Kiu ya Wazanzibari kubadili mfumo wa Muungano ilikatishwa bila kusinzwa na wakalazimishwa kunywa mate yao na Bunge Maalum la Katiba mwishoni mwa mwaka jana. Ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kuwa angeliondoka na kuiwacha Jamhuri ya Muungano ikiwa na Katiba Mpya ni miongoni mwa ahadi zake zilizofeli.

Lakini uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka huu unaonekana kuwa na majibu kwa Wazanzibari waliopigania mageuzi ya kimsingi kwenye uendeshaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa takribani nusu karne nzima ya uhai wa Muungano wenyewe. Kuna uwezekano wa mabadiliko ya kiutawala.

Ni wao, Wazanzibari, ndio ambao tangu miaka ya awali wamekuwa wakijitokeza kila mara kupinga hiki na kukataa kile, lakini upinzani wao ukawa unakabiliwa na kiburi cha Kaka Mkubwa, ambaye anajiona ana nguvu za kutosha dhidi ya nduguye za kuweza kufanya na kupata analotaka kwenye mahusiano yao.

Namna mchakato wa kupatikana katiba ulivyoendeshwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kulizaa majibu ambayo leo Wazanzibari yamewapa fursa ya kufanya mageuzi wanayotaka, ikiwa tu wataupita uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa salama na amani.

Kupitia Bunge hilo, ambalo mijadala yake ilioneshwa moja kwa moja na televisheni, Wazanzibari walipata ramani ambayo wangeliweza kuitumia kufika wapatakapo. Kuliwapambanua nani ni nani na nani anasimamia nini kwenye muktadha huu. Waliokuwa wamesimama pamoja na kwa ajili ya ajenda ya Zanzibar walijiweka wazi kama ilivyokuwa kwa wabunge kutoka Zanzibar ambao walikuwa kinyume cha ajenda hiyo. Vyama viwili vikuu vinavyoongoza siasa za Zanzibar – Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) – vilijianika wazi kwa namna ambayo haikuwahi kujitokeza huko nyuma. Alimradi mpaka Bunge linamalizika, tayari Wazanzibari walishajuwa nini wangelikifanya baadaye.

Ndio maana si jambo la ajabu hata kidogo kwamba CCM na serikali zake ziliamua kuwa wasingeliweza kwenda kwenye Kura ya Maoni kuamua juu ya Katiba Iliyopendekezwa kabla ya kwanza kuupisha uchaguzi mkuu. Walizisoma, ingawa kwa kuchelewa, nyoyo za Wazanzibari. Mbinu ya CCM hapa ilikuwa ni kuuwacha muda utibu majeraha ya Bunge la Katiba nyoyoni humo, kisha wajilete upya baadaye. Tena ikashindwa kuzisoma nyakati.

Kuahirisha kura ya maoni na kuutanguliza uchaguzi mkuu kungelikuwa na maana tu kwa CCM, endapo ingelikuwa kwenye Bunge la Katiba iliweza kuonesha sura tafauti na iliyoonesha. Lakini baada ya yote yaliyotokea bungeni Dodoma, hakuna mbinu nyengine yoyote ambayo ingelitosha ’kuziroga’ tena nyoyo za Wazanzibari. Na hilo CCM inalijuwa vyema. Kwamba tangu wakati huo imeshawapoteza Wazanzibari moja kwa moja na kuwarejesha haiwezi tena.

Habari za ndani ya CCM zenyewe zinasema kuwa chama hicho kilielezwa waziwazi hayo na wataalamu wake kwenye vikao vyao, baada ya wataalamu hao kuombwa na viongozi wa juu wa CCM kuwafanyia tathmini ya kwa nini ufuasi wake unashuka. Waliambiwa mambo manne yanachangia, na la juu kabisa kwenye orodha ni namna ambavyo waliliendea na kulitendea Bunge la Katiba. Msimamo wa CCM kwenye Bunge hilo, waliambiwa, umekijeruhi laisalkiasi visiwani Zanzibar kufika umbali wa kwamba hata kule kwenye ngome zake – kusini ya Unguja – nako hakuwezi tena kuaminika kuwa sehemu salama kwa chama hicho.

Bahati mbaya kwake, ni kuwa viongozi wa Zanzibar ambao wamebatizwa jina la “madalali“ hawana la kufanya tena. Hawawezi kuyafanyuwa waliyoyafanya Dodoma. Hawawezi kuirejesha rasimu bungeni kubadili mambo. Walichodhani wangeliweza kukifanya kilikuwa ni kuwatuma waliokuwa wajumbe wa bunge hilo kurudi kwa wananchi kuwaeleza yale mazuri ambayo yamo kwenye Rasimu Iliyopendekezwa, lakini majibu waliyoyakuta kwa wananchi yakawatisha na kuwaangusha zaidi. Mikutano ikasusiwa.

Wazanzibari, bila kujali vyama vyao, wamegeuza mgongo kwa kila wanayedhani amewachuuza na kuichuuza dhamira ya nchi yao kuwa taifa huru lenye uwezo wa kujiamulia na kujitendea ndani ya Jamhuri ya Muungano. Na muda wote huo wamekuwa wakiitumia kila fursa wanayoipata kuelezea hilo kwa vitendo. Ndio maana idadi ya wanachama wa CCM wanaokihama chama hicho ndani ya kipindi hiki tangu Bunge Maalum la Katiba limalizike ni kubwa zaidi kuliko waliowahi kufanya hivyo ndani ya kipindi cha miaka mitano kabla.

Wazanzibari wamefanya hivyo pia kwenye uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu, ambapo wengi wa waliojitokeza walikuwa vijana wa umri ya kati ya miaka 20 na 25, ambao huu wa mwaka huu huenda ukawa uchaguzi wao wa kwanza au wa pili tu kupiga kura. Kwao wao, demokrasia ilianza baada ya uchaguzi wa tatu wa vyama vingi, na hawana mawaa ya chaguzi za kabla ya hapo. Hawana woga wa 1995 wala wa 2000. Wana dhamira ya 2015.

Ndio maana kwa mara ya kwanza, CCM ililazimika kutumia nguvu kuandikisha wasiostahiki kuandikishwa hata kwenye majimbo ya mkoa wa Kusini Unguja, ngome yake kuu na chaka kubwa la kushinda chaguzi zilizotangulia. Ndio maana pia, hata kwenye kura za maoni kuwatafuta wagombea hao hao wa CCM zilizomalizika hivi karibuni, mwangwi wa kilichotokea Bunge la Katiba ulisikika kwa mbali. Tena nguvu ikapaswa kutumika dhidi ya wana-CCM wenyewe, achilia mbali rushwa na vitisho.

Wazanzibari wanaingia kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba wakati nchi ikiwa imevimba kote kote. Upande wa Tanzania Bara, ambako kawaida CCM ilikuwa haikumbani na upinzani wa kutisha sana, mwaka hu uni tafauti. Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umemsimamisha kada wa zamani wa CCM, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa, kuwa mpeperusha bendera ya urais. Wimbi la wana-CCM kuhama chama hicho na kumfuata Lowassa aliko halijawahi kushuhudiwa ndani ya miaka yote 20 ya chaguzi za vyama vingi.

Kwa mara ya kwanza, nako CCM inajikuta ikilazimika kutumia mbinu ilizokuwa ikizitumia Zanzibar miaka yote kupambana na upinzani. Dalili ni kuwa, kwa mara nyengine tena, CCM inazisoma vibaya alama za nyakati. Kwamba watu wa Tanzania Bara wanatafautiana sana na Wazanzibari kwenye suala la kukabiliana na nguvu ya dola.

Wakati Naibu Mkuu wa Polisi, Abdullah Kaniki, alipozuia vyama visikusanye umma wa wananchi kwenye shughuli za kuchukuwa na kupeleka fomu za ugombea pamoja na kusaka wadhamini mikoani, alijikuta amri yake ikidumu kwa masaa manane tu baada ya kutolewa, baada ya hapo ikavunjika yenyewe vipande vipande, pale umati mkubwa usiowahi kushuhudiwa mkoani Mbeya siku ya pili yake.

Mambo yana zama na zamu, kama alivyowahi kusema aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, siku hizo akizungumzia kuwa bado zama za wapinzani kuongoza Zanzibar hazikuwa zimefika. Sasa uchaguzi wa 2015 una uwezekano mkubwa sana wa kubadilisha zamu maana zile zama zimeshafika. Watilkal ayyaam…..

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.