NIMEKUWA nikiyasoma, tena na tena, makala ya Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), yaliyochapishwa Septemba 10 kwenye blogi la gazeti la The Hill la huko Washington, Marekani. Gazeti hilo si la kuchezewa wala kudharauliwa. Tangu liasisiwe 1994 limekuwa ni muhimu na lina uzito katika siasa za Marekani na, kwa kiwango fulani, za ulimwengu kwa jumla. Ni gazeti ambalo wanasiasa wa Marekani na wote wenye kuhusika na siasa lazima walisome. Wakati wa msimu wa Bunge la Marekani (Congress) linapokuwa linakutana gazeti hilo huchapishwa kila siku. Huchapishwa kwa karatasi na katika mtandao.

Ni gazeti linalosomwa na wabunge wa Marekani na linaloandika mambo mengi kuyahusu mabaraza yote mawili ya Bunge la nchi hiyo, yaani Baraza la Wawakilishi (House of Representatives) na Baraza la Senate (Senate). Taarifa nyingi za habari kuhusu Ikulu ya Marekani (White House), Bunge la Marekani na taasisi za kisiasa za Marekani huchapishwa kwanza katika jarida hilo pamoja na habari kutoka ofisi zenye kazi za kuwashawishi wabunge zilizo katika Barabara ya K, jijini Washington.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Hakuna popote duniani penye barabara yenye uzito wa kisiasa kama Barabara ya K ya Jiji la Washington. Huko ndiko kwenye ofisi nyingi zinazoajiriwa kuwapigia debe wanasiasa, sera fulani na hata nchi fulani au viongozi wao kwa lengo la kuwashawishi wabunge wa Marekani. The Hill linajigamba kwamba ni la aina ya pekee na hakuna anayeweza kulishinda katika kuchapisha habari madhubuti zisizopendelea upande wowote kuhusu namna Bunge la Marekani linavyofanya kazi. Linajigamba pia kwamba habari zote kuu kuhusu siasa za Marekani na biashara za nchi hiyo huanzia gazetini humo. Gazeti hilo na jukwaa lake la mtandaoni huwaunganisha wanasiasa, wachambuzi wa siasa na taasisi za siasa.

Kadhalika gazeti hilo ndilo linaloongoza ajenda ya kisiasa nchini Marekani. Ndilo lenye kuamua nini cha kujadiliwa na lina ushawishi mkubwa juu ya maoni ya wabunge kuhusu masuala mbalimbali. Kwa hivyo, Kinana alipoamua kuandika makala yake katika gazeti hilo alikuwa anawalenga wabunge wa Marekani na Rais wa Marekani akitambua wazi kwamba makala yake yatamfikia Rais Barack Obama mwenyewe moja kwa moja ayasome au yatamfikia kupitia wasaidizi wake na washauri wake kuhusu mambo ya Afrika. Makala hayo ya Kinana yanatisha. Tena yanakirihisha na yanaweza hata kukutapisha. Pia ni yenye kusikitisha.

Ninasema hivi kwa sababu Kinana amejisahau na amesahau kwamba anaowalenga ni watu wenye uwezo wa kutofautisha baina ya ukweli na uzandiki. Baada ya kuyasoma makala ya Kinana nilijiuliza: Dhamira yake ilikuwa nini kwa kuandika makala hayo yenye maudhui ya kutisha? Hitimisho langu ni kwamba Kinana hakuwa na nia njema kwa Tanzania, na hasa kwa Zanzibar. Huenda akawa anadhamiria kuuchimba mchakato wa demokrasia nchini Tanzania. Makala yake yalinikumbusha hotuba aliyoitoa mwaka jana huko Gombani ya Kale, kisiwani Pemba. Hotuba hiyo ilinichochea kuandika makala katika gazeti hili (“Hiki kiburi cha Kinana kina nini?”,Raia Mwema, Toleo la 351).

Niliandika kwamba hotuba yake ya Gombani ya Kale, ilikuwa ya kusikitisha na ilikuwa na matamshi ya namna mbili: “ya uzushi mtupu” na “yaliyoubiruwa ukweli”. Vivyo hivyo, makala yake ya majuzi kwenye blogi ya The Hill. Mna mengi katika makala hayo yasiyo ya kweli.

Kwa ufupi, yanashutumu kwamba wale wasichana wawili wa Kiingereza, Katie Gee na Kirstie Trup, walioshambuliwa kwa kumiminiwa tindikali huko Zanzibar 2013 walishambuliwa na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki), maarufu kwa jina la “Uamsho”; kwamba Uamsho ni “kundi la kigaidi lenye funganisho zinazojulikana na Boko Haram” na kwamba kwa msaada wa polisi wa Uingereza na Shirika la Polisi la Kimataifa, Interpol, “wanachama” wa Uamsho walikamatwa kwa kosa hilo la jinai na hivi sasa wameshtakiwa mahakamani. Kama huo si uzandiki basi ni nini? Tunaofuatilia siasa za Tanzania tunajuwa kwamba viongozi wa Uamsho wamekamatwa kwa sababu za kisiasa. Wametiwa ndani ili wasiweze kuendelea na kampeni dhidi ya muundo wa sasa wa Muungano na kwamba uchaguzi utapomalizika wataachiwa.

Hii ni mara ya mwanzo ulimwengu kusikia kwamba Jumuiya ya Uamsho ina uhusiano na Boko Haram, kundi la kigaidi lenye chimbuko lake Nigeria. Hii ni shutuma ya kitoto na ni ya uchochezi. Inastahiki kulaaniwa na wote wale wenye kufanya jitihada za kijitu uzima za kupambana na ugaidi wa kimataifa. Vita dhidi ya ugaidi ni mapambano yasiyo na utani, yanayohitaji busara, ukweli na moyo wa dhati kupambana nao.

Hii pia ni mara ya mwanzo ulimwengu kusikia kwamba masheikh wa Uamsho waliokamatwa Zanzibar na kupelekwa Dar es Salaam wanashtakiwa kwa kosa la jinai la mashambulizi dhidi ya wale wasichana wawili wa Kiingereza. Kinana amesahau kusema kwamba masheikh hao, wenye kuheshimiwa na waumini wa dini yao, wameyaambia mahakama jinsi walivyoteswa na hata baadhi yao kulawitiwa wakiwa kizuizini. Mark Trup, baba wa mmoja wa wasichana hao, ameliambia gazeti la Evening Standard la London wiki iliyopita kwamba maneno ya Kinana ni “upuuzi mtupu” au ameyasema kwa sababu za kisiasa. Salum Msangi, kaimu mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai huko Zanzibar, amekanusha kwamba kuna watu waliokamatwa kwa shambulio hilo.

Hii ni aibu kubwa kwa kiongozi kama Kinana kuambiwa kwamba anasema uongo hasa kwa jambo nyeti kama hili. Na ikiwa anathubutu kudanganya kwa jambo kama hili tunawezaje kumuamini kwa mengine? Kinana ameendelea kuandika kwamba Jumuiya ya Uamsho ina historia ndefu ya kuwalenga wageni na hata viongozi wa kidini wa Kikristo na wa Kiislamu “wasiounga mkono lengo lao la kuuvunja Muungano wa Tanzania kwa ugaidi na kuigeuza Zanzibar iwe ni dola yenye itikadi kali”. Kinana ameshutumu kwamba Edward Lowassa, anawaunga mkono magaidi na kwamba ameahidi kuwa akichaguliwa Rais atawaachia huru wale waliokamatwa kwa kufanya shambulio la tindikali. Huku ni kuupindua ukweli kwani Kinana hakueleza yote aliyoyasema Lowassa kwamba watuhumiwa hao, waliopelekwa Tanzania Bara kinyume cha sheria, wataachiwa huru huku kesi yao ikiendelea mahakamani.

Kinana amesahau kwamba katika mfumo wa utawala wa kisheria mtu huwa hana hatia mpaka atapohukumiwa na mahakama kwamba ana hatia. Na huo tujuavyo ndio msimamo wa Lowassa. Anapolijadili suala hili Kinana anajikanganya. Mara anasema kwamba viongozi wa Uamsho ndio waliofanya shambulio la tindikali, mara anasema kuwa wao “wanashukiwa” kwa shambulio hilo, ilimradi inavyoonyesha ni kwamba hajui anasema nini. Lakini sisi tunajuwa anachotaka kusema. Anachotaka kusema ni kuutahadharisha ulimwengu, hasa wa nchi za Magharibi na hususan Marekani, usiuvumilie ushindi wa Lowassa, kwamba Lowassa akishinda Tanzania itakuwa medani ya magaidi.

Labda anayataka madola hayo yaingilie kati iwapo Lowassa na Ukawa watashinda uchaguzi au labda chama chake cha CCM kinajiandaa kuchukua hatua ovu za kuupindua ushindi huo endapo ukitokea. Labda anayataka madola hayo yakionee huruma chama chake kikichukuwa hatua hiyo. Baada ya kushindwa kuwatisha wananchi wa Tanzania, Kinana ameona bora awageukie wageni na aanze kuwatisha wao. Na kwa nini basi akaona haja ya kuwatisha? Kwa sababu, na haya ameyaandika yeye mwenyewe, “kuna uwezekano ingawa kwa sasa ni mdogo wa Lowassa na wafuasi wake wa upinzani kushinda” katika uchaguzi na hivyo Tanzania kuwa medani mpya ya magaidi.

Hii ni mantiki isiyoingia akilini. Sitoshangaa nikisikia kwamba makala ya Kinana, yasiyo na kichwa wala miguu, yalipachikwa kwenye gazeti la The Hill kwa msaada wa ofisi ya wapigadebe iliyo Barabara ya K na yenye lengo la kuwashawishi wabunge wa Marekani wauone upinzani wa Tanzania kwa macho mengine na waione Zanzibar kuwa ni nchi yenye kuwafuga magaidi na kwamba magaidi hao watajititimua pale upinzani utapokishinda CCM katika uchaguzi ujao.

Jengine analolisema Kinana ni kwamba Lowassa alikataliwa na wapiga kura alipojaribu kutaka ateuliwe na CCM awe mgombea wake katika uchaguzi wa urais. Ukweli ni kwamba bado hatujui iwapo Lowassa atakubaliwa au atakataliwa na wapiga kura. Tujuavyo ni kwamba alikataliwa na vigogo wa CCM, au hasa na “the system”, lile niliitalo “dubwasha” lenye kuiongoza serikali na CCM. Wapigaji kura, wananchi wa kawaida, bado hawakutoa uamuzi wao. Utakuwa bayana Oktoba 25.

Kinana ametaja shutuma za ufisadi zinazomuandama Lowassa na kwamba alilazimika kujiuzulu uwaziri mkuu kwa sababu ya ufisadi. Kinana amesahau kwamba hadi leo Serikali ya CCM haikumfikisha mahakamani Lowassa na kwa hivyo, mbele ya macho ya sheria Lowassa hana hatia. Yeye mwenyewe Lowassa amekwishajitetea kwa kusema ya kwamba alijiuzulu uwaziri mkuu kwa sababu ilibidi awajibike kisiasa na alifanya hivyo kuilinda Serikali ya CCM. Zaidi ya mara moja amesema ya kwamba alihusika na sakata la Richmond “kwa maagizo kutoka juu”.

Angekuwa mkweli Kinana angeutaja ufisadi uliozagaa katika ngazi za juu kabisa za Serikali ya Tanzania, pamoja na ule unaohusika na biashara ya kusafirisha kwa magendo pembe za ndovu nje ya nchi. Ni ufisadi huo uliolifanya Shirika la Serikali ya Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) likatae Alhamisi iliyopita kuipa Tanzania shilingi zaidi ya trilioni moja (sawa na dola za Marekani milioni 472.8). Fedha hizo zingetumika kugharimia miradi kadhaa katika sekta ya nishati.

Kwa makala yake katika The Hill Kinana hajajitendea haki yeye mwenyewe wala chama chake wala wapigakura wa Tanzania ambao kura zao chama chake kinazisaka. Inanibidi niulize tena swali nililoliuliza katika makala ya toleo la 351 la Raia Mwema: “Kwa nini kiongozi wa hadhi kama ya Kinana akawa haoni taabu usiku kuuita mchana na mchana kuuita usiku?” Uongo mchana kweupe! Hatutochoka kuuliza: Kinana, kwa nini? Kwani kunani? Chambilecho mshairi wa Kenya Abdilatif Abdalla:

“Kana na kuku kunena, kunenwa k’akutakiwi
Kuna wanakokuona, kunena kwamba si kuwi
Kunena wakikuona, kukuita k’awakawi
Kunena kana kwanuk’a, nikukome kukunena?”

CHANZO: RAIA MWEMA

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.