MAKALA yangu ya mwisho ilieleza kirefu kidogo kuhusu michakato ndani ya chama-tawala, jinsi ambavyo haijali sana kuwatendea haki wote wanaosaka nafasi katika chama hicho na ni kwa nini baadhi ya hao wanaohisi hawakutendewa haki, kujitoa ndani ya chama hicho na kujiunga na upinzani.

Shauri la Edward Lowassa bila shaka linachukua nafasi ya juu kabisa katika hili, lakini wako wengi wengine. Yupo waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, makamu wa rais, Gharib Bilal, Jaji Mkuu mstaafu, Augustine Ramadhani na wengine wengi wanaoweza kuitwa Watanzania waandamizi, na ambao, kama wote wangependa kusema ya moyoni, wangesema kwamba hawakutendewa haki.
Kama nilivyokwisha kusema, kutotendeana haki si jambo jipya ndani ya chama hicho, na hili nililieleza kwa kutoa mifano inayotokana na historia ya CCM. Nilieleza, hata hivyo, kwamba kilichobadilika hapa ni kwamba makada wa chama hicho, kwa mara ya kwanza wamejenga uthubutu ambao ulikuwa haujazoeleka hadi sasa.
Hii ina maana kwamba makada kama John Malecela walikuwa wanajua kwamba wameonewa lakini hawakuwa na uthubutu huo. Chama kingeweza kufanya lolote kumhusu kada yeyote, na kada huyo akakubali sudi yake kama vile imetoka kwenye mamlaka isiyopingika. Huo ndio utamaduni uliojengwa na TANU na baadaye CCM chini ya Julius Nyerere. Huo ndio utamaduni ulioendelezwa na warithi wa Nyerere hadi leo hii.
Ni utamaduni ulioshindwa kuinua macho yake na kuangalia ni kwa kiasi gani mambo yamebadilika katika medani ya siasa nchini. Utamaduni huo umeshindwa kabisa kwenda na wakati na kukubali mabadiliko. Wakuu wa chama wanaelekea kuathirika na mgando wa kimawazo unaowafanya wadhani kwamba bado mwaka 1968, wakati mkuu wa chama akiweza kuwafukuza wabunge kwa kitendo kimoja tu cha kuwanyang’anya kadi za chama, na huo ukawa ndio mwisho wao kisiasa.
Hali imebadilika sana. Mosi, hatunaye Nyerere tena, mkuu aliyejiweka katika nafasi adhimu ya watu kumwangalia kwa hofu kutokana na misimamo yake isiyotetereka. Hofu hiyo haikutokana na matumizi ya mabavu kila wakati, ingawaje hata mabavu yalitumika si haba. Zaidi ya mabavu, alikuwa na nguvu ya ushawishi kuliko ushawishi wa nguvu. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja na hoja ikajengeka. Aidha alikuwa na uadilifu uliojionyesha na kumpambanua waziwazi.
Kwa uwezo mkubwa, Nyerere aliweza kuchanganya nguvu za dola iliyokuwa chini yake na ushawishi huo kutekeleza alichotaka kukifanya. Wapo walioumia lakini wakashindwa kumshutumu kwa lolote kwa kuchelea, ama kuonekana kama wasaliti mbele ya umma, ama kutiwa kizuizini, ikiwa ni sehemu ya mabavu aliyotumia Nyerere katika utawala wake.
Pili, sehemu kubwa ya nguvu za Nyerere ilitokana na hali iliyokuwapo ya uelewa mdogo wa watu wetu kuhusu masuala mengi ya kisiasa na kimaendeleo. Watu waliokuw a na sifa za kuwa “wasomi” walikuwa ni wachache, na hao wachache hawakujenga ujasiri wa kubishana na Mwalimu. Baadhi ya wachache waliojenga uthubutu huo walishikiliwa kizuizini. Katika msamiati wa wakati huo, neno “kizuizini” lilikuwa na uzito usio wa kawaida.
Tatu, mfumo wa chama kimoja uliojengwa na Nyerere ulikuwa ndio utamaduni wa nchi karibu zote za Afrika, pamoja na nchi za Uropa Mashariki zilizokuwa chini ya mfumo wa “kijamaa.” Ndiyo maana inakuwa vigumu kumlaumu Nyerere kwa baadhi ya makosa ya wakati huo kwani yalitokana na muktadha wa kisiasa wa wakati huo duniani.
Nne, hata kwa wale waliomlaumu na kumhukumu Nyerere kwa “udikteta” wa kipindi chake madarakani, hakuna aliyewahi kusema kwamba alitenda makosa ya kufinya uhuru wa watu wake kwa nia ya kuwaibia, kujilimbikizia mali au kuitajirisha familia yake. Sote tunajua jinsi familia yake ilivyokuwa ya kawaida kabisa. Leo hatuna uhakika wa hilo kutokana na wembamba wa maadili miongoni mwa familia za watawala wetu.
Tumeingia, taratibu lakini kwa uendelevu, katika utamaduni wa kusaka nafasi na ofisi kwa kutumia fedha na halafu kuzitumia hizo nafasi na ofisi kupata fedha zaidi. Katika kuzisaka hizo nafasi na ofisi, familia zetu zimekuwa ndizo nguzo kuu tunazozitumia na tunazokusudia kuzinufaisha. Kwa jinsi hii, watawala wetu hawana nguvu ya kimaadili inayoweza kuwalinda wanapotaka kufanya uamuzi wa kutowatendea haki wenzao. Wenzao wanao uhuru mkubwa zaidi wa kung’aka na kufoka, na hata kuondoka katika chama na kujiunga na chama kingine. Ndivyo ilivyotokea safari hii.
Tano, kwa kuwa dhana ya chama kwamba ni umoja wa watu wenye itikadi inayofanana, na kwamba itikadi hiyo imejengeka juu ya misingi ya kifalsafa inayoeleweka, imekwisha kufa, hakuna tofauti kati ya chama kimoja na kingine. Kifalsafa na kiitikadi, Chadema na CCM ni kitu kile kile, tukiacha tofauti iliyo dhahiri kwamba kundi moja limo madarakani na kundi jingine lingependa kuliondoa kundi lililomo madarakani ili hili jipya lichukue nafasi yake.
Hili linajidhihirisha pia katika uundwaji wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na hatua zilizochukuliwa ili vyama viachiane majimbo ili kuongeza kasi ya kuiondoa CCM madarakani. Hii ina maana kwamba vyama hivi havina tofauti za kimsingi kisiasa, kiitikadi na kifalsafa. Siasa, itikadi na falsafa ya vyama vyote hivi ni kukiondoa chama kilicho madarakani ili viingie vyenyewe.
Kwa msingi huo, ni halali kabisa kwa Chadema na washirika wake wa Ukawa kumvuta Edward Lowassa na Frederick Sumaye kuja upande wao. Aidha, kwa sababu hiyo hiyo, ni halali kabisa kwa hawa wawili, na wengine waliokwisha kuhama na watakaoendelea kuhama kutoka CCM kwenda Chadema, kutoka Chadema kwenda CUF, kutoka CUF kwenda ACT, na kadhalika. Kwani tofauti baina yao ni nini ukiacha ukweli kwamba huko nyuma walikuwa wakirushiana shutuma?
Ndani ya miaka ishirini iliyopita, tumewaona wanasiasa wakibadili vyama kama mashati, bila haya. Katika miaka hamsini ushey niliyofuatilia “utani” wa timu za Simba na Yanga, ni mtu mmoja niliyewahi kumjua aliyehamisha ushabiki wake kutoka klabu moja kwenda nyingine. Naye aliponzwa na kumpenda msichana kutoka “upande wa pili,” na sharti la uchumba kutoka kwa baba mkwe likawa ni huyo bwana “asilimu.” Lakini kwa vyama kuhama imekuwa ni kila siku.
Sita, tumekwisha kuona kwamba wanasiasa wetu wana kipaumbele kimoja tu, nacho ni kuingia au kubakia madarakani. Kwa wale walio madarakani, chochote kinachoweza kuwafanya waendelee kukaa madarakani ni halali. Kwa wale walio nje ya madaraka, chochote kinachoweza kuwafanya waingie madarakani ni halali. Katika hali ya ukame wa falsafa, ni vigumu kumnyooshea kidole yeyote anayehama kutoka chama kimoja kwenda kingine au anayebakia ndani ya chama ambacho hakifanani na mtazamo wake wa kisiasa. Na hawa ni wengi.
Ni dhahiri kwamba Edward Lowassa anayo nia thabiti ya kwenda Ikulu, na nia hii haijatetereka kwa kipindi cha miongo miwili. Amesuka mitandao iliyotanda kila kona ya nchi. Ni mitandao hiyo hiyo iliyotumika kufanya kampeni kabambe za Jakaya Kikwete miaka kumi iliyopita. Sasa ni jipi la kushangaza?
Chadema na Ukawa wanataka, tena sana, kuing’oa CCM madarakani. Lowassa anataka, tena sana, kuingia Ikulu, ndoto yake ya zaidi ya miaka ishirini. Huu ni ubia unaotupa taswira ya msukumo mkubwa ambao CCM itakuwa na kibarua kigumu kuuzuia.
Tayari yamejitokeza matamko ya wakubwa ndani ya chama-tawala yanayodhihirisha kwamba kuna mtafaruku. Kuna maneno ambayo yakisemwa na mtu mzima jamii inajiuliza kulikoni. Ni maneno ya mtu anayeshindwa kujiamini kutokana na mfadhaiko uliosababishwa na tukio au hali ambayo hakutarajia. Lakini hadi sasa hakuna jambo lililotokea ambalo lisingetabirika.
Tukiacha na kuweka mbali uzandiki, tunaweza kukumbuka mambo ya msingi tuliyojifanya kuyasahau, mambo ambayo yana umuhimu mkubwa, si tu katika siasa, bali katika maisha mapana.
Kwanza ni umuhimu wa kuwa wakweli kwa kiasi kinachowezekana. Pili ni kuheshimiana sote kwa misingi ya utu. Tatu ni kutendeana haki kadri tunavyoweza na kuacha tabia ya kuchagua wapi tutende haki na wapi tuipige haki teke. Nne ni kutetea haki hiyo pale ambapo haituhusu moja kwa moja.
Haya yametoweka kabisa ndani ya CCM, na chama hicho kinaendeshwa kwa imla ya mwenyekiti wake. Ikiwa hivyo kinaacha kuwa chama, kinageuka kuwa kampuni binafsi. Kitakimbiwa na wengi.
Chanzo: Makala ya Jenerali Ulimwengu kwenye Raia Mwema, 9 Septemba 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.