Kama halitotokea la kutokea, basi tarehe 25 Oktoba mwaka huu Wazanzibari wataelekea tena kwenye vituo vya kupigia kura kushiriki katika uchaguzi wa tano wa vyama vingi tangu mfumo huo uliporejeshwa tena nchini mwao mwaka 1992. Katika chaguzi zilizopita za 1995, 2000, 2005 na 2010 utashi na ushabiki wa vyama, ndio uliotoa muelekeo mkubwa zaidi wa upigaji kura wa watu. Lakini hali ni nyengine kabisa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Matukio yaliyojiri ndani ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla katika muda wa karibu miaka mitatu sasa yameufanya uchaguzi huo uwe na sura ya kipekee inayotajwa na wanasiasa wa Chama cha Wananchi (CUF) kuwa ni ya ‘mwaka wa maamuzi’. Matukio yote hayo yamekusanywa ndani ya kapu moja la mchakato wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mchakato ambao umeibua tena kile kinachozungumzwa sasa kuwa ni Ajenda ya Zanzibar ndani ya Muungano.

Ni dhahiri sasa kuwa Ajenda ya Zanzibar ndiyo itakayosimamia maamuzi ya kila Mzanzibari mpiga kura. Ni ajenda hiyo ambayo Wazanzibari walijaribu bila mafanikio kuifanikisha wakati walipotoa maoni yao mbele ya Tume ya Marekebisho ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba. Ajenda ya Zanzibar ni kupigania muungano wa uadilifu, wa haki sawa na usio na ujanja, magube, ulaghai, ubabe, dharau na unyonyaji kati ya nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, yaani Tanganyika na Zanzibar.

Kinyume na upotoshaji ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi wa CCM wa pande zote mbili za Muungano wa kutaka kuonesha kuwa dai la Zanzibar la kutaka kuwa na muungano wa haki na usawa wa serikali tatu ni chokochoko zilizoanzishwa wapinzani wenye nia ya kutaka kuuvunja Muungano, na hasa chama cha CUF kwa upande wa Zanzibar, Wazanzibari wengi sasa wanajua kwamba mtu wa kwanza aliyesimama kutetea mamlaka ya Zanzibar ndani ya mfumo wa Muungano uliopo wa serikali si mwengine ila ni Mzee Abeid Amani Karume, mmoja wa waasisi wawili wa muungano huo.

Kabla hata haujatimiza miaka 10, Mzee Karume alibaini kasoro ya muungano wa kijanja uliopo, akaamu kufunga safari na timu ya baraza lake la mawaziri kuelekea Tanganyika na kumkabili mwasisi mwenzake wa Muungano Mwalimu Julius Nyerere akimtaka airejeshee Zanzibar mambo ya msingi ya mamlaka yake iliyoyasabalia kwenye muungano huo. Jaribio lake halikufua dafu.

Lakini hilo halikuizika wala kuisahaulisha Ajenda ya Zanzibar ndani ya muungano wa Tanzania; kwani mrithi wake wa urais wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi alimpokea kijiti na kuendeleza mbio hizo. Wakati Mzee Karume alidai mamlaka zaidi, Mzee Jumbe aliliandama tatizo la msingi la muungano, yaani MUUNDO wake. Na kwa kuwa alikuwa mmoja wa mashahidi wa muungano huo ulipoasisiwa, kwa mara ya kwanza akataka muungano urejeshwe kwenye muundo wake halisi uliokusudiwa, yaani Muungano wa Serikali Tatu. Yaliyompata Mzee Jumbe kwa kusimamia ajenda ya Zanzibar yanajulikana na Wazanzibari wote.

Pamoja na hayo ajenda ya Zanzibar haikufa pia, na mara baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, Chama cha Wananchi (CUF) kikaifufua tena ajenda hiyo kwa kutangaza rasmi ndani ya katiba yake kuwa msimamo wake kuhusu Muungano ni kupigania muungano wa serikali tatu. Na kwa muda wote tangu kuasisiwa kwake kimekuwa kikiuhamasisha umma wa Wazanzibari kusimamia kwa pamoja ajenda hiyo iliyowekewa jiwe la msingi na marais wa kwanza na wa pili wa Zanzibar.  Na naam Wazanzibari walihamasika pale Rais Kikwete alipotangaza uamuzi wa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Wazanzibari waliowengi walidhihirisha kuwa wamepevuka na kukomaa kiuzalendo, kiuono na kisiasa na wakatamka bila ya kutafuna maneno kuwa wanataka nchi yao irejeshewe mamlaka yake kama alivyodai kwa mara ya kwanza Mzee Karume, yaani kuwa na Muungano wa Mkataba. Tume ya Katiba ya Jaji Warioba iliutambua ukweli huo, lakini baada ya kuchambua maoni ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano na ili kupata maridhiano ya kitaifa wakaisimamia hoja ya Mzee Aboud Jumbe Mwinyi ya kuwa na muungano wa serikali tatu.

Kama inavyojulikana ulimwengu mzima kuwa suala la Katiba ni suala la kitaifa, ni suala la wananchi kwa ujumla wao, lakini CCM, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jakaya Mrisho Kikwete iliupora mchakato wa katiba ya Watanzania na kuyatia kapuni maoni ya wananchi iliyoona yanakinzana na sera na maslahi ya chama hicho. Ikawafanya Watanzania walio wengi kuwa ni wajinga wasiojua wasemalo na badala yake ikapitisha Katiba kulingana na utashi wa chama hicho ambayo ni ya kuendeleza mfumo uliopo wa Muungano wa serikali mbili. Bahati nzuri katiba hiyo ambayo rasimu yake ilipitishwa kiharamu na kinyume cha sheria kwa kukosa theluthi mbili ya kura za Zanzibar, bado haijapigiwa Kura ya Maoni.

Kwa yaliyotokea Dodoma Wazanzibari wamepoteza imani kikamilifu kwa CCM Zanzibar kwamba inaweza kusimamia na kutetea Ajenda ya Zanzibar ndani ya Muungano. Wametambua kwamba si wao Wazanzibari wa sasa tu waliosalitiwa na viongozi wa CCM Zanzibari,  lakini walichokifanya wanasiasa hao Dodoma ulikuwa ni uhaini kwa Mzee Karume na Mzee Jumbe, waasisi wa Ajenda ya Zanzibar ndani ya Muungano.  Kwa msimamo wao wa wazi kabisa waliouonyesha Ddodoma viongozi hao wamewatamkia kinagaubaga Wazanzibari kwamba, kwao wao “chama kwanza nchi baadaye” au kwa usahihi zaidi maslahi kwanza mengine yote baadaye.

Wazanzibari wamebaki vinywa wazi, wakijiuliza bila ya kupata majibu, kwamba kwa nini CCM imeipinga Rasimu ya Jaji Warioba inayomfanya Rais wa Zanzibar awe na hadhi sawa na Rais wa Tanganyika? Kwa nini wamekataa Zanzibar kuwa na hadhi sawa na Tanganyika kama nchi mbili washirika katika Muungano wa Shirikisho la Serikali Tatu uliopendekezwa na Rasimu iliyotokana na maoni ya wao wananchi wenyewe?  Na badala yake kuridhia nchi yao iendelee kuwa maamuma tu ndani ya Muungano?

Kwa nini wamekataa mawaziri wa nchi yao wasiwe na hadhi sawa na wa Tanganyika badala ya ujanja na unyonyaji unaoendelea kufanywa hivi sasa kwa mawaziri wa kilimo, afya, uchukuzi, viwanda na elimu a Tanganyika kulitumia jina la Tanzania kimataifa kwa maslahi ya upande mmoja tu wa muungano ilhali kisheria hadhi ya mawaziri hao ni sawa na ya mawaziri wenzao wa Zanzibar wa wizara hizo zisizo za Muungano?

Wanapoyatafakari yote hayo ndipo wanapohisi kuwa si mwanga wa matumaini, bali ni giza totoro ndilo litakalougbika mustakabali wa Zanzibar kwa nusu karne ijayo kama si zaidi, endapo watairuhusu CCM iendelee kubakia madarakani na kuipitisha Katiba Inayopendekezwa. Baada ya kushuhudia yaliyowasibu wana CCM kindakindaki, kina Mzee Hassan Nassor Moyo na Mansour Yusuf Himidi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Othman Masoud na mashekhe wao kwa sababu ya kusimamia ajenda ya Zanzibar sasa Wazanzibari wameng’amua kuwa si kweli hata chembe kuwa Ajenda ya Zanzibar, dai la kupigania Muungano wa haki, wa heshima, wa uwazi na wa kiadilifu ni la mvutano baina ya CCM na CUF. Hili sasa Wazanzibari wote wanalielewa barabara ukiacha wale wachache wanaojifanya mbumbumbu wa kutotaka kuelewa.

Wazanzibari wanaamini kuwa kukichagua Chama cha Wananchi (CUF) chenye sera rasmi ya kutetea na kuisimamia Ajenda ya Zanzibar katika Muungano, na ambacho kilidhihirisha hivyo kivitendo wakati wote wa mchakato wa Katiba ndiko kutakakoinusuru nchi yao. Wanajua kwamba Oktoba 25 ni fursa ya dhahabu kwao ya kuleta mabadiliko, vitakayojivunia vizazi na vizazi vijavyo. Fursa ambayo wakiipoteza itabaki kuwa ndoto, pengine karne nzima ijayo. Na hilo litakuwa ni kosa la kihistoria ambalo hawaonyeshi kuwa wako tayari kulifanya.

*Makala ya Khamis Mzee.

One thought on “Wa 2015 sio tu uchaguzi mkuu, bali uchaguzi mkubwa kwa Z’bar”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.