UCHAGUZI mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uchaguzi wa kumchagua Rais wa Zanzibar unaotarajiwa Oktoba 25 unakabiliwa na mtihani mgumu kutokana na kampeni chafu inayoendeshwa na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni Dk. Ali Mohamed Shein peke yake anayeeleza atawafanyia nini wananchi akichaguliwa tena akianzia na kutaja mafanikio ya serikali tangu 2010, na kutoa ahadi mpya nyingi na kubwa zisizotekelezeka.

Wasaidizi wake katika chama hawamsaidii bali wanaeneza uongo sana. Fikiria wanapotaja Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaohusisha Chama cha Wananchi (CUF) chenye nguvu kubwa Zanzibar na vyama vingine vitatu kuwa ni kundi la magaidi ambalo eti linatumia Jumuiya ya Uamsho kueneza ugaidi nchini.

Huku ni kukosa umakini na kuamua kwa makusudi kuchochea chuki za kidini Zanzibar ambako kilio kikubwa cha wananchi ni masheikh wao kutungiwa kesi ya ugaidi na kuwekwa jela Tanzania Bara bila ya kujulikana kikomo cha kadhia hiyo.

Ni fitna tosha dhidi ya kile walichokuwa wakikisema viongozi Uamsho kuwa Muungano unainyima haki Zanzibar ya kujitawala na kujiamulia mambo yake.

Kitendo cha Zanzibar kuingiliwa uhuru wake CCM na Serikali ya Muungano (SMT) ambayo imehodhi sio tu nguvu zote za dola bali pia za kiuchumi kupitia Benki Kuu (BOT) iliyo na mamlaka ya kusimamia na kuidhamini Zanzibar iweze kupata mikopo ya nje, kinazidi kuthibitisha udhaifu wa viongozi wa CCM.

Si hilo tu lakini Zanzibar haiwezi kujitegemea chini ya muundo wa Muungano uliopo wa serikali mbili na kuwepo ulazima kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikitaka isitake ifuate Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ambayo imehodhi mamlaka ya mambo yote ya ulinzi na usalama na kwamba Rais wa Zanzibar si amiri Jeshi mkuu, hana mamlaka ya kikatiba ya kuamuru vyombo vya dola kwa lolote lile.

Na kwa sababu hiyo, hana uwezo wa moja kwa moja wa kuamuru Jeshi liwe la Polisi au la Ulinzi (JWTZ), lazima apewe idhini ya kufanya hivyo na mamlaka iliyo juu yake – Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Ni uongo usio na kificho kuwaeleza wananchi kuwa Zanzibar ina mamlaka kamili ya kidola na vikosi vyake havitasita kuchukuwa hatua kudhibiti vitendo vya kigaidi view vinafanywa na masheikh au na watu wengineo.

Kwamba hakuna atakaeachwa, atashikwa hata akiwa ni mfuasi wa chama gani, ni kauli za vitisho zinazochapuzwa na uongo wa kujikweza katika majukwaa ya kampeni ambayo wagombea hasa wa CCM wanaona ni sawa tu kutumia misamiati ya kushabikia kuwepo ugaidi, pasina kutafakari athari za propaganda za aina hiyo.

Ugaidi si suala la mzaha bali ukatili na unyama usioendana na heshima na utu wa binaadamu. Ugaidi ni ushenzi na uwendawazimu usioweza kuwa sera ya kuomba kura. Hakika makada wa CCM wanajenga watu chuki kwa malengo ya kufanikisha matakwa yao ya kisiasa.

Hawajali kuwa vitendo kama hivi ndivyo vinavyopandikiza mihemuko ya hisia ambayo katika wakati huu wa uchaguzi huweza kusababisha kuitumbukiza nchi katika mauaji mabaya ambayo kwingineko yameishia kuwasomokeza viongozi wa kisiasa, vyombo vya dola na waandishi wa habari Mahakama ya Makosa ya Uhalifu wa Binadamu (ICC) iliyoko The Hague, nchini Uholanzi.

Zanzibar tangu dahari ni nchi ya watu mchanganyiko wa makabila na dini, wanaoishi kwa upendo mkubwa na kusaidiana. Waislamu na Wakristu wamekuwa wakiishi kama ndugu miaka yote ya historia ya Zanzibar. Kuwachochea chuki leo ni hatari isiyovumilika.

Wanaotaka ugaidi waone mifano ya nchi zilizofikwa na uovu huo. Hebu waitazame Kenya inavyohaha kuimarisha ulinzi wa ndani na mipakani hasa kaskazini katika kukabiliana na kinachoitwa ugaidi.

Basi makada wa CCM wasaka uongozi, wanaposimama majukwaani na kujenga hoja ya ugaidi wakidhani ndio turufu ya kuweza kuchaguliwa, wajue wanaota uwendawazimu badala ya ustaarabu na uzalendo, na wala haitawasaidia ila hasara.

Mtu mwenye kufikiri vizuri anachokiona ni kushuhudia makada hao walivyofilisika kisiasa.

UKAWA kupitia viongozi wagombea urais wa Tanzania, Edward Lowassa, na mgombea urais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, wanachosimamia sio ugaidi isipokuwa kutumia akili kupambana na CCM kwa lengo la kutokomeza mifumo ya utawala mchovu na kujenga badala yake, utawala mpya utaokuza mifumo inayoimarisha haki, uadilifu na imani ya kuwaondolea shida Watanzania na Wanzanzibari.

Wanalenga kupunguza athari za umasikini kutoka walikokuwa kwenye ukiritimba wa CCM kujiona ni chama pekee chenye haki ya kutawala na kufanya watakavyo hata kama viongozi na makada wake hadi Jumuiya zake zinakosea.

Makada wa CCM kila leo wanawataja Lowassa na Maalim Seif kama ajenda ya mikutano yao ya kampeni. Kila siku midomoni mwa viongozi wakubwa wa CCM na makada wapandia meli iliyotoboka wakiwahusisha wagombea hao wa CUF na CHADEMA katika uvurugaji wa nchi kukosa muelekeo na kuwaacha mamilioni ya Watanzania na vilio vya unyonge, ulofa na hofu ya matumaini ya kurudisha malengo ya Azimio la Arusha ambalo limepigwa teke na watawala wa CCM na malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia manifesto ya Chama cha ASP yaliyozikwa kwa kukumbatia viongozi wabadhirifu, wapenda mali na wanaoabudu rushwa serikalini.

Zanzibar inanyonywa na wazawa wake wakibaguliwa na kuporwa ardhi waliyorithi na kuitumia kama rasilimali ya kuendeleza maisha yao. Kwa mgongo wa uwekezaji, wageni wamemilikishwa ardhi na kuwa kikwazo cha maendeleo ya Wazanzibari.

Ni kwa muktadha huo, UKAWA kupitia CUF na CHADEMA wamevaa njuga na kuhakikisha mfano uliopo wa serikali zote mbili za CCM, unabadilika na kutoa nafasi kwao kuanzisha mfumo unaokidhi matumaini mapya ya wananchi ya kujikomboa kutoka manyanyaso ya wageni wanaopora rasilimali za nchi na zaidi kuondoa kabisa ubaguzi wa kipato na uchumi na miongoni mwa Watanzania na Wazanzibari.

Kwa kasi yao kubwa na moyo wa kuzidi kujitoa mhanga, wanasiasa hawa wawili wenye historia ya ushupavu kiuongozi wakiwa serikialini na katika CCM kabla ya kufukuzwa kiaina, hakuna kurudi nyuma; dhamira ya mabadiliko itazidi kuimarika kupitia sera za UKAWA zinazolingania vuguvugu la kuondoa muundo wa serikali mbili na kuleta wa serikali tatu unaotarajiwa kutambua haki ya kila nchi – Zanzibar na Tanzania Bara – kuwa washirika wa Muungano usiokuwa na shaka ya nchi moja kuiburuza nchi nyingine.

Chanzo: Makala ya Enzi Talib kwenye gazeti la Mawio la tarehe 2 Oktoba 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.