi wa nguvu dhidi ya wapinzani wa chama kinachotawala.
Katika mikutano ya kampeni za uchaguzi, wapigakura na wananchi, kwa jumla, wanataka kusikia kuhusu sera za vyama na sio vitisho wala uongo wa kitoto kama ule wa kwamba wenye kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar wanataka kumrejesha Sultan Jamshid. Hata Lowassa basi?

Chanzo: Raia Mwema, 7 Oktoba 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.