Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle inayorusha matangazo yake kutokea Bonn, Ujerumani, imekanusha vikali taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii nchini Tanzania kwamba imekuwa ikifanya utafiti wa maoni ya wananchi juu ya nani anayeongoza kuelekea uchaguzi mkuu unaofanyika tarehe 25 Oktoba.

Katika ujumbe wake chini ya kichwa cha habari “Tangazo Muhimu” iliyoutuma kupitia ukurasa wa Facebook hivi leo, Idhaa hiyo imesema imegundua “kuna ujumbe unaosambazwa kwa njia wa WhatsApp katika mitandao ya kijamii kwamba DW inakusanya maoni kuhusu wagombea wawili wakuu wa uchaguzi wa Tanzania, John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)… (lakini) tungependa kuwajulisha hatufanyi utafiti wowote wa maoni kuhusu wagombea.”

Hadi sasa ujumbe huo haujafahamika ulikoanzia, lakini wengi wa waliotuma maoni chini ya tangazo hilo la DW, wanasema wameushuhudia ujumbe huo ukisambazwa. Idhaa ya Kiswahili ya DW ni moja kati ya idhaa 30 za shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani ambayo imekuwa ikirusha matangazo yake kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Imekuwa ikiripoti changuzi zote zinazofanyika katika eneo lenye wasikilizaji wake, hasa Afrika Mashariki na Kati, lakini haijawahi kuwa sehemu ya mchakato wa uchaguzi wowote ule. Katika uchaguzi wa mara hii nchini Tanzania, imefungua ukurasa maalum kwenye mtandao wake: http://www.dw.com/sw/idhaa-ya-kiswahili/uchaguzi-mkuu-wa-tanzania-2015/s-101616 ambao unaripoti matukio mbalimbali yanayohusiana na uchaguzi huo.

 

One thought on “Deutsche Welle haikusanyi maoni uchaguzi wa Tanzania”

  1. Salaam, nikweli nami nimebahatika kuusoma, inashangaza kuona Dunia ya leo kuwa kuna campaign za uchochezi wa kila aina.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.